1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lahm astaafu kutoka soka la kimataifa

18 Julai 2014

Baada ya kurudi nyumbani na Kombe la Dunia mikononi mwake, nahodha wa timu ya taifa ya Ujerumani Philipp Lahm amestaafu kutoka soka la kimataifa. Hayo yamethibitishwa na Shirikisho la Soka Ujerumani

https://p.dw.com/p/1CezV
Philipp Lahm
Picha: Reuters

Beki huyo wa Bayern Munich mwenye umri wa miaka 30 amefanya uamuzi huo, baada ya kumpigia simu rais wa DFB Wolfgang Niersbach.

Niersbach alimshukuru kwa mchango wake wa miaka kumi katika timu ya Ujerumani ambapo pia aliibuka kuwa kielelezo kwa chipukizi wengine. Kushinda Kombe la Dunia ni kama kilele cha kazi yake ya kandanda kufikia sasa, ambayo inajumuisha pia taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, mataji sita ya Bundesliga na sita ya Kombe la Shirikisho la Soka Ujerumani.

Lahm alianza kazi yake ya kandanda mnamo Februari 2004 katika ushindi wao wa mabao mawili kwa moja dhidi ya Croatia. Kisha akaichezea Ujerumani mechi 113 na kufunga magoli matano. Kabla ya kushinda Kombe la Dunia la 2014, Lahm na timu yake waliibuka washindi wa tatu Kombe la Dunia mwaka wa 2006 na 2010, na wakawa makamu bingwa wa dimba la Euro 2008. Pia alicheza katika Euro 2004 na 2012.

Mkataba wa Lahm na mabingwa wa Bundesliga Bayern ulirefushwa kabla ya Kombe la Dunia na utakamilika mwaka wa 2018.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Mohammed Khelef