1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

London. Kiongozi wa kanisa azishutumu Uingereza na Marekani kwa vita nchini Iraq.

23 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCgk

Kiongozi wa kiroho wa kanisa la Kianglikana ametoa shutuma kali dhidi ya serikali za Uingereza na Marekani leo, akisema kuwa sera zao za kijinga , nchini Iraq zinawaweka Wakristo katika hali ya hatari katika eneo hilo.

Askofu mkuu wa Canterbury Rowan Williams, kiongozi wa Waanglikani wapatao milioni 77 duniani, amesema Wakristo wanashambuliwa na kulazimika kukimbia eneo la mashariki ya kati kwasababu raia wenzao wanawaona kuwa wanaunga mkono vita vya msalaba vinavyoongozwa na mataifa ya magharibi.

Askofu mkuu Williams ameandika katika makala iliyochapishwa katika gazeti la London Times kuwa katika wakati huu wa Krismass, tuomba kwa ajili ya mji mdogo wa Bethlehem, na kuwakumbuka wale ambao wamewekwa katika hatari kutokana na ufinyu wa mawazo ya kuona mbali pamoja na ujinga.

Williams ambaye hachelei kusema kweli, amekuwa kila mara akikosoa vita vya Iraq, akisema kuwa hakuna msingi wa kiroho , kwa hatua ya kuivamia nchi hiyo.