1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maadhimisho ya miaka 12 tangu kutokea mauaji ya Srebrenica

11 Julai 2007

Wananchi wa Bosnia leo wanazika mabaki ya waislamu 450 waliouwawa miaka 12 iliyopita huko Srebrenica.

https://p.dw.com/p/CHBA
Waislamu 8000 waliuwawa Srebrenica
Waislamu 8000 waliuwawa SrebrenicaPicha: AP

Mauaji hayo ya halaiki ndio mabaya kabisa kuwahi kutokea barani Ulaya tangu vita vya pili vya dunia.

Watu zaidi ya 30 elfu walionusurika kwenye mauaji ya halaiki ya Srebrenica wanahudhuria maadhimisho hayo yaliyogubikwa na huzuni.

Shughuli hiyo ya kidini inafanyika kwenye makaburi ya kumbukumbu ambako mabaki ya watu zaidi ya 2,400 waliouwawa yalizikwa.

Miongoni mwa watu wanaotajwa kuhudhuria maadhimisho hayo ni pamoja na mwendesha mashtaka mkuu wa Umoja wa mataifa katika kesi za uhalifu wa kivita Carla Del Ponte na watu wengine kiasi 2000 ambao walianza maandamano ya siku nne ya kuwakumbuka wafu yaliyoanza jumapili iliyopita.

Miongoni mwa mabaki ya watu 465 yanayozikwa leo kuna pia mabaki ya mwanamke mmoja wa miaka 75 pamoja na wahanga wengine wakiume waliokuwa na umri kati ya miaka 13 na 77.

Mabaki hayo yalifukuliwa kutoka makaburi ya pamoja yaliyoko kwenye mji wa mashariki na baadae kufanyiwa uchunguzi wa DNA.

Wanajeshi wa Bosnia na Serbia waliendesha mauaji ya kiasi cha waislamu 8000 wake kwa waume katika mji wa Srebrenica wakati huo ukiwa pepo ya Umoja wa mataifa chini ya ulinzi wa walinda amani kutoka Uholanzi mwishoni mwa vita vya Bosnia mwaka 1992 hadi 1995. Itakumbukwa kwamba mwaka 2002 serikali ya uholanzi ilijiuzulu baada ya kutolewa ripoti iliyowalaumu wanasiasa kwa kutuma wa nchi hiyo katika kazi ya kijeshi ambayo haikufaulu.

Mauaji hayo ndio mkasa pekee katika vita vya Bosnia ambao umetajwa kuwa mauaji ya halaiki na mahakama ya Umoja wa mataifa inayoshughulikia uhalifu wa kivita pamoja na mahakama ya kimataifa ya sheria mjini The Hague.

Uamuzi wa mahakama ya kimataifa ya sheria ICJ uliwafanya baadhi ya viongozi wa kiislamu kutaka mauaji ya Srebrenica kupewa hadhi maalum na kuwekwa katika mamlaka ya sheria za serikali jambo ambalo liliibua mivutano ya kisiasa katika nchi ambayo tayari hali yake ya kisiasa ina mashaka.

Radovan Karadzic na kamanda wake wa jeshi Ratko Mladic ni watu waliokuwa wakisimamia jeshi la Bosnia na Serbia na ambao wanatuhumiwa kuhusika zaidi na mauaji hayo ya halaiki bado hawajakabiliwa na sheria.

Wawili hao wanatuhumiwa kusababisha mauaji ya zaidi ya watu laki mbili katika vita vya Bosnia.

Karadzic inaaminika amejificha kwenye maeneo yanayodhibitiwa na Serbia huko Bosnia. Ratko Mladic inadaiwa anahifadhiwa nchini Serbia.