Maandamano Iran kuunga mkono utawala
3 Januari 2018Watu walikuwa wakipiga makelele , "kiongozi, tuko tayari" na picha zilionesha maelfu ya watu wakiandamana katika miji ya Ahvaz, Kermanshah, Gorgan na kwingineko. Waandamanaji walipunga bendera ya Iran na picha za kiongozi mkuu wa kidini Ayatollah Ali Khamenei , pamoja na mabango yaliyoandikwa , "kifo kwa wachochezi".
"Tutatoa damu katika mishipa yetu kwa kiongozi wetu," ilikuwa ni kauli mbiu nyingine waandamanaji waliyokuwa wakiimba. Kumekuwa na ripoti chache za maandamano ya kuipinga serikali baada ya utawala kuja pamoja kupambana na ghasia hizo wiki iliyopita ambapo watu kiasi ya 21 waliouwawa.
Marekani iliendelea kuweka mbinyo kwa viongozi wa taifa hilo la Kiislamu, ambapo balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley akitoa wito kwa Umoja huo kufanya kikao cha dharura kuzungumzia hali hiyo.
"Watu wa Iran wanalilia uhuru," amesema katika mkutano na waandishi habari. "Watu wote wanaopenda kuwa huru wanapaswa kusimama kuwaunga mkono." amesema Haley.
Mataifa mengi yanaangalia
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani Heather Nauert alisema kwamba mataifa yote yanaangalia kwa karibu hali nchini Iran.
„Mataifa mengi duniani yanaangalia kile kinachotokea Iran, wanaangalia kwa karibu sana. Marekani , hata washirika wetu na marafiki pia wanaangalia. Ufaransa , Ujerumani, Uingereza, mmesikia mengi kutoka kwao katika siku za hivi karibuni wakielezea wasi wasi wao, kama tulivyoeleza wasi wasi wetu juu ya ukandamizaji dhidi ya haki za binadamu. Tunaangalia hayo kwa karibu. Hii ni pamoja na kukamatwa watu kwa kuandamana kwa amani."
Viongozi wa Iran wamesema maandamano , ambayo yalianza kuhusiana na suala ya kiuchumi Disemba 28 lakini haraka yakageuka kuwa makubwa zaidi, walikuwa sehemu ya mpango wa mataifa ya kigeni kuudhoofisha utawala huo. "Maadui wamejiunga pamoja na wanatumia kila mbinu , fedha , silaha , sera na huduma za ujasusi kuleta matatizo katika taifa hilo la Kiislamu, amesema Ali Khamenei.
Hata wanamageuzi , ambao waliunga mkono maandamano makubwa yaliyopita dhidi ya madai ya udanganyifu katika uchaguzi mwaka 2009 , mara hii wameshutumu ghasia na uungaji mkono uliopata kutoka Marekani.
Mwandishi. Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman