1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

London yateremsha pazia la Michezo ya Olimpiki 2012

13 Agosti 2012

Michezo ya Olimpiki jijini London ilikamilika jana katika sherehe ya kufana baada ya wiki mbili za tamasha la spoti ambalo liliipa sifa taifa mwenyeji na kutazamwa na mabilioni ya watu kote ulimwenguni.

https://p.dw.com/p/15oyl
LONDON, ENGLAND - AUGUST 12: A general view of the stadium as a Union Jack is formed during the Closing Ceremony on Day 16 of the London 2012 Olympic Games at Olympic Stadium on August 12, 2012 in London, England. (Photo by Rob Carr/Getty Images)
Olympia 2012 AbschlußfeierPicha: Getty Images

Rais wa kamati ya kimataifa ya Olimpiki - IOC Jacques Rogge aliisifu michezo hiyo kuwa ni “furaha na utukufu” kabla ya mashindano hayo kukamilika rasmi katika sherehe iliyodumu saa tatu na kupambwa na wasanii wa muziki. Katika sherehe hiyo pia kulishuhudiwa tukio la kukabidhiwa bendera ya Olimpiki kwa Meya wa mji wa Rio de Janeiro, ishara ya kuanza maandalizi kusubiri miaka minne kufika mwaka wa 2016 ambapo michezo hiyo itaandaliwa katika mji huo wa Brazil.

Marekani iliongoza orodha ya medali ikiwa na dhahabu 46, nane mbele ya China, huku Uingereza ikiwa na 29, ikiwa ni idadi bora zaidi tangu mwaka wa 1904. baada ya siku 16 za mashindano, mataji 302 ya Olimpiki yalipeanwa na rekodi 46 za ulimwengu zikavunjwa. Zaidi ya mashabiki milioni saba walijitokeza kushangilia mashindano ya vitengo mbalimbali.

Meya wa London Boris Johnson aliridhika na michezo ya Olimpiki
Meya wa London Boris Johnson aliridhika na michezo ya OlimpikiPicha: Getty Images

Katika siku ya mwisho ya michezo hiyo, medali 15 zilipewa washindi, huku kikosi cha Marekani cha mchezo wa kikapu kwa wanaume kikinyakua dhahabu baada ya kuishinda Uhispania. Siku ya mwisho pia ilianza na tamaduni yam bio za marathon ambapo Stephen Kiprotich wa Uganda alishinda medali ya dhahabu jambo ambalo halikutarajiwa. Kiprotich aliwapiku magwiji wa Kenya ambao bingwa mtetezi mara mbili wa ulimwengu Abel Kirui alichukua medali ya fedha naye Wilson Kipsang akipata shaba.

Na bila shaka baada ya London sasa macho yote yataelekea Amerika Kusini. Mkuu wa Tume ya uuzaji ya Kamati ya Kimataitaifa ya Olimpiki Gerhard Heiberg anasema mji wa Rio utatumiwa kama majaribio kwa sababu bara hilo halijawahi kuwa tamasha kubwa kama hilo. Kisha baada ya hapo linalweza kupelekwa barani Afrika mnamo mwaka wa 2024. mapema wiki hii Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga alitangaza kuwa mji mkuu Nairobi unapanga kuwasilisha ombi la kuandaa michezo hiyo katika mwaka wa 2014. miji ya Tokyo, Madrid na Istanbul inawasilisha maombi ya kuandaa michezo ya mwaka wa 2020, huku uamuzi ukitarajiwa kutoldewa mwaka ujao.

Bayern yaipiku Dortmund

Mchezaji aliyesajiliwa msimu huu Mario Mandzukic aliisaidia Bayern Munich kuishinda Borussia Dortmund magoli mawili kwa moja na kulibeba kombe la Ujermani la Super mjini Munich jana Jumapili. Mandzukic aliyesajiliwa kwa kita cha euro milioni 13 kutoka Wolfsburg alifunga bao katika dakika ya sita kabla ya Thomas Mueller kutikisa wavu dakika tano baadaye.

Bayern walitangaza kuwa wako imara msimu huu
Bayern walitangaza kuwa wako imara msimu huuPicha: Bongarts/Getty Images

Robert Lewandowski wa Dortmund alifunga moja katika dakika ya 75 lakini licha ya mashambulizi makali, Bayern wailinda ngome yao vilivyo na kupata ushindi wa kwanza katika kipindi cha miaka miwili na nusu. Bayern ilikiwa imeshindwa na Dortmund katika mechi tano zilizopita, lakini walianza wka kasi sana kuliko mabingwa hao wa Bundesliga, ambao mchezaji bora wa mwaka nchini Ujerumani Marco Reus alicheza mwecho yake ya kwanza. Mechi hii inakuja zikiwa zimesalia chini ya wiki mbili kwa msimu mpya wa Bundesliga kuanza.

Man City yaizamisha Chelsea

Kule Uingereza, Manchester City ilitoka nyuma na kushinda kombe lao la kwanza msimu huu wakati ilipoishinda Chelsea magoli matatu kwa mawili katika mchuano wa Community Shield.

Fernando Torres aliiweka Chelsea kifua mbele lakini Branislav Ivanovic akatimuliwa uwanjani dakika mbili baadaye kwa kupewa kadi nyekundu, na kuufanya mchezo kuiendea City. Yaya Toure alisawazisha mapema katika kipindi cha pili lakini magoli mengine kutoka kwa Carlos Tevez na Samir Nasri yakahitimisha mchuano licha ya goli la lake Ryan Betrand katika dakika za mwisho.

Licha ya ushindi, mkufunzi wa City Roberto Mancini alikiri kuwa hafurahii hatua ya klabu hiyo kutowasajili wachezaji wapya. Mechi hiyo ambayo huwaleta pamoja mshindi wa kombe la FA na Ligi kuu EPL, huwa ni ya kufungua msimu mpya wa ligi ambao unaanza mwishoni mwa wiki hii tarehe 18.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman