1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

M23 kukomesha uasi Congo

M23.Congo,Bisimwa6 Novemba 2013

Waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwenye eneo la vurugu mashariki mwa nchi hiyo wametangaza kukomesha uasi wao wa miezi 18 baada ya kushindwa na vikosi vya serikali vikisaidiwa na vile vya Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/1ACyA
Kiongozi wa kisiasa wa kundi la M23 Bertrand Bisimwa.
Kiongozi wa kisiasa wa kundi la M23 Bertrand Bisimwa.Picha: JUNIOR D.KANNAH/AFP/Getty Images

Taarifa ya kundi la M23 ilitolewa hapo Jumanne kwamba itamaliza uasi wake na badala yake itapigania malengo yake kwa njia za kisiasa inakuja baada ya takriban waasi 200 waliokuwa wamejichimbia milimani kutimuliwa na mashambulizi ya vikosi vya serikali ya Congo.

Wajumbe kutoka Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya wamelikaribisha tangazo hilo na kusisitiza katika taarifa ya pamoja kwamba hiyo ni hatua moja katika kuushughulikia mzozo ulioichagiza Congo na ukosefu wa utulivu nchini humo pamoja na kukomesha umwagaji damu unaofanywa na makundi yote ya wapiganaji yasio halali nchini humo.

Balozi wa Marekani nchini Congo Russ Feingold ameita hatua hiyo kuwa muhimu na ya kusisimua inayoelekea kwenye mwelekeo sahihi.

Kundi la M23 ladhoofika

Kundi la M23 linadaiwa kuwa lilikuwa likipatiwa msaada wa kijeshi na wa kifedha kutoka Rwanda nchi ambayo rais wake ni Mtutsi.Serikali ya Rwanda imekanusha madai hayo licha ya ushahidi uliotolewa katika repoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa.Hata hivyo uungaji mkono wao huo umeonekana kupunguwa katika miezi ya hivi karibuni kutokana na ongezeko la shinikizo la kimataifa kuitaka nchi hiyo kuacha kuchochea mizozo ya Congo kwa kuunga mkono waasi.

Waasi wa kundi la M23 .
Waasi wa kundi la M23 .Picha: Isaac KasamaniAFP/Getty Images

Rais wa kundi la M23 Betrand Bisimwa amesema katika taarifa hapo Jumanne kwamba anawaamuru makamanda wa waasi kuviandaa vikosi vyake kwa ajili ya mchakato wa kusalimisha silaha,kuvunjwa kwa kundi hilo na kujumuishwa katika jamii chini ya masharti ya yatakayofikiwa katika makubaliano ya amani na serikali ya Congo.

FDLR kuandamwa

Katika mji mkuu wa Kinshasa msemaji wa serikali ya Congo Lambert Membe ameapa kwamba jeshi la nchi hiyo hivi sasa litaelekeza juhudi zake katika kuwaadama wapiganaji wa Kihutu kutoka kundi la FDLR ambalo alinaongozwa na Wanyarwanda waliosaidia kufanya mauaji ya kimbari nchini humo hapo mwaka 1994.

Wanajeshi wa Congo mashariki mwa nchi hiyo katika harakati zao za kuwatimuwa waasi wa M23.
Wanajeshi wa Congo mashariki mwa nchi hiyo katika harakati zao za kuwatimuwa waasi wa M23.Picha: Reuters/Kenny Katombe

Takriban wapiganaji 100 wa kundi la M23 wametekwa na vikosi vya serikali na kiongozi wa kundi hilo Sultani Makenga na maafisa wengine waandamizi inaaminika wamekimbilia katika nchi jirani ya Rwanda au Uganda.

Kuvunjwa kwa kundi la M23 kunatowa ushindi wa wazio na mkubwa kabisa kwa serikali ya Congo tokea kwa uasi wa kutaka kujitenga wa mwaka 1963 katika jimbo la kusini la Katanga.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/AP

Mhariri: Josephat Charo