1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leo Ghana na Uruguay na Brazil na Holland

1 Julai 2010

Je, Ghana itaandika historia kuwa timu ya kwanza kuingia nusu-finali?

https://p.dw.com/p/O8Vt
Richard Kingson kipa wa Ghana akizima hujuma za Marekani na leo za Uruguay ?Picha: AP

Duru ya 3 ya Kombe la Dunia inaanza leo alaasiri kwa mabingwa mara 5 wa Dunia-Brazil, wakipania kuipiga kumbo na kuitoa nje Holland; na tumaini pekee la Afrika-Ghana,ikiandika historia kuwa timu ya kwanza ya bara la Afrika kuingia nusu-finali ikiwa itaitoa Uruguay leo usiku huko City Stadium,Johannesberg.

Wakati mmoja ikitamba na kuhanikiza kama ni dola kuu la kabumbu duniani,Uruguay,mabingwa wa kwanza wa dunia,lilipoanzishwa huko Montevideo, 1930, wamepania leo kutamba tena baada ya kupita miaka 40.

Kabla ya Brazil na Argentina,kupepea bendera ya Amerika Kusini, Wauru ndio waliokuwa majogoo wa dimba ulimwenguni.Walitoroka kwanza na kombe la dunia nyumbani 1930 na utamu ulipowakolea, wakasema, "mramba asali-harambi mara moja." Nyumbani mwa Brazil ,Maracana Stadium, mjini Rio, Wauru, waliwachezesha wabrazil samba na kutwaa taji lao la pili 1950.

Wauru mahasimu wa Ghana usiku wa leo, wana sifa nyengine: Wametawazwa mara 2 mabingwa wa dimba wa olimpik na kuvaa taji la Amerika kusini-Copa America mara 8 kati ya mara 14 walizoshiriki.

Uruguay, isitoshe, imefika nusu-finali ya Kombe la dunia 1954 mwaka Ujerumani, ilipotwaa Kombe mara ya kwanza huko Bern, Uswisi na tena 1970 lilipochezwa Mexico-Pele akicheza mara ya mwisho kwa Brazil.

Ghana, huku Afrika nzima ikiwa nyuma yake leo usiku, inadai "Mla, ni mla leo, mla jana ,kala nini ". Ghana,inaelewa kwamba, leo ni siku yake ya kuandika historia na kuvunja rekodi za Simba wa nyika-Kameroun na Simba wa Terange-Senegal, 2002.

Wanaelewa pia kuwa mazuamri ya vuvuzela yalihanikiza kuwa, huu ni mwaka wa Afrika,lakini kwavile, wenzao wamevuliwa nguo na kufedheheshwa, nyota nyeusi-Black-Star, ndio leo kulinawirisha bara la Afrika.

Mpambano wa leo, ni wa kwanza kabisa kati ya Wauru na Waghana na timu zite mbili hakuna wapiga-ramli seuze wachawi walioona mojawapo kuwasili nusu-finali.Lakini, inawezekana.

Wakuwakodolea macho sana upande wa Wauru, ni Diego Forlan na Luis Suarez na upande wa Ghana,Asamoah Gyan na Kevin-Prince Boateg waliovunja tumbuu la lango la Marekani kuweka miadi ya usiku wa leo na wauru.Andre Ayew,mwana wa Abedi Pele,leo mwiko kucheza.

Kabla changamoto hii,itakua zamu kwanza ya mabingwa mara 5 wa dunia-Brazil, wakitamba tena na Kaka na Robinho, kupambana na wadachi-Holland .Wakati Kaka wa Real Madrid ,bado hakuwika katika kombe hili ,jogoo la Bayern Munich, Arjen Robben,limeshafumania lango la adui.Waulze Waslovakia.Ni Robben,licha ya kuchechemea kwake ,akishirikiana na Sneider,wanaotazamiwa kuwazuwia Wabrazil kusakata samba huko Copa Cabana.

Staili inayocheza Brazil katika kombe hili, imekoslewa mno na sio tu na Franz Beckenbauer,nahodha na kocha wa zamani wa Ujerumani, bali hata na mfalme Pele:Pele hafurahishwi na staili ya kocha Dunga. Alikosoa na ninamnukulu, "Staili ya leo ya Brazil ni kurudisha ghafula mashambulio"-counter-attack.

Dunga, anatetea staili yake inayoegemea ngome ya Lucio kati ya uwanja na Juan pamoja na Maicon na Bastos. Mbele yao hawa 4 ,Dunga hupenda kuwachezesha Felipe Melo na mkongwe Gilberto Silva kama kinga zaidi. Kuna shaka iwapo Melo, atakuwa fit kuzima vishindo vya wadachi alaasiri ya leo.Brazil inatilia mkazo zaidi kuimarisha ngome yake tangu Dunga kushika usukani wa timu hii. Wadachi kwahivyo, watakuwa na kibarua kigumu kuvunja tumbu.Lakini, wamewahi si mara moja ,kuitimua nje Brazil.Walifanya hivyo, 1974 wakiwa njiani kucheza finali na Ujerumani. Wapiganapo ndovu 2 -wasema -ziumiazo ni nyasi.

Mwandishi:Ramadhan Ali /DPAE

Mhariri:Abdul-Rahman