1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON: Brown asema Uingereza haijashindwa Irak

3 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBT1

Waziri mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, amesema leo kwamba kuondoka kwa kikosi cha mwisho cha Uingereza kusini mwa Irak hakuashirii kushindwa.

Brown amesema hatua hiyo ilipangwa kabla kuchukuliwa na haipaswi kufahamika kana kwamba Uingereza imeshindwa.

Hata hivyo wataalamu wa maswala ya usalama nchini Uingereza wanasema hatua hiyo ni muhimu na huenda hatimaye ikasababisha kuondoka majeshi yote ya Uingereza kutoka Irak.

Aliyekuwa zamani waziri wa mashauri ya kigeni na ulinzi wa Uingereza, Malcolm Rifkind, amesema, ´Kama serikali ya Uingereza ingetangaza hadharani wasiwasi mkubwa iliyokuwa nao na kukataa sera za kipuuzi zilizokuwa zikiendelezwa na Donald Rumsfeld kwa kufuata maagizo ya rais Bush, basi hiyo ingesaidia kubadili sera na ni idadi ndogo tu ya wanajeshi wa Marekani, Uingereza na Wairaki ambao wangepoteza maisha yao katika miaka michache iliyopita.´

Mapema leo wanajeshi wa Irak wamepandisha bendera ya Irak katika ikulu ya mjini Basra baada ya wanajeshi wa Uingereza kuondoka kutoka kambi yao iliyokuwa imesalia mjini humo.

Hatua hiyo inalipa mamlaka jeshi la Irak kusimamia usalama huku likikabiliwa na changamoto ya mashambulio yanayofanywa na wanamgambo wa kishia.

Kuondoka kwa wanajeshi 500 wa Uingereza mjini Basra kunaufanya mji huo ulio wa pili kwa ukubwa nchini Irak kuwa bila na majeshi ya kigeni kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 2003.

Kamanda wa jeshi la Irak, jenerali Mohan al Fireji amethibitisha kuondoka kwa wanajeshi hao wa Uingereza mjini Basra. Magari ya jeshi la Uingereza yameondoka ikulu ya mjini Basra kuelekea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Basra, yapata kilomita 20 nje ya mji huo.