1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

''Kura ya Maoni'' kuhusu uhuru mashariki ya Ukraine

11 Mei 2014

Majimbo mawili yenye mvutano mkubwa mashariki mwa Ukraine yanapiga ''Kura ya Maoni''juu ya kujitangazia uhuru, huku rais wa mpito wa Ukraine akionya kuwa hatua hiyo inayapeleka majimbo hayo kwenye maangamizi.

https://p.dw.com/p/1Bxkz
Visanduku vya kupigia ''kura ya maoni'' kuhusu uhuru wa majimbo ya mashariki
Visanduku vya kupigia ''kura ya maoni'' kuhusu uhuru wa majimbo ya masharikiPicha: Brendan Hoffman/Getty Images

Kura hiyo inataka ridhaa ya raia juu ya kile kilichoitwa uhuru wa jamhuri za umma katika majimbo ya Donetsk na Luhansk, ambako wanaharakati wanaoiunga mkono Urusi wameyateka majengo ya serikali na kupambana na vikosi vya usalama vya Ukraine.

Kura hiyo inasimamiwa na vuguvugu la waasi na haitambuliwi na serikali mjini Kiev, wala nchi za magharibi. Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani Jen Psaki amesema Marekani haitayambua matokeo ya ''kura hiyo isiyo halali'' na kuongeza kura hiyo ni jaribio la kuigawa zaidi Ukraine na kuizidishia mgogoro.

Mkuu wa mchakato wa uchaguzi wa wanaharakati wanaotaka kujitenga katika jimbo la Donetsk Roman Lyagin amekaririwa na vyombo vya habari akisema upigaji kura ulianza mapema katika mji wa Mariupol na wilaya nyingine moja kwa sababu ya mvutano mkubwa katika maeneo hayo.

Mkuu wa uchaguzi wa waasi wanaotaka uhuru wa majimbo ya mashariki, Roman Lyagin
Mkuu wa uchaguzi wa waasi wanaotaka uhuru wa majimbo ya mashariki, Roman LyaginPicha: Reuters

Hatua kuelekea gizani

Katika tangazo la rais wa mpito wa Ukraine Oleksandr Turchynov kupitia tovuti ya Ikulu hapo jana, rais huyo alisema wale wanaotaka kujitenga kwa majimbo ya mashariki hawajui kwamba hatua hiyo itasababisha kusambaratika kwa uchumi na mfumo wa kijamii kwa raia wengi. ''Hii ni hatua kuelekea kwenye lindi kuu'', alisema rais Turchynov.

Kura hiyo iliyoandaliwa kwa pupa inafanana na ile iliyopigwa mwezi Machi katika jimbo la kusini mashariki la Crimea ambayo iliidhinisha kujitenga na Ukraine, na kujiunga na Urusi siku chache zilizofuata.

Mlango wa mazungumzo

Serikali ya sasa mjini Kiev iliingia madarakani baada ya maandamano ya muda mrefu yaliyomuondoa madarakani rais Viktor Yanukovych ambaye aliegemea upande wa Urusi.

Alexandr Turtschynov, rais wa mpito wa Ukraine
Oleksandr Turchynov, rais wa mpito wa UkrainePicha: picture-alliance/Itar-Tass/Maxim Nikitin

Urusi na watu wengi wa mashariki mwa Ukraine walilaani serikali hiyo, wakiita kundi la watu wenye msimamo mkali wa kizalendo ambao wana nia ya kukandamiza haki za raia wanaozungumza lugha ya kirusi.

Rais wa mpito Turchynov alisema jana Jumamosi kuwa serikali iko tayari kufanya mazungumzo na wawakilishi wa watu wa mashariki, isipokuwa wale aliowaita ''magaidi ambao nia yao ni kuiharibu Ukraine''.

Serikali ya Kiev imeituhumu Urusi kwa kuchochea na kuongoza machafuko mashariki mwa nchi hiyo kwa lengo la kuiyumbisha Ukraine au kutafuta kisingizio cha kushambulia, tuhuma ambazo Urusi imezikanusha.

Hata hivyo, waandalizi wa kura hii katika majimbo ya mashariki wamesema uamuzi wa kutumia uhuru wao kujiunga na Urusi au kubaki sehemu ya Ukraine lakini yenye mamlaka makubwa ya ndani, utafikiwa baadaye.

Mwandishi: Daniel Gakuba/APE/AFPE

Mhariri:Caro Robi