1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Müller asisitiza Marshalll Plan kwa Afrika

8 Septemba 2016

Waziri wa ushirikiano wa maendelo wa Ujerumani Gerd Müller akiridhishwa na bajeti ya wizara ya euro bilioni 8 ametilia tena mkazo azma yake ya kulisaidia bara la Afrika kwa Mpango wa Marshall.

https://p.dw.com/p/1Jyab
Picha: picture-alliance/dpa/Phototek/U. Grabowsky

Waziri huyo amekiri kwamba shabaha ya asilimia 0.7 ya pato la jumla la taifa katika suala la maendeleo haikufikiwa lakini wako njiani kuelekea huko.

Mwanasiasa huyo wa chama cha CSU alikuwa akizungumza katika kikao cha bajeti katika bunge la Ujerumani Jumatano usiku.Amesisitiza kwamba mpango wa bajeti wa wizara yake ni lazima utekelezwe.

Hata hivyo upinzani umesema kwamba mpango huo wa bajeti wa wizara hiyo hautoshi na wametaka uongezewe fedha zaidi.

Takriban euro bilioni nane zilitengwa kwa ajili ya bajeti ya wizara ya ushirikiano wa maendeleo kwa mwaka 2017. Wizara hiyo imelinganisha ongezeko la bajeti hiyo la kama euro milioni 580 kwa mwaka huu wa sasa kuwa ni kubwa kabisa kuwahi kushudiwa kabla katika historia ya bunge ya hilo.

Marshall Plan kwa Afrika

Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Ujerumani Gerd Müller akiwa ziarani Senegal.
Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Ujerumani Gerd Müller akiwa ziarani Senegal.Picha: DW/A. Kriesch

Müller amesisitiza umuhimu wa wizara yake kukabiliana na sababu za ukimbizi.Amesema kikao hicho cha bajeti hakiwezi kuendeshwa bila ya kusikiliza kilio cha msaada kutoka mji wa Allepo nchini Syria ambapo kuna watu 500,000 waliokwama.

Ziada ya hilo amerudia tena wito wake wa kulisaidia bara la Afrika kwa kupitia Mpango wa Marshall. Katika ziara yake ya hivi karibuni barani humo ameutaka Umoja wa Ulaya utowe euro bilioni 10.

Alipozitembelea Senegal,Niger na Rwanda waziri huyo alirudia tena wito wake wa kuwepo kwa Mpango huo wa Marshall kuisaidia Afrika kwa kuiga mfano wa mpango kama huo uliotumika kuijenga upya Ulaya baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Ukosoaji waandamana na furaha

Waziri wa Fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble.
Waziri wa Fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble.Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Waziri wa Fedha Wolfgang Shäuble wa chama cha CDU na Waziri wa Uchumi wa chama cha SPD Sigmar Gabriel wametowa wito wa kuungwa mkono kwa wito wake wa kuanzishwa kwa kodi mpya ya maendeleo kwa ajili ya uwekezaji ili kukuza biashara katika nchi za kimaskini.Yeye na mawaziri wenzake tayari wameliwasilisha pendekezo hilo.

Ukosoaji wa upinzani umekwenda sambamba na kufurahiwa kwa bajeti hiyo.Michael Leutert wa chama cha sera za mrengo wa kushoto cha Die Linke mtizamo wake ni kwamba ongezeko hilo la euro milioni 580 mwakani ambazo hata bado kuingia zitatumika kulipia madeni.

Akisisitiza haja ya kuongezwa kwa bajeti ya wizara hiyo Anja Hajduk wa chama cha Kijani kwa mara nyengine ametowa wito alioutowa mwaka 2017 wa kuongozwa euro bilioni mbili zaidi ambapo kwayo bilioni 1.2 zitumike kwa ajili ya msaada wa maendeleo na zilizobakia kwa ajili ya ulinzi wa mazingira.

Amesema ni kwa ongezeko hilo tu ahadi ya kufikia kiwango cha asilimia 0.7 ifikapo mwaka 2020 itaweza kutimizwa.

Mwandishi : Mohamed Dahman /epd

Mhariri : Yusuf Saumu