1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leo Magazetini hapa Ujerumani

11 Oktoba 2010

Wahariri wa magazeti ya hapa Ujerumani hii leo wameziangazia mada kadhaa yakiwemo matamshi ya Horst Seehofer kuhusu uhamiaji,ajali ya kiwanda kilichomimina tope za sumu nchini Hungary na mivutano ya kiuchumi na China.

https://p.dw.com/p/Pb39
Nembo ya kampuni ya BMW ya magariPicha: DW


Tuanze basi na gazeti la Südwest la Ulm.Gazeti hilo linaanza kwa kueleza kuwa viwanda vikubwa vya kutengeza magari katika eneo la kusini mwa Ujerumani mkoani Bavaria vinapata faida kubwa hasa magari yake yanaponunuliwa na wateja wa Uturuki na mataifa mengine ya kiarabu.

Biashara na Dini

Makampuni ya BMW,Siemens na mengine makubwa ya mkoa wa Bavaria yanapata pato kubwa kwasababu ya biashara hiyo ila matamshi ya kiongozi wa chama cha CSU-Hörst Seehofer huenda yakaubadili mtazamo wa wateja wa eneo hilo.Mhariri huyo anaeleza kuwa kauli zake kuhusu masuala ya uhamiaji na biashara kamwe hazipendezi na hilo huenda likaiathiri biashara na soko la bidhaa za Ujerumani.Mwanasiasa huyo tayari alishatoa matamshi ya aina hiyo ambayo si ya kuridhisha.Mapema Bwana Seehofer alishaligusia suala la Umoja wa Ulaya kupata wanachama wapya na jinsi linavyomkera ukizingatia kuwa Uturuki imeshawasilisha ombi lake la kuwa mwanachama.

Gazeti hilo linaendelea kueleza kuwa chama chake cha CSU kinaandaa kikao maalum kitakachofanyika mwisho wa mwezi ili kujadili masuala mengi tofauti.

Kwa mujibu wa mhariri wa Südwest,wanachama wa CSU wana mitazamo tofauti kuhusu masuala mengi yanayojumuisha kuzikumbatia tofauti za kidini zilizopo hapa Ujerumani hasahasa Uislamu na tamaduni za Kijerumani.

Gazeti hilo linamalizia kwa kusema kuwa Seehofer hana budi ila kuelezea bayana yapi yatakayoungwa mkono,mtazamo wake na washirika watakaoweza kuvumiliwa.

Tope za sumu na Wataalam

Ungarn Umweltkatastrophe Giftschlamm Flash-Galerie
Mji wa Devecser ulio kusini magharibi mwa mji mkuu wa Budapest, Hungary,kulikovuja tope za sumuPicha: AP

Likitugeuzia mada,Gazeti la Frakfurter Allgemeine linaiangazia ajali ya kiwanda cha alumini kilichovuja tope za sumu nchini Hungary.

Gazeti hilo la Berlin limeandika kuwa Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban hana jinsi ila kukiri kuwa nchi yake haina wataalam stadi wa kupambana na athari za ajali hiyo.Ushindi wake bungeni umetiwa doa na athari za ajali hiyo.Yeyote yule anayezielewa sheria za kimataifa bila shaka ataweza kujieleza ukiyazingatia matatizo ya kwake.Imebainika kuwa hakuna kampuni yoyote  inayoweza kufanikiwa kupambana na athari za mkasa huo.Sera za Waziri Mkuu Viktor Orban za masuala ya biashara zina mushkil kidogo na pia makampuni ya nchi yake nayo pia yanatatizika baadhi ya nyakati.

Uchumi na China

Mada ya mwisho inayoangaziwa na wahariri hii leo ni masuala ya uchumi na mitazamo tofauti kati ya China na Umoja wa Ulaya katika suala la uchumi na biashara.

Gazeti la Der Neue Tag linaeleza kuwa wawakilishi wa serikali ya Rais Barack Obama wa Marekani  walikuwa na wasiwasi mkubwa kwasababu China na wakawa wanatapatapa kutafuta kisingizio cha kuiwekea mipaka ya kibiashara.Kwa upande mwengine ilijaribu kujisogeza kwa Umoja wa Ulaya ili kupata sauti kubwa zaidi.Hata hivyo Waziri wa Fedha wa Marekani Timothy Geithner hakufanikiwa kulitimiza hilo kwani mosi,azma ya sera za masuala ya fedha za Marekani  ni kuhakikisha kuwa thamani ya sarafu ya dola  inaimarika.           

Mwandishi:Thelma Mwadzaya-DPA

Mhariri:Abdul-Rahman