1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Loew ana kibarua kikubwa kuchagua timu

Bruce Amani
3 Julai 2017

Mafanikio ya timu ya taifa ya Ujerumani iliyopelekwa katika dimba la Kombe la Mabara nchini Urusi yana maana kuwa kocha Joachim Loew ana kazi kubwa ya kuamua ni nani atamchagua na nani wa kumuwacha katika timu ya taifa

https://p.dw.com/p/2fqtw
Fußball Training Deutschland Nationalmannschaft
Picha: Getty Images/Bongarts/A. Hassenstein

Tatizo kubwa la Loew sasa huenda likawa ni nani wa kumwacha nje ya kikosi chake.

Wachezaji kama vile wafungaji wa mabao mengi katika Kombe la Mabara Timo Werner, Lars Stindl na Leon Goretzka, ambao wote walitikisa nyavu mara tatu katika dimba hilo, wana kila haki ya kuamini kuwa mchezo wao mzuri nchini Urusi utawapa fursa ya kujumuishwa katika kikosi cha Kombe la Dunia 2018.

Antonio Ruediger, Sebastian Rudy na Mathias Ginter pia walidhihirisha uwezo wao wakati Julian Draxler, aliyekuwa nahodha wa kikosi kuchukua nafasi ya Manuel Neuer, alishinda tuzo ya mchezaji bora wa mashindano hayo. Loew mara nyingi husititiza umuhimu wa kuwa na wachezaji katika kila nafasi ili kufanikiwa katika kiwango cha kimataifa. Kwa kuangalia mchezo wao katika siku chache zilizopita, inaonekana kuwa huenda akawa na karibu watatu.

Deutschland Fußball Nationalmannschaft | Mannschaftsfoto
Kikosi kilichoiwakilisha Ujerumani dimba la MabaraPicha: picture-alliance/GES/M. Gilliar

Wachezaji vigogo ni Neuer, Jerome Boateng, Mats Hummels, Toni Kroos, Sami Khedira, Mesut Ozil, Thomas Mueller na Marco Reus, ambao wote walianchwa nyuma ili kuwa katika hali imara tayari kwa mwaka ujao.

Wachezaji wengine kadhaa wa timu ya kwanza walibaki nje kwa kuwa ni majeruhi wakiwemo Leroy Sane, Ilkay Guendogan, Julian Weigl na Jonathan Tah.

Lakini hakuna anayeweza kuchukulia kuwa nafasi yake iko salama wakati kukiwa na wachezaji waliotamba katika timu ya chini ya umri wa miaka 21 kama vile Jeremy Toljan, Niklas Stark, Maximilian Arnold, Max Meyer, Serge Gnabry na Davie Selke ambao wanatafuta nafasi katika kikosi cha taifa. Licha ya ushindi huu, kocha Loew anasema Kombe la Dunia ni mtihani mwingine mpya "hatuna ttaizo lolote la sisi kuitwa timu inayopigiwa upatu. Tuna furaha. Lakini kuna kitu kimoja ambacho ni wazi kabisa kwa kila kinyang'anyiro hasa katika awamu ya mwondowano unapaswa kucheza kwa asilimia 100 kama unataka kufuzu katuka duru ijayo. Na tutajaribu kabisa kufanya hivyo mwaka ujao.

GES/Fussball/Abflug der deutschen Nationalmannschaft nach Frankfurt
Timo Werner alikuwa mmoja wa wafungaji boraPicha: picture alliance/GES/Markus Gilliar

Lakini mafanikio ya Ujerumani yanatokana na nini?

Haya yote tuliyoyaona sio suala la kubahatisha. Shirikisho la kandanda la Ujerumani – DFB linastahili sifa kwa kuwekeza mashinani. Mpango wa kukuza vipaji vya vijana ulifanyiwa mabadiliko na kuzinduliwa upya mwaka wa 2003, wakiwa na lengo la kuimarisha viwango vya kandanda kote nchini na kuleta usawa katika vyama vyote vya kandanda vya kikanda nchini Ujerumani. Vituo vya mafunzo lazima victimize viwango vilivyowekwa na DFB na watalaamu wa nje. Katika msimu wa 2015-16, Vilabu vya Ujerumani viliwekeza zaidi ya euro milioni 150 katika idara zao za mafunzo ya vijana.

Na kwa kuiita timu ya Ujerumani iliyoshiriki na kutwaa Kombe la Mabara nchini Urusi kama Timu B ni kukikosea heshima kile Ujerumani imefanikisha katika mwongo mmoja uliopita. Ujerumani haitengenezi wachezaji wa Timu B, bali inawatengeneza washindi. Muenendo huo uliwekwa muda mrefu uliopita na utaendelea kwa miaka mingi ijayo.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo