Liberia uchaguzini, Sirleaf mashakani | Matukio ya Afrika | DW | 11.10.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Liberia uchaguzini, Sirleaf mashakani

Matarajio makubwa yamewekwa nyuma ya mwanamke wa kwanza kuwa rais barani Afrika na mmoja kati ya washindi watatu wa Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka huu, Elein Johnson-Sirleaf, kwamba anaweza kuchaguliwa tena.

Rais Ellen Johnson-Sirleaf

Rais Ellen Johnson-Sirleaf

Mambo si rahisi kwa mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel na rais wa Liberia, Ellen Johnson-Sirleaf. Na wakosoaji wake hawapati tabu kumshambulia.

Mtaa wa Benson katika mji mkuu, Monrovia. Kama ilivyo kwenye miji mingine mikubwa duniani, watu hukaa na kujadiliana kuhusiana na wagombea wa uchaguzi, hofu na matarajio. Mmoja wao ni Jeremia Blake, mwanamme wa miaka 40, ambaye mambo yamemfika kooni.

"Hatumtaki tena Ellen Johnson-Sirleaf kuwa raia wa nchi hii. Tena kwa sababu nyepesi tu: chini ya utawala wake, Waliberia wameishi kwa umasikini mkubwa. Alipokuwa akiingia madarakani mwaka 2005, aliiahidi jumuiya ya kimataifa na Waliberia kwamba ufisadi utakuwa adui namba moja wa taifa. Hivi sasa ufisadi na yeye Bibi Sirleaf wamekuwa marafiki wakubwa." Amesema Blake.

Ahadi yake ya kutokuvumilia ufisadi hakuweza kuitimiza katika miaka yake mitano madarakani. Kinyume chake ni kuwa shirika la kimataifa la kupambana na ufisadi duniani, Transparency International, limeiweka Liberia katika nafasi ya juu kabisa kwa ufisadi duniani. Jambo hili, kwa watu kama Jeremia Blake, ni sababu ya Rais Sirleaf kuangushwa kwenye uchaguzi huu.

Mgombea wa upinzani, Winston Tubman

Mgombea wa upinzani, Winston Tubman

Nyuma ya Jeremia Blake amesimama Betty Arsen, mtoto mmoja mkononi, na mwengine mgongoni. Yeye anachotafuta kutoka kwa wagombea uraisi ni elimu tu kwa watoto wake hawa wa kike.

"Tulimchagua Bibi Sirleaf kwa matumaini kwamba angeliwasadia wanawake. Lakini maisha ni magumu sana kwetu. Ada ya masomo ni ya juu sana. Kwa msichana wangu huyu mdogo, ninalipa dola 7,000 kwa muhula mmoja, hiyo ni zaidi ya euro 70. Nami sina kazi. Ninaishi kwa biashara ndogo ndogo za hapa na pale." Anasema Betty.

Hata hivyo, bado kuna mengi ambayo raisi huyu wa kwanza wa kike barani Afrika ameweza kuyafanya kwa nchi hii iliyokuwa kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka 14. Benki ya Dunia ilikubali kuipa Liberia mkopo wa dola bilioni nne za Kimarekani.

Rais Sirleaf aliwavutia wawekezaji kuwekeza katika ardhi tajiri ya nchi hii ndogo na masikini. Mfano wa wawekezaji hao ni kampuni ya ArcelorMittal. Baadaye kidogo yakagunduliwa mafuta kwenye pwani ya Liberia. Kampuni kubwa ya mafuta ya Marekani, Chevron, ikachukuwa jukumu la uchimbaji. Vile vile, vikwazo dhidi ya almasi na magogo ya Liberia vikaondoshwa.

Lakini kwa Waliberia wengi, alichoweza kufanya Bibi Sirleaf ni kulisaidia kundi la wachache. Na hili linamfanya akose imani ya watu masikini, kama anavyosema Jeremia Blake, kwamba dau lake analiweka kwa wagombea wawili, Winston Tubman wa chama cha Congress for Democratic Change na Charles Brumsline wa chama cha Liberty.

Winston Tubman ni mkuu wa chama kikuu cha upinzani na makamo wake ni nyota wa zamani wa soka na mpinzani wa Rais Sirleaf katika uchaguzi wa 2005, George Weah.

Chama cha Congress for Democratic Change kimepata uungwaji mkono mkubwa kutokana na kuwemo kwa George Weah.

"Ni siasa safi za Kiafrika. Sera zinakuwa nyuma. Mbele anawekwa mtu mwenye nguvu, mwenye haiba, ambaye anajaribu kutumia taswira yake kuwashajiisha watu." Amesema Rudolf Elbling, ambaye ni mshauri wa ufundi katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Liberia.

Lakini, kwa hakika si siasa za Kiafrika peke yake. Ni ukweli pia kwamba umasikini umewafika Waliberia pabaya. Hivi sasa idadi ya wasiokuwa na kazi ni zaidi ya asilimia 80.

Idadi hii, hata kama si hoja kwenye chaguzi, inaweza kuleta matokeo mabaya kwa mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, Ellen Johnson-Sirleaf.

Mwandishi: Stefanie Duckstein/ZPR
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo