1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Liverpool yaadhibiwa Manchester United hoi

Sekione Kitojo
23 Oktoba 2017

Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp  analazimika  kuifanyia  mabadiliko safu  yake  ya  ulinzi , baada  ya  kuadhibiwa  na  Harry Kane wa Tottenham Hot Spurs.

https://p.dw.com/p/2mMh8
Fußball Hertha BSC - FC Liverpool 0:3
Picha: picture-alliance/dpa/S. Stache

Manchester  United  haikucheza  na  mtiririko  wake wa kawaida kama  ilivyo  kwa  mahasimu  wake  katika  Premier League Manchester  City  ama  Tottenham , mchezaji  wa  kati  wa Huddersfield Town Tom Ince  amesema  baada  ya  ushindi  wa mabao 2-1  wa  timu  yake  dhidi  ya  kikosi  cha  kocha  nyota Jose Mourinho siku  ya  Jumamosi.

Huddersfield  iliangusha  mbuyu  siku  ya  Jumamosi  ikiwa  ni  kipigo cha  kwanza  kwa  kikosi  cha  Jose Mourinho  msimu  huu, ambapo mchezaji  huyo  wa  kiungo ,  baba  yake  Paul Ince  aliichezea Manchester  United  mara  204  katika  miaka  ya  90.

Liverpool vs. Chelsea - Premier League Jürgen Klopp
Kocha Juergen KloppPicha: Getty Images/C. Mason

Nae  kocha  nyota Jurgen Klopp  wa  Liverpool  aliona  rangi  zote kwa  wakati  mmoja  jana  Jumapili  baada  ya  kikosi  chake kuadhibiwa  vikali  na  Tottenham Hot Spurs  kwa  mabao 4-1  na kushuhudia  kipigo  cha  juu  kabisa  katika  ligi  hiyo  yenye ushindani  mkubwa  barani  Ulaya. Liverpool  ambayo  imeporomoka hadi  nafasi  ya  tisa  ikiwa  na  pointi  13 , imefungwa  mabao 16 hadi  sasa  ikiwa  ni  udhaifu  mkubwa  wa  safu  ya  ulinzi  ambao kocha  huyo  anatakiwa  kufanyia  kazi.

Großbritannien Fußball Jose Mourinho von Manchester United
Kocha wa manchester United Jose MourinhoPicha: Imago/Sportimage/S. Bellis

Liverpool kukwaana na Huddersfield

Hata  hivyo  Liverpool itataka  kurejea  katika  njia  ya  ushindi Jumamosi  ijayo  itakapokwaana  na  Huddersfield  Town , inayoongozwa  na  kocha  ambaye  alikuwa pamoja  nae  katika benchi  la  ufundi  la  timu  ya  Borussia  Dortmund, David Wagner.

Nchini  Ufaransa , Neymar  alikuwa  shujaa  na  pia aliyetia  doa wakati mshambuliaji  huyo raia  wa  Brazil  alipofunga  bao  na  kisha kutolewa  nje  kwa  kadi  nyekundu wakati Paris Saint Germain ilipopata  sare  ya  mabao 2-2 katika  pambano  kali la  mahasimu wakubwa  dhidi  ya  marseille  katika  League 1  jana  Jumapili.

Frankreich Paris Saint Germain vs Toulouse Neymar
Mchezaji wa kati wa PSG NeymarPicha: picture-alliance/dpa/AP/K. Zihnioglu

Baada  ya  Florian Thauvin  kuifungia  Marseille  bao  la  pili , na Neymar  akiwa  na  kadi  ya  njano moja tayari  alionekana  kupiga kichwa  mshambuliaji  wa  marseille  kutoka  Argentina  Lucas Ocampos na  kutolewa  kwa  kadi  ya  pili  ya  njano.

Nchini  Italia  Sami Khedira  wa  Ujerumani  alipachika   mabao matatu  katika  ushindi  wa  mabao 6-2 ya  Juventus  Turin dhidi  ya Udinese na  kuweka  mbio  za  kuwania  ubingwa  hai  ikiwa Juventus inafukuzana  na  viongozi  Napoli  na  Inter Milan.

Cristiano Ronaldo anaonekana  kuwa  mchezaji  anayeweza kutoroka  na  taji la  mchezaji  bora  wa  FIFA katika  mwaka  2017 kutokana  na   hali  bora  ya  timu  yake  ya  Real Madrid, sherehe zitakazofanyika  mjini  London leo  Jumatatu.

Al Ahly yaingia  fainali

Katika  bara  la  Afrika Al Ahly  ya  Misri  inakuwa  klabu  ya  kwanza kupachika  mabao 6  katika  mchezo  wa  Champions League  barani Afrika  katika  nusu  fainali  wakati  walipowararua  Etiole sahel  ya Tunisia  kwa  mabao 6-2  mjini  Alexandria  jana  Jumapili na  kufikia fainali. Mabingwa  hao  mara  nane  wa  taji  hilo ilifuzu  kwa  jumla ya  mabao 7-4 na  kukabiliana  na  Wydad  Casablanca  ya Morocco  katika  fainali  itakayochezwa  kwa  mikondo  miwili ikiwa mkondo  wa  kwanza  utafanyika  mwishoni  mwa  juma  nchini  Misri.

Ägypten Fussball Al-Zamalek vs Al-Ahly
Mchezaji wa Al Ahly ya Misri (kulia) Marouf YoussefPicha: picture-alliance/dpa/A. Malky

Nayo TP Mazembe  mabingwa  watetezi  wa  kombe  la  CAF  la Shirikisho  wataoneshana  kazi  katika  fainali  na  SuperSport  ya Afrika  kusini  baada  ya  timu  hizo  kufuzu  kuingia  katika  fainali itakayofanyika  Novemba  19.  Nchini  Tanzania  homa ya  pambano la  watani  wa  jadi  Simba  na  Yanga  hapo tarehe 28  mwezi  huu  imeanza  kupanda na  mashabiki  wanalizungumzia  pambano  hilo kana kwamba linafanyika  kesho. 

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre / afpe / dpae

Mhariri:  Mohammed Abdul rahman