Maandamano makubwa Cairo baada ya mswada kuidhinishwa
1 Desemba 2012Katiba hiyo mpya , ambayo imeidhinishwa baada ya vikao virefu usiku wa jana na ambayo imesusiwa na wajumbe wenye msimamo wa kati na Wakristo, inazua wasi wasi mkubwa kuhusu masuala ya haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na uhuru wa kidini, wanasema wanaharakati.
Morsi atapitia upya mswada huo leo Jumamosi,(01.12.2012), amesema spika wa bunge Hossam el-Ghiriani, na anatarajiwa baadaye kuitisha kura ya maoni katika muda wa wiki mbili.
Katiba hiyo imechukua nafasi ya kati katika mzozo mbaya kabisa wa kisiasa nchini humo tangu pale Morsi alipochaguliwa mwezi Juni mwaka huu, ukiyahusisha kwa kiasi kikubwa makundi ya Kiislamu na wapinzani kutoka makundi yenye misimamo ya wastani.
"Iilaaniwe bunge la katiba," kundi kubwa ambalo lilikuwa na vipaaza sauti liliimba wakati wakiingia katika uwanja wa Tahrir, eneo lililotumika katika vuguvugu ambalo liliuondoa madarakani hatimaye utawala wa rais Hosni Mubarak mapema mwaka 2011.
Mabango yakimshutumu "Morsi kuwa ni dikteta" wakati waandamanaji wakipaaza sauti "Ulaaniwe utawala wa kiongozi," wakiwa na maana ya kiongozi wa chama cha udugu wa Kiislamu, ambapo Morsi alijitokeza kupitia chama hicho kabla ya kuwa rais.
Maandamano msikitini
Maandanano mengine yalizuka wakati Morsi alipokuwa akisali katika msikiti mjini Cairo, baada ya imam kuwataka Waislamu kumuunga mkono rais, lakini hakukuwa na tukio kubwa.
Mapambano yalizuka katika mji wa kaskazini wa Alexandria baina ya waandamanaji wanaomuunga mkono na rais Morsi na wale wanaompinga, duru za usalama zimesema , lakini hakukupatikana taarifa mara moja za watu waliojeruhiwa. Maandamano yanatarajiwa kufanywa na kambi zote mjini Cairo leo Jumamosi(01.12.2012).
Mzozo wa hivi sasa ulizuka baada ya rais Morsi kutoa tamko hapo Novemba 22 akijipa madaraka makubwa na kuwezesha uamuzi wake wowote kutopingwa na mahakama, hali ambayo ilizusha maandamano pamoja na mgomo wa majaji.
Katiba mpya huenda isipitishwe
Amri aliyotoa imezuwia chombo kikuu cha sheria , mahakama ya katiba kuwa na uwezo wa kulivunja bunge linaloongozwa na kundi la Waislamu , katika uamuzi ambao wangeuchukua siku ya Jumapili kuhusu uhalali wa kisheria wa bunge hilo la katiba.
Bunge la katiba limeandika mswada wa katiba ambao utachukua nafasi ya katiba ya zamani ambayo imesitishwa baada ya kuondolewa madarakani kwa rais Hosni Mubarak mwaka jana , lakini kukamilishwa kwake kumesogezwa mbele kutokana na mtafaruku uliosababishwa na amri aliyoitoa rais Morsi.
Mgomo wa majaji uliotishwa na mahakama ya katiba pamoja na mahakama nyingine kunaweza kuiweka hatua ya kura ya maoni katika hatari, iwapo majaji ambao kwa kawaida hufanya uchunguzi wa uchaguzi watakataa kuipa kura hiyo uhalali.
Wanaharakati wameushambulia mswada huo wa katiba , wakisema unalinda baadhi ya sheria kwa kukandamiza nyingine.
Mwandishi: Sekione Kitojo /afpe
Mhariri: Iddi Ssessanga