1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LIBYA INA NJIA NDEFU KUELEKEA DEMOKRASIA

23 Agosti 2011

Libya ni mada inayoendelea kugonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani. Lakini hata hatima ya baadhi ya wapokea pensheni nchini Ujerumani,ni miongoni mwa mada zilizoshughulikiwa katika magazeti ya leo Jumanne.

https://p.dw.com/p/RhWF

Basi tukianza na Libya, DIE BADISCHE ZEITUNG linasema:

"Mifano ya Tunisia na Misri imeonyesha kuwa kumshinda dikteta haimaanishi moja kwa moja kuwa huo, ni mwanzo wa demokrasia. Na nchini Libya utaratibu wa kidemokrasia huenda ukawa mgumu zaidi. Kwa hivyo, ni muhimu kwa jumuiya ya kimataifa na hasa Ulaya na Marekani, kuendelea kusaidia kwa dhati jitahada za kuijenga upya Libya. Sio kwa fedha, kwani nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta, haina shida hiyo, bali inaweza kushauriwa katika ujenzi wa taasisi za kidemokrasia. Hapo Ujerumani ingeweza kutoa mchango wake kwa vile haikusaidia kijeshi."

Hata gazeti la MITTELDEUTSCHE ZEITUNG linaamini, kumalizika vita vya Libya, haimaanishi kuwa hata wajibu wa Ulaya na NATO umemalizika. Kwani sasa kuna changamoto mpya, kama kuhifadhi amani, kuleta upatanisho wa kitaifa na kuijenga upya nchi iliyoteketezwa.Linaongezea:

"Hiyo si kazi ndogo na itahitaji muda katika taifa lililokuwa na makundi mengi ya kikabila ambako sasa, Baraza la Mpito la Kimataifa limeshika jukumu la uongozi, lakini hata viongozi wa kikabila na ndugu wa Kiislamu wana usemi. Ni dhahiri kuwa Libya ina safari ndefu mbele yake, na bila shaka njiani, itakumbana na vikwazo."

Gazeti la SÄCHSISCHE ZEITUNG linasema, jumuiya ya kujihami NATO imesaidia kumaliza haraka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Libya na hivyo, kuzuia umwagaji zaidi wa damu. Linasema:

"Hayo ni sahihi, lakini ni sahihi pia kwa mizozo ya dunia hii kusuluhishwa kwa operesheni za kijeshi na nchi za kigeni. Cha ajabu ni kwamba takriban kila wakati, hayo yametokea kule ambako nchi za magharibi zina maslahi yake yenyewe. Kwa maneno mengine, kule kwenye mafuta. Kwa maoni ya gazeti hilo, Syria ambako hakuna utajiri wa mafuta, wapinzani wa serikali watangojea sana kupata msaada wa kijeshi kutoka angani. Inaumiza, lakini hivyo ndio mambo yanavyokwenda kawaida."

Tukigeukia mada ya wapokea pensheni nchini Ujerumani ambako baadhi yao huendelea kufanya kazi, hata baada ya kustaafu, gazeti la MAIN-POST linasema:

"Kustaafu na kupumzika ni ya kale, hatima ya siku hizi, ni kufanya kazi mpaka kufa. Katika jamii ya leo, pengo kati ya masikini na matajiri linazidi kuwa kubwa, hasa katika jamii ya wazee. Wapokea pensheni waliofanyakazi bila ya kusita, wana maisha tofauti na wale waliokuwa na ajira ya hapa na pale, mishahara midogo au walishindwa kufanya kazi kwa sababu tofauti. Wazee hao wanatoka tupu na hawana budi kufanya kazi hata baada ya kufikia umri wa kustaafu."

Lakini kwa maoni ya DRESDNER NEUSTE NACHRICHTEN, hiyo sio sababu pekee.Linaeleza hivi:

"Ukweli wa kufurahisha ni kwamba kwa wastani, umri wa kuishi umeongezeka - na wastaafu wanafurahi, pale ujuzi wao unapohitajiwa hata baada ya kufikia umri wa miaka 65 mbali na kuongezea pato lao."

Mwandishi: Martin,Prema/dpa

Mhariri: Abdul-Rahman