1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON: Mwanamaji wa kike asema alitishwa

9 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CCBB

Mwanamke pekee aliyekuwa miongoni mwa mabaharia 15 wa Uingereza waliozuiliwa na Iran amesema alitishwa na kifungo cha miaka mingi gereza kwa kufanya ukachero kama hangekubali kufanya alichoambiwa na watu waliokuwa wakimzuilia.

Katika mahojiano yake ya kwanza tangu kuachiliwa huru Alhamisi iliyopita mjini Tehran, yaliyochapishwa leo na gazeti la Sun nchini Uingereza, Faye Turney, amesema aliulizwa alihisi vipi kufa kwa ajili ya nchi yake.

Aidha amesema alihofu alikuwa akipimwa ili atayarishiwe jeneza lake. Afisa huyo amesema asubuhi moja alisikia mbao zikikatwa na misumari ikikomelewa karibu na chumba alimokuwa akizuiliwa na afisa wa kike akachukua vipimo vyake. Faye Turney mama wa mtoto wa kike mwenye umri wa miaka mitatu, amesema aliwekwa katika chumba akiwa peke yake kwa siku tano.

Gazeti la Sun limeripoti kwamba mama huyo alikuwa na hofu ya kubakwa alipokamatwa.

Iran ilitoa barua tatu zinazosemekana ziliandikwa na mwanamke huyo moja kati yao ikisema alikuwa anatumiwa kwa masilahi ya sera za serikali za Marekani na Uingereza.