Lebanon yaahirisha tena uchaguzi wa Rais. | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.12.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Lebanon yaahirisha tena uchaguzi wa Rais.

Jaribio lengine la Bunge la Lebanon la kupiga kura kwa ajili ya kumchagua Rais wa Nchi hiyo, limeshindikana kufanyika hii leo na kikao kuahirishwa mpaka Jumamosi ya Desemba 22 mwaka huu.

default

Spika wa Bunge la Lebanon, Nabih Berri, kwa mara ya tisa mfululizo, ameahirisha zoezi la kuchagua rais wa nchi hiyo.

Wabunge wa bunge la nchi hiyo, ambao wamegawanyika, walishindwa tena kwa mara ya tisa kumchagua Rais wa nchi hiyo.

Taarifa zilizotolewa zimeeleza kuwa, Spika wa bunge la nchi hiyo, Nabih Berri aliamua kuahirisha uchaguzi huo, uliopaswa kufanyika leo, mpaka Jumamosi.

Bunge la nchi hiyo, linapaswa kukutana ili kuweza kumthibitisha, mkuu wa Majeshi ya nchi hiyo kuwa Rais wa nchi.

Jeneral Michel Suleiman, atachaguliwa na kikao hicho cha bunge kuwa rais, baada ya kukubalika na pande zote mbili zinazopingana bungeni.

Kwa mara ya kwanza, kikao cha bunge cha kumchagua Rais wa nchi, kilikuwa kifanyika mwezi Septemba, lakini hakikufanyika na badala yake kuahirishwa.

Mapema leo, wabunge wa nchi hiyo walijitokeza bungeni mjini Beirut, ili kuweza kumchagua kiongozi mpya wa Lebanon.

Dalili za kutofanyika kwa uchaguzi huo, zilionekana mapema leo, baada ya kutolewa taarifa zilizokinzana, kuhusiana na upigaji kura huo.

Wabunge walio wengi walifanya mazungumzo na Spika wa nchi hiyo ambaye ni kiongozi wa upinzani kutaka kuchaguliwa kwa rais huyo, bila kufanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo.

Uchaguzi huo, ambao umekuwa ni gumzo sasa nchini humo, pia ulitawala vichwa vya magazeti ya leo nchini humo, ambapo gazeti la kila siku la An Nahar ambalo linamilikiwa na wawakilishi wengi bungeni lilitoka na habari isemayo, Mkuu wa majeshi anakuwa rais bila ya katiba kurekebishwa, huku Gazeti la Al Anwar likibashiria mshangao katika kikao hicho cha leo cha bunge, wakati gazeti la wapinzani likisema hakuna uchaguzi wowote, utakaofanyika.

Uchaguzi huo umeelezwa kuwa hatua muhimu katika kumaliza mgogoro uliokuwepo muda mrefu ambao umedhoofisha nchi hiyo, na kuacha pengo lililosababishwa kutochaguliwa kwa rais wa nchi hiyo tangu Novemba 23, baada ya aliyekuwa akiiongoza nchi hiyo Emile Lahoud kumaliza muda wake wa uongozi na bila kuchaguliwa kwa mrithi wake.

Licha ya vyama vya siasa vinavyopingana nchini humo kwa pamoja kuamua kumchagua Jenerali Sleiman, wamekuwa wakibishana jinsi ya kurekebisha katiba ya nchi hiyo ili kumuwezesha Afisa huyo mwandamizi wa serikali kuwa Rais wa nchi.

Na pia bado hawajakubaliana jinsi ya kupanga serikali mpya na nani atachaguliwa kuongoza nafasi za juu za jeshi la nchi hiyo.

Mwishoni mwa wiki Marekani ilituma mjumbe wake nchini Lebanon kukutana na pande hizo zinazopingana ili kuwapa shinikizo kuweza kumaliza suala hilo, lenye kuleta wasiwasi wa kisiasa nchini humo tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza mwaka 1975 hadi mwaka 1990.

Mjumbe huyo wa Marekani David Welch, amesema nchi yake inaamini kuwa ni muda muafaka kwa Lebanon kuchagua rais mpya na kwamba hakuna sababu yoyote ya kuchelewesha uchaguzi huo.

Kwa upande wake Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy, amezitaka pande zote ndani na nje ya nchi hiyo kuhakikisha kuwa Lebanon inapata Rais.

Mgogoro unaoendelea kati ya pande hizo mbili nchini Lebanon uliingia katika sura mbaya zaidi wiki iliyopita baada ya bomu kulipuka katika gari na kumuua Brigedia Jenerali Michel El Hajj, ambaye alitajwa kuwa mkuu wa majeshi, endapo Jeneral Sleiman atachakuliwa kuwa Rais.

 • Tarehe 17.12.2007
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CcpL
 • Tarehe 17.12.2007
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CcpL

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com