1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON:Urusi yatoa tamko rasmi kuhusu mzozo wa kidiplomasia na Uingereza

18 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBhb

Urusi imetoa tamko rasmi baada ya Uingereza kuamua kuwafukuza wanadiplomasia wanne wa Urusi.Katika mkutano na waanmdishi wa habari naibu Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Alexander Grushko alisema kuwa nchi yake itatoa jibu mwafaka ila hakutoa maelezo.

Uingereza iliwafukuza wanadiplomasia hao baada ya nchi ya Urusi kukataa kumrejesha mshukiwa mkuu Andrei Lugovoi katika mauaji ya Alexander Litvinenko afisa wa ujasusi wa zamani kwenye shirika la KGB.Waendesha mashtaka nchini Uingereza wanaamini kuwa Andrei Lugovoi ambaye pia ni afisa wa ujasusi wa zamani alimtilia sumu Bwana Litvinenko alipokuwa mjini London mwaka jana.Urusi kwa upande wake inashikilia kuwa katiba yake hairuhusu kurejeshwa nchi nyingine ili kushtakiwa kwa raia wake.

Uingereza inasema kuwa hatua yoyote ya Urusi ya kulipiza kisasi haikubaliki kufuatia mvutano huo wa kidiplomasia.Uingereza imetangaza kubadili mfumo wa visa kwa Urusi huku mzozo huo ukishika kasi.Mvutano huo unatokea wakati Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown anafanya ziara rasmi ya kwanza nchini Ujerumani.Kiongozi huyo anasisitiza kuwa nchi yake bado inataka uhusiano mzuri na Urusi ila hajaomba msamaha kwa vitendo vya serikali yake.