1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura ya maoni yaingia siku ya pili, Misri

Mjahida15 Januari 2014

Raia wa Misri wanapiga kura kwa siku ya pili na ya mwisho katika kura ya maoni juu ya katiba mpya, huku serikali ikisema kura hiyo inanuiwa kurejesha utawala wa kidemokrasia, baada ya kuondolewa Mohammed Mursi.

https://p.dw.com/p/1AqkP
Mwanajeshi akiangalia vitambulisho vya wapiga kura kiabloa ya kushiriki katika zoezi.
Mwanajeshi akiangalia vitambulisho vya wapiga kura kiabloa ya kushiriki katika zoezi.Picha: picture-alliance/dpa

Idadi ndogo ya watu imejitokeza katika vituo vya kupiga kura katika saa ya kwanza ya upigai kura hii leo Jumatano.

Kulingana na maafisa wa afya, zaidi ya watu kumi waliuwawa huku wengine 40 wakijeruhiwa baada ya mapambano kati ya maafisa wa polisi na wafuasi wa rais wa zamani Mohammed Mursi, katika siku ya kwanza ya zoezi hilo hapo jana.

Kura hii ya maoni inayofanyika kwa siku mbili inakuja baada ya miezi sita tangu kuondolewa madarakani kwa Mursi ambapo wafuasi wake, wamesusia kura hiyo na kusema hawatatambua matokeo yake.

Kundi hilo la udugu wa kiislamu hivi maajuzi lilipigwa marufuku na serikali ya Misri na kuitwa kundi la kigaidi.

Mmoja wa wafuasi wa Mohammed Mursi
Mmoja wa wafuasi wa Mohammed MursiPicha: Khaled Desouki/AFP/Getty Images

Hata hivyo kundi hilo limewataka wafuasi wake kujitokeza barabarani na kupinga kura hiyo ya maoni.

Kwa upande wake Serikali ya isri imeapa kutovumilia matokeo yoyote yanayonuiwa kusambaratisha zoezi hilo.

Usalama Waimarishwa katika zoezi la kura ya maoni

Jumla ya maafisa wa usalama 250,000 wamesambazwa kwa zaidi ya vituo vya kupigia kura 30,000 kote nchini humo.

Iwapo kura hiii ya maoni itapitishwa itachukua nafasi ya katiba iliokuwa hapo awali ya mwaka 2012 iliopatikana chini ya uongozi wa Mohammed Mursi, rais wa kwanza aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia nchini Misri.

Baada ya kupinduliwa kwa Mohamed Mursi maandamano na ghasia zilianza kushuhudiwa zilizosababisha mauaji ya wengi. Wafuasi wa Mursi walitaka kiongozi wao arejeshwe Madarakani.

Kwa wengi, kura hii imegeuka kuwa kura ya imani kwa mkuu wa jeshi Abdel-Fathah al-Sisi, jenerali aliemuondoa Mohammad Mursi mwezi Julai.

Inasemekana al Sisi kwa sasa ana nia ya kugombea urais nchini humo na wengi wanamuona kama mtu anayeweza kudhibiti hali katika nchi hiyo ya kiarabu.

Maafisa wa usalama nje ya kituo cha kupigia kura
Maafisa wa usalama nje ya kituo cha kupigia kuraPicha: Reuters

Milioni 53 ya raia nchini humo wana haki ya kupiga kura katika kura hii ya maoni juu ya katiba mpya ilioanza hapo jana na kuendelea hii leo.

Iwapo katiba hii mpya itapitishwa, itatoa haki kwa wanawake, uhuru wa kuabudu na uhuru wa kujieleza.

Lakini inasemekana kuimarisha nguvu za jeshi, ikilipa mamlaka ya kumteua waziri wa ulinzi kwa kipindi cha miaka minane ijayo, na kuwashtaki raia kwa mashambulizi dhidi ya maafisa wa kijeshi.

Aidha Matokeo ya kura ya maoni yanatarajiwa kutolewa siku ya Jumamosi.

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/AP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman