1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya yaahidi ushirikiano kuchunguza shambulio la Lockerbie

29 Septemba 2011

Watawala wapya wa Libya wamesema wako tayari kushirikiana watakapotakiwa kuwakabidhi watu wahojiwe kuhusiana na shambulio la bomu dhidi ya ndege ya abiria katika anga ya Lockerbie nchini Scotland mnamo mwaka 1988.

https://p.dw.com/p/12iny
Mabaki ya ndege ya Pan Am aina ya Boeing 747 karibu na Lockerbie, ScotlandPicha: AP

Waziri wa sheria katika utawala wa mpito, Mohamed al-Alagi amesema yuko tayari kuchunguza washukiwa wengine waliohusika katika shambulio la Lockerbie. Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari hapo jana mjini Tripoli waziri huyo alisema utawala wa Libya hautakataa ombi lolote la kumhoji mtu yeyote anaeshutumiwa kuhusika na shambulio hilo, mbali na Abdel Baset al Megrahi, kwa kuwa uchunguzi utasaidia kufichua ukweli.

Libyen Großbritannien Lockerbie Attentäter Ankunft in Tripolis
Abdel Baset al-Megrahi, aliporejea TripoliPicha: AP

Al Megrahi alitiwa hatiani kwa shambulio hilo mwaka 2001 na kuhukumiwa kifungo cha maisha katika jela ya Scotland, lakini akaachiwa huru Agosti 20 mwaka 2009 baada ya madaktari kusema alibakiwa na miezi mitatu kabla kufa kutokana na saratani.

Mshukiwa wa pili raia wa Libya, Al Amin Khalifa Fhimah, pia alisimama kizimbani katika mahakama ya Scotland iliyokuwa ikiendesha vikao vyake nchini Uholanzi lakini hakupatikana na hatia na kuachiwa mwaka 2001.

Ndege ya Pan Am ilikuwa njiani kuelekea New York Marekani ikitokea London Uingereza wakati iliporipuka na kuanguka katika mji wa Lockerbie. Watu 259 waliokuwa ndani ya ndege hiyo walikufa, wengi wao wakiwa Wamarekani. Wengine 11 waliokuwa ardhini pia walikufa. Waendesha mashtaka wa Scotland walisema Jumatatu wiki hii kwamba wamelitaka baraza la mpito la Libya liwasaidie kuchunguza shambulio hilo.

Waziri mkuu wa zamani aitwa mahakamani

Wakati huo huo Libya imetoa amri ya kumtaka waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Baghdadi al Mahmudi, afike mahakamani. Mahmudi alikamatwa wiki iliyopita katika mpaka wa kusini magharibi wa Tunisia na Algeria. Mahakama ya Tunisia ilimhukumu kifungo cha miezi sita jela kwa kuingia nchini kinyume na sheria, lakini hukumu hiyo ikabatilishwa Jumanne wiki hii kufuatia rufaa iliyokatwa na mawakili wake.

Kwa upande mwingine waasi wa Libya wamesema watoto wawili wa Gaddafi wamenasa katika miji ambayo ingali imezingirwa na vikosi vya mapinduzi. Kwa mujibu wa Ahmed Bani, msemaji wa baraza la mpito, mtoto wa Gaddafi, Seif al Islam yuko mjini Bani Walid na kakake Muatassim yuko Sirte.

Libyen Muammar Gaddafi Moammar Gadhafi
Kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar GaddafiPicha: picture-alliance/dpa

Watawala wapya wa Libya wamesema wanaamini Gaddafi analindwa na watu wa kabila la kuhamahama la Tuareg katika mji wa jangwani wa Ghadamis karibu na mpaka wa Algeria. Hata hivyo, msemaji wa baraza la mpito amesema hawezi kuhakikisha kuhusu mahala alipo kiongozi huyo wa zamani.

Mapigano Sirte

Wafuasi wa Gaddafi wanakabiliana na mashambulio dhidi ya mji alikozaliwa wa Sirte na wamefaulu kuwazuia wapiganaji wa utawala mpya kuudhibiti mji huo, licha ya mapigano ambayo yamekuwa yakiendelea kwa wiki mbili.

Mapigano makali yaliripotiwa jana mjini Sirte huku wapiganaji wa utawala mpya wa Libya wakilazimika kurudi nyuma kiasi kilometa tatu kutoka mjini huo kutokana na mashambulio kutoka kwa wafuasi wa Gaddafi. Kamanda wa wapiganaji wa baraza la mpito amesema wapiganaji watatu waliuwawa kwa bahati mbaya wakati wenzao walipovurumisha kombora kutoka kifaru kilichokuwa nyuma yao.

Mwandishi: Josephat Charo/RTRE/AFPE/DPAE

Mhariri: Hamidou Oummilkheir