1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya yasimamishwa Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa

2 Machi 2011

Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa imeisimamisha Libya uwanachama wake katika Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja huo kutokana na ukandamizaji wa utawala wa Muammar Gaddafi dhidi ya waandamanaji wanaompinga kiongozi huyo.

https://p.dw.com/p/10Rps
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moonPicha: dapd

Mwaka mmoja tu uliopita, Libya ilichaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza hili la Haki za Binaadamu. Kitendo hiki, licha ya kukosolewa na watetezi wa haki za binaadamu, kilichukuliwa kama dalili za kufunguka kwa nchi hiyo kwenye uso wa jumuiya ya kimataifa. Lakini sasa hali imebadilika kwa pamoja na, yumkini moja kwa moja, ndani ya Baraza hilo.

Hapo jana, Rais wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa, Mswisi Joseph Deiss, alisema uamuzi huo ni muhimu kulinda heshima ya Umoja huo.

"Heshima ya jumuiya ya kimataifa, hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa, Baraza Kuu la Usalama na Baraza la Haki za Binaadamu, iko hatarini. Lazima tuipe maana imani ya Umoja wa Mataifa kwa haki za binaadamu." Alisema Deiss.

Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa
Hadhara Kuu ya Umoja wa MataifaPicha: AP

Ijumaa ya wiki iliyopita, kamati maalum ya baraza hilo hilo, ikaonesha kuvunjwa moyo kwake na Libya na ikapaza sauti ya pamoja dhidi ya nchi hiyo. Ikasema inafadhaishwa sana na "uvunjaji wa haki za binaadamu wa makusudi na wa hali ya juu."

"Nimeshitushwa sana na upoteaji wa maisha ya watu na ukandamizaji dhidi ya raia unaofanywa na utawala wa Gaddafi na wafuasi wake." Alisema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon.

Jana, Katibu Mkuu huyo hakuzungumzia tu kuhusu matumizi mabaya ya nguvu dhidi ya raia, bali pia dhidi ya kitisho cha wimbi la wakimbizi na hatari inayoyakabili mataifa jirani na Libya na, hivyo, akasisitiza Umoja wa Mataifa kuchukua hatua madhubuti na za haraka.

Ban Ki-moon akakaribisha wazo la kulifikisha suala hili kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya The Hague, Uholanzi. Hili, kwa mujibu wa Katibu Mkuu huo, ni katika kuthibitisha kuwa uhalifu dhidi ya ubinaadamu unashughulikiwa kisheria.

Katika mdahalo mfupi uliofanyika baada ya hotuba ya Katibu Mkuu, ilikuwa wazi kwamba jumuiya nzima imeamua kusimama dhidi ya utawala wa Gaddafi.

Muammar Gaddafi
Muammar GaddafiPicha: Libya State Television via APTN/AP/dapd

Ni mjumbe wa Venezuela tu, Balozi Jorge Valero, aliyeeleza upinzani wa nchi yake dhidi ya azimio hilo akiliita kuwa ni njama ya mataifa ya kibeberu kutafuta sababu ya kuivamia Libya kijeshi, huku akiishutumu wazi wazi Marekani kuwa nyuma ya mpango huo.

Balozi wa Marekani katika Umoja huo, Susan Rice, alijibu tuhuma hizo kwa maneno makali.

"Ni jambo la aibu kwa nchi mwanachama wa Umoja huu, ambaye rekodi yake chafu inajieleza wazi, anavyotumia nafasi aliyopewa kueneza uongo, hofu na chuki." Alisema Balozi Rice.

Lakini naye akitumia jukwaa hilo kupeleka ujumbe kwa utawala wa Tripoli, Balozi Rice alisema kwamba utawala ambao unawamiminia risasi raia wake wenyewe, hauna nafasi kwenye Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa.

Licha ya kuwa uamuzi huu wa kuisimamisha Libya unabakia kuwa miongoni mwa maamuzi magumu kufikiwa na Umoja huu, bado matokeo yake kwa Gaddafi na wafuasi wake hayajafahamika. Japokuwa kama alivyosema Balozi Rice, ujumbe wake ni mmoja tu, nao ni kuwa mauaji lazima yasite na "Gaddafi lazima aondoke leo kabla ya kesho".

Mwandishi: Thomas Schmidt/ZPR
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman