1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Löw amuita Weidenfeller katika timu ya Ujerumani

8 Novemba 2013

Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Löw amemwita kikosini Roman Weidenfeller kwa mara ya kwanza. Mlinda lango huyo wa Borussia Dortmund ataichezea Ujerumani mechi za kirafiki dhidi ya Uingereza na Italia

https://p.dw.com/p/1AEJL
Picha: picture-alliance/augenklick/firo Sportphoto

Löw, amesema Weidenfeller mwenye umri wa miaka 33 hatimaye ameanza kupata fursa yake ya kuichezea timu ya taifa. Amesema mchezo wake katika klabu ya Dortmund ambao sasa iko katika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi, umekuwa mzuri kiasi cha kutoweza kupuuza.

Ijapokuwa mlinda lango wa Bayern Munich Manuel Neuer anasaliwa kuwa kipa nambari moja wa Ujerumani, Löw amesema sasa Weidenfeller ana jukumu la kupigania nafasi yake ya kuwa mlinda lango wa akiba au nambari tatu katika timu ya taifa kabla ya tamasha la dimba la dunia nchini Brazil hapo mwakani.

pia amemwita kikosini mshambuliaji Miroslav Klose baada ya kupona jeraha lakini kiungo Bastian Schweinsteiger bado yuko nje. Klose, mchezaji mwenye uzoefu mkubwa mwenye umri wa miaka 35 wa klabu ya Lazio, anarejea kikosini baada ya kuwachwa nje ya mechi za kufuzu kwa dimba la dunia mwezi uliopita, dhidi ya Jamhuri ya Czech na Sweden.

Sasa ana fursa ya kuweka rekodi ya mfungaji wa magoli mengi nchini Ujerumani, ambapo kwa sasa anatoshana na Gerd Mueller wote wakiwa na magoli 68. kiungo wa Bayern Bastian Schweinsteiger anahitaji kufanyiwa upasuaji kwenye kifundo chake cha mguu.

Kikosi cha Löw kinamjumuisha kipa wa Borussia Dortmund Roman Weidenfeller. Licha ya kukosekana kwa Schweinsteiger, Bayern wana wachezaji sita kwenye orodha ya Löw wakiongozwa na nahodha Phillip Lahm. Arsenal inawakilishwa na wachezaji wawili Mesut Ozil na Per Mertesacker, huku pia Premier League ikiwakilishwa na mchezaji mwngine kwa jina Andre Schuerrle wa Chelsea.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters

Mhariri: Josephat Charo