Laurent Gbagbo afikishwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu | Matukio ya Afrika | DW | 30.11.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Laurent Gbagbo afikishwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu

Aliyekuwa rais wa Cote D' Ivoire, Laurent Gbabo amewekwa rumande mara tu baada ya kufikishwa mjini The Hague mapema leo (30.11.2011) akikabiliwa na mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita.

Laurent Gbagbo

Laurent Gbagbo

Ndege iliyompeleka Laurent Gbabo ilitua kwenye uwanja wa ndege wa Roterdam saa 10:00 alfajiri. Alisafirishwa hapo jana kutokea Korhogo, mji wa kaskazini mwa Cote d' Ivoire ambako alikuwa amewekwa katika kuzuizi cha nyumbani tokea alipoondolewa kwa nguvu madarakani mnamo mwezi wa Aprili mwaka huu.

Naibu Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Dje Noel, alisema katika mji mkuu wa Cote d'Ivoire, Abidjan, kwamba Gbagbo amepelekwa mjini The Hague chini ya ulinzi maalumu. Mapema ICC ilitoa hati ya kisheria ya kuwezesha kukamatwa kwa Gbagbo kabla ya kupelekwa mjini The Hague.

Gbagbo anadaiwa kutenda uhalifu kati ya mwezi wa Disemba mwaka jana na mwezi wa Aprili mwaka huu, kwa kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya kukataa kuondoka madarakani, licha ya kushindwa katika uchaguzi na mpinzani wake, Alassane Outtara.

Hadi kufanyika kwa uchaguzi wa mwishoni mwa mwaka jana, Gbagbo alishakuwa madarakani kwa muda wa miaka 10. Maelfu ya watu walikufa kutokana na mapigano na maelfu ya wengine walikimbilia katika nchi jirani.

Siku Laurent Gbagbo aliyokamatwa kwa mara ya kwanza, Aprili 2011.

Siku Laurent Gbagbo aliyokamatwa kwa mara ya kwanza, Aprili 2011.

Gbago, pamoja na wafuasi wake kadhaa, alikamatwa tarehe 11 Aprili baada ya majeshi yaliyokuwa yanamuunga mkono Ouattara kuivamia hoteli ambamo Gbagbo alikuwa anakaa pamoja na mkewe, Simone, ambaye bado amewekwa katika kuzuizi cha nyumbani katika mji wa Odienne uliopo kaskazini magharibi mwa Cote d'Ivoire. Mahakama za Cote d'Ivoire pia zimemfungulia Simone mashtaka ya uhalifu wa kiuchumi, ikiwa pamoja na uporaji, ujambazi na wizi wa fedha.

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limesema kupelekwa kwa Gbagbo kwenye Mahakama ya ICC mjini The Hague ni hatua muhimu katika kuleta haki. Mjumbe wa shirika hilo, Elise Keppler, amesema leo ni siku ya furaha kubwa kwa wahanga wa uhalifu uliotendwa baada ya kufanyika uchaguzi nchini Cote d'Ivoire.

"Kupelekwa kwa Gbagbo kwenye mahakama ya mjini The Hague kunatoa onyo kwa viongozi wa kisiasa na kijeshi kwamba hakuna anayeweza kuwa mkubwa kuliko sheria", amesema Keppler.

Hata hivyo, mwenyekiti wa Jumuiya ya Kutetea Haki za Binadamu nchini Cote d'Ivoire, Rene Okou Legre, amesema nchi hiyo bado inakabiliwa na matatizo mengi.

"Matatizo bado hayajatatuliwa. Mfarakano katika jamii bado ni wa kina kirefu. Baada ya vita siyo rahisi kwa watu kuinuka na kusonga mbele.Jamii imesambaratika na hasa magharibi mwa nchi, ambako mfarakano una mizizi mirefu. Bado wapo watu wenye silaha katika sehemu hiyo wanaoweka mbele matumizi ya nguvu badala ya mazungumzo." Amesema Legre.

Mwandishi: Abdu Mtullya/DPAE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

 • Tarehe 30.11.2011
 • Mwandishi Abdu Said Mtullya
 • Maneno muhimu Gbagbo ICC
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/13JPE
 • Tarehe 30.11.2011
 • Mwandishi Abdu Said Mtullya
 • Maneno muhimu Gbagbo ICC
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/13JPE