1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano mengine makubwa yafanyika Misri

19 Julai 2013

Jeshi la Misri limeimarisha ulinzi kwenye majengo ya serikali katika siku ambayo kundi la Udugu wa Kiislamu na wapinzani wao wamepanga maandamano makubwa kutetea misimamo yao juu ya kupinduliwa kwa Mohamed Mursi.

https://p.dw.com/p/19Af4
Supporters of deposed Egyptian President Mohamed Mursi hold posters during a protest outside Rabaa Adawiya mosque in Cairo July 9, 2013. Egypt's interim President Adli Mansour on Tuesday named liberal economist and former finance minister Hazem el-Beblawi as prime minister in a transitional government, as the authorities sought to steer the country to new parliamentary and presidential elections. The posters read, "No substitute for the legitimacy." REUTERS/Louafi Larbi (EGYPT - Tags: POLITICS CIVIL UNREST)
Ägypten Unruhen Pro Mursi Anhänger 9. Juli 2013Picha: Reuters

Wanajeshi wanaripotiwa kuweka vizuizi kwenye barabara zote muhimu kuelekea mji mkuu, Cairo, ambako ndiko kitovu cha maandamano ya makundi mawili yanayopingana nchini Misri.

Jeshi limesema linajaribu kuzuia kuingizwa kwa silaha na sio kuzuwia maandamano, ingawa pia limeshaonya kwamba litatutumia nguvu ikibidi, dhidi ya waandamanaji watakaoleta fujo.

Rais wa serikali ya mpito, Adli Mansour, aliapa kwenye hotuba yake ya jana kwamba angeilinda nchi dhidi ya kile alichokiita "machafuko":

"Tunafahamu fika kwamba wale wanaotaka kufuata njia ya umwagaji damu kwa mabango ya uongo na madai ya uongo. Wanataka kulidhalilisha taifa, kwa imani kwamba wakifanyacho ni sahihi." Alisema Mansour kupitia televisheni ya taifa ya Misri.

Ingawa hakuwataja majina, ni wazi kwamba Mansour alililenga kundi la Udugu wa Kiislamu, ambalo limeyaita maandamano ya leo kuwa "ya kelele kali" nchini kote Misri, likidai kurudishwa madarakani kwa Mursi.

Chama cha Kisalafi chaonya

Tayari chama cha Kisalafi, washirika wa zamani wa Udugu wa Kiislamu waliomgeuka Mursi na kuunga mkono mapinduzi ya kijeshi dhidi yake, kimeshazionya pande zote mbili kuutatua mgogoro huu unaozidi kukua kwa amani.

Wafuasi wa Mohamed Mursi kwenye maandamano mjini Cairo.
Wafuasi wa Mohamed Mursi kwenye maandamano mjini Cairo.Picha: Getty Images

"Ninaamini kwamba Udugu wa Kiislamu wanapaswa kukifahamu kipindi hiki tulichonacho, ili wawe sehemu yake. Wakati huo huo, naamini wale walio madarakani wanapaswa kung'amua kwamba kuzidisha shinikizo dhidi ya Udugu wa Kiislamu na kuzidharau hisia za wafuasi wake kutakuwa na matokeo mabaya kabisa." Alisema Nader Bakar, msemaji wa chama hicho cha Nur.

Hapo jana, Umoja wa Afrika nao ulieleza wasiwasi wake kwa hali ya Misri, ukisema nchi hiyo itatumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe, ikiwa kundi la Udugu wa Kiislamu halikushirikishwa kwenye mchakato unaoendelea.

Kati ya nafasi 33 kwenye baraza jipya la mawaziri, Udugu wa Kiislamu hawana nafasi hata moja, ingawa kundi hilo lenyewe lilishasema kwamba haliitambui serikali iliyopo.

Maandamano "dhidi ya magaidi"

Makundi yanayoitwa "ya kiliberali" yanafanya maandamano yake kwenye uwanja maarufu wa Tahriri, wakishinikiza utekelezwaji wa mpango uliotangazwa na jeshi unaoelekeza namna nchi hiyo itakavyorudi kwenye utawala wa kiraia.

Rais wa muda wa Misri, Adly Mansour.
Rais wa muda wa Misri, Adly Mansour.Picha: Khaled Desouki/AFP/Getty Images

Miongoni mwa yaliyomo kwenye mpango huo ni kuifanyia marekebisho katiba iliyopitishwa kwenye kura ya maoni ya mwaka jana na kuungwa mkono na Udugu wa Kiislamu, na kuitisha chaguzi za bunge na uraisi ndani ya miezi tisa kutoka sasa.

Vuguvugu la Tamarod, ambalo ni moja ya makundi hayo ya wapinzani wa Mursi, limeyaita maandamano yake kuwa ni dhidi ya "magaidi", wakiwalenga Udugu wa Kiislamu, wanaowashutumu mwa mkururo wa mauaji ya maafisa wa usalama kwenye eneo la Sinai, linalopakana na Israel, ambako tangu Mursi aondoshwe madarakani, maafisa watatu wameshauawa.

Tangu jeshi kumuondoa madarakani Mursi hapo tarehe 3 mwezi huu, watu kadhaa wameshauwa. Miongoni mwao ni wafuasi 51 wa Udugu wa Kiislamu waliopigwa risasi na jeshi mbele ya makamo makuu ya Kikosi Maalum cha Jeshi mjini Cairo, ambapo walikuwa wakiandamana kutaka Musri aachiliwe.

Jeshi limeyaelezea mauaji hayo kwamba yalikuwa ya kujilinda, baada ya kushambuliwa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/dpa
Mhariri: Saumu Yusuf