1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dola la kiislamu la ladai kuhusika na mashambulizi Lebanon

Admin.WagnerD13 Novemba 2015

Waziri mkuu wa Lebanon Tammam Salam amefanya mkutano na mawaziri wa usalama na mkuu wa majeshi nchini humo huku nchi hiyo ikiomboleza vifo vya raia wake 44 waliouawa kwenye mashambulizi mawili ya kujitolea mhanga.

https://p.dw.com/p/1H5KT
Libanon Spurensicherung nach dem Anschlag in Beirut
Picha: Getty Images/AFP

Waziri huyo mkuu aliongoza mkutano huo wa usalama huku waliohudhuria wakinyamaza kimya kwa muda kama ishara ya kuwapa heshima walioauawa.

Salam amesema mashambulizi hayo ya kikatili yaliyofanywa katika mtaa wa Burj al-Barajneh hayakulenga eneo moja au watu wa mahdhebu fulani, bali nchi nzima ya Lebanon.

Eneo lililokumbwa na milipuko hiyo ni lenye shughuli nyingi za biashara kusini mwa mji mkuu, Beirut, ambalo ni ngome ya kundi la Hezbollah.

Mashambulizi hayo ni ya kwanza kwenye ngome ya Hezbolla nchini Lebanon kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja, na yamejiri huku kundi hilo likiendelea kujihusisha na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria kwa mwaka wa tano sasa.

Kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran limetuma wanamgambo wake kuunga mkono rais wa Syria Bashar al-Assad dhidi ya makundi ya kiislamu ya madhehebu ya Sunni likiwemo dola la kiislamu la IS.

Lebanon pia inakumbwa na mzozo wa kisiasa ambapo mizozo kati ya vyama,makundi yaliyojitenga na madhehebu yamezuia serikali kufanya maamuzi muhimu na hivyo kuacha nchi hiyo bila rais kwa miezi 17.

Majeshi yalishika doria na kuzingira eneo la milipuko,ambayoo hadi asubuhi hii lilikuwa limetapakaa vifusi,magari yaliyoharibiwa,piki piki na vioo vilivyo vunjika.

Duru kutoka hospitalini zaarifu kuwa idadi ya walioaga dunia imeongezeka na kufikia 44 huku zaidi ya watu 200 wakijeruhiwa.

Waziri wa Haki Ashraf Rifi amesema baada ya kuhudhuria mkutano huo wa kiusalama kuwa wana imani kamili kwa vikosi vya usalama vya nchi hiyo ya kuhakikisha utangamano nchini humo,baada ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyomalizika mwaka 1990.

Rifi ametoa mwito kwa makundi yote ya upinzani kushirikiana katika kumchagua rais kuimarisha serikali na bunge.Taasisi za serikali nchini humo zimelemazwa kutokana na mzozo wa kisiasa.

Shule na vyuo vikuu kote nchini Lebanon zilifungwa siku nzima leo huku nchi hiyo ikiomboleza .Wataalamu wa kutafuta ushahidi waliovalia mavazi meupe walionekana wakifanya kazi katika eneo la mkasa lililokuwa limezingirwa na vikosi vya usalama.

Ghadhabu ya familia

Nazmiyeh Tarif ambaye alimpoteza binamu wake Adel Termos kwenye mlipuko wa pili amesema aliomba waliowashambulia wakutwe na maafa mabaya zaidi.

Anschlag Beirut Libanon
Wanajeshi wa Lebanon wakimkamata mshukiwa wa mashambuliziPicha: picture-alliance/AP Photo/B. Hussein

''Ni watu wasio na hisia za kibinadamu..eh mungu wape mabaya zaidi kuliko waliyotusababishia, wapige na tetemeko linaloweza kuitikisa Marekani na Saudi Arabia''Tarif amesema.

Vyombo vya habari nchini humo hata hivyo vimesema Adel Termos alijirusha kwa mshambulizi wa pili wa kujitoa mhanga baada ya kumuona akikaribia umati wa watu waliokusanyika nje ya msikiti uliolengwa na mshambulizi wa kwanza.

Katika hospitali ya Razoul al-Aazam,watu walijitokeza kuchukua miili ya wapendwa wao.Wengine walilipua risasi hewani kwa bunduki maalum nje ya hospitali hiyo,ishara kamili ya kuomboleza nchini Lebanon.

Usalama umeimarishwa katika maeneo ya kuingia mitaa ya kusini mwa Beirut huku wanajeshi wakiwataka watu kuonyesha vitambilisho na kupekua magari .

Mwandishi:Bernard Maranga/Reuters/AP

Mhariri: Gakuba Daniel