1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya inataka msaada wa Ulaya kwa kumiminikiwa na wahamiaji

Miraji Othman27 Mei 2009

Libya iko shidani kutokana na wahamiaji wasiokuwa halali

https://p.dw.com/p/HyOG
Bendera za Umoja wa Ulaya na LibyaPicha: AP/DW

Hivi karibuni Libya imetaka ipewe msaada zaidi kutoka nchi za Ulaya ili ikabiliane na tatizo la idadi inayozidi ya wakimbizi wanaoingia kwa magendo nchini humo, na kutoka hapo husafiri, kupitia Bahari ya Mediterranean, hadi Ulaya.

Karibu ya wahamiaji milioni moja wa aina hiyo wamemiminika nchini Libya, wakipitia kwenye mpaka wake wenye urefu wa kilomita alfu tano pamoja na nchi nyingi za Kiafrika zilizo maskini. Hali hiyo imeiweka nchi hiyo yenye kutoa mafuta katika shida, kwani inatumia fedha zake nyingi kuzuwia mmiminiko huo wa watu. Jambo hilo limeelezwa na wizara ya mambo ya kigeni ya Libya katika taarifa ilio ya nadra. Haijasema kwa muda gani shida hiyo imekuweko.

Uhamiaji ni suala la msisimiko kwa serekali za nchi za Ulaya, hasa katika wakati huu ambapo kuna mzozo wa kiuchumi duniani. Pia suala la uhamiaji ni la utata huko Libya, ambako kiongozi wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi, mwenyekiti wa sasa Umoja wa Afrika, AU, anataka Waafrika waikubali fikra yake ya Bara la Afrika kuwa na serekali moj, kama mfano wa Marekani, mfumo ambao utaruhusu watu, rasil mali na bidhaa kuweza kwenda huku na kule ndani ya Bara la Afrika bila ya vizuwizi.

Walibya wengi, ambao wanalalamika kwamba ongezeko kubwa la wahamiaji wa Kiafrika katika nchi hiyo limesababaisha hali ya kukosekana usalama, kusambaa magonjwa na kuengezeka usafirishaji wa madawa ya kulevya na matatizo mengine ya kijamii, wanaitaka serekali ya nchi yao iuandame uhamiaji usiokuwa wa halali. Wizara ya mambo ya ndani ya Libya ilisema ilitoa taarifa hiyo iili kuuomba Umoja wa Ulaya na jamii ya kimataifa kwamba Umoja huo utekeleze ahadi yake ya kutoa msaada wa kiufundi na vifaa pamoja na mafunzo. Taarifa hiyo ilisema jamii ya kimataifa lazima ibebe dhamana ya kuuona uhamiaji huo kuwa ni suala la uutu ambalo linazigusa nchi nyingi duniani, na ni jambo linalosababisha vifo vya maelfu ya binadamu.

Mwezi Februari mwaka huu, Umoja wa Ulaya uliipa Libya Euro milioni 20 kuisaidia kupambana na uhamiaji usiokuwa halali. Doria za mipakani pamoja na mitambo ya Rader zinazowekwa baharini imefanya iwe vigumu zaidi kwa wahamiaji haramu wanaoukimbia umaskini katika nch zao kuingia Spain kutokea Moroko. Hivi sasa maelfu ya wahamiaji wanajaribu kuwasili Ulaya kutoka upande wa Mashariki. Libya inapakana na Tunisia, Algeria, Misri, Sudan, Chad na Niger.

Umoja wa Ulaya umekuwa ukijaribu kufungua ukurasa mpya katika uhusiano wake na Libya tangu nchi hiyo ya Afrika Kaskazini ilipoachana na silaha zilizopigwa marufuku hapo mwaka 2003. Pande hizo mbili hivi sasa zinashauriano juu ya mkataba wa kibiasdhara na kisiasa ili kupanuwa ushirikiano wao katika maeneo tangu ya siasa za kigeni na usalama, uvuvi wa samaki, uhamiaji, nishati, usafiri na utaoaji wa Viza.

Ikiashiria kwamba msaada iliopewa Libya kutoka Umoja wa Ulaya hautoshi, wizara ya mambo ya kigeni ya huko Tripoli ilisema nchi hiyo inatumia fedha katika shughuli za kuwaokoa wahamiaji walioko katika shida baharini, kuwapatia makaazi na kuwarejesha walikotoka wahamiaji wasiokuwa wa halali. Imetumia jumla ya dola za Kimarekani milioni 32.44 katika kipindi cha miaka mitatu hadi mwaka 2008 kwa ajili ya shughuli hizo.