1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano makubwa Misri

22 Juni 2012

Wananchi wa Misri wanajiandaa na maandamano makubwa leo katika mji Mkuu wa Misri, Cairo, wakilitaka Baraza la Kijeshi Kukabidhi madaraka kwa utawala wa Kiraia.

https://p.dw.com/p/15Jdi
Maandamano
MaandamanoPicha: DW

Chama cha Udugu wa Kiislamu, makundi kadhaa pamoja na wananchi wa Misri wamekusanyika katika uwanja wa al-Tahrir ambao ni uwanja muhimu wa harakati za kisiasa wenye kumbukumbu za kuuondoa madarakani utawala wa Hosni Mubarak Februari mwaka Jana.

Akizungumzia hilo msemaji wa chama cha Udugu wa Kiislamu, Aiman Sedek, alisema,"Tunatamka bayana kuwa tunapinga kifungu cha ziada cha katiba na kuwa Baraza kuu la Kijeshi likabidhi madaraka mara moja kwa rais aliyechaguliwa."

Baraza hilo la Kijeshi kwa sasa lina majukumu makubwa, likiingoza serikali na kukiwa hakuna Bunge mara baada ya hukumu ya mahakama kulifuta Bunge la taifa hilo.

Afisa uchaguzi akihesabu kura baada ya uchaguzi wa duru ya pili
Afisa uchaguzi akihesabu kura baada ya uchaguzi wa duru ya piliPicha: dapd

Subira ya matokeo ya uchaguzi

Maandamano ya leo yanaungwa mkono na wanaharakati wengi waliokusanyika katika uwanja huo, huku wananchi wote wa Misri wakiwa na shauku kujua matokea ya üchaguzi wa urais yaliyofanyika tarehe 16 na 17 baina ya Mohammed Morsi kutoka chama cha Udugu wa Kiislamu, na Ahmed Shafiq, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa mwisho wa Hosni Mubarak kabla ya kuondolerwa madarakani.

Matokeo uchaguzi yana ishara kuwa Mohammed Mursi anaweza kutangazwa mshindi. Tume ya uchaguzi imesema imeshindwa kutangaza matokeo hayo jana kwa kuwa ilitaka kupata nafasi ya kushugulikia malalamiko yaliyowasilishwa na wagombea wote wa nafasi ya urais.

Maoni ya waandamanaji kwa Mubarak

Wakati hali katika medani ya siasa ikiwa hivyo, hali ya Afya ya mfungwa wa maisha ambaye aliyekuwa Rais wa taifa hilo, Hosni Mubarak, bado imezorota baada ya kuhamishiwa kutoka gerezani na kupelekwa kwenye hospitali ya kijeshi.

Hosni Mubarak akiwa kizimbani
Hosni Mubarak akiwa kizimbaniPicha: dapd

Akiwa katika hospitali ya kijeshi kupata matibabu, wananchi waliopo katika uwanja wa al-Tahrir kujiandaa na maandamano ya leo bado wanachukizwa na yale aliyoyatenda Mubarak akiwa madarakani

Mmojawapo wa waandamanaji alisema " Hapana, hapana, kulikuwa na wizi na mambo mabaya, lazima aende jehenamu, tazama namna watoto wake walivyo na sisi tulichokifanya, aende jehanamu tu."

Endapo tume ya uchaguzi ya Misri itatangaza mshindi wa nafasi ya urais atakuwa ni rais wa nne wa taifa hilo la Kaskazini mwa Afrika tangu kuondolewa utawala wa Kifalme.

Mwandishi:Adeladius Makwega/DPAE/AFPE

Mhariri: Miraji Othman