1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura ya maoni juu ya kaitba yafanyika leo Misri

Josephat Charo26 Machi 2007

Wamisri leo wanapigia kura mabadiliko ya kikatiba yaliyozusha utata ambayo serikali ya Misri inasema yanaendeleza demokrasia. Upinzani nchini humo unadai mabadiliko hayo yatabana uhuru wa raia.

https://p.dw.com/p/CHHZ
Rais Hosni Mubarak wa Misri
Rais Hosni Mubarak wa MisriPicha: AP

Hakukuwa na dalili za wapigaji kura kukimbilia maelfu ya vituo vya kupigia kura nchini Misri hii leo saa chache baada ya vituo kufunguliwa mwendo wa saa mbili asubuhi. Mjini Cairo idadi ya wapigaji kura vituoni ilikuwa ndogo huku kukiwa na msongamano mkubwa wa magari na usalama ukiwa umeimarishwa. Msongamano huo umesababishwa na hatua kali za usalama zilizochukuliwa na serikali. Upigaji kura ulitarajiwa kushika kasi leo mchana wakati serikali ilipoanza kuwapeleka wafanyakazi wake vituoni kutumia mabasi.

Katika kituo cha shule kubwa mjini Alexandria maafisa wa uchaguzi wamesema watu 53 pekee wamepiga kura kati ya wapigaji kura 3,576 waliojiandikisha. Rais Hosni Mubarak, mkewe Suzanne, na mwanamwe wa kiume, Gamal, wamepiga kura katika kitongoji cha Heliopolis, kaskazini mashariki mwa Misri, anakoishi rais Mubarak.

Mwezi Disemba mwaka jana, rais Hosni Mubarak aliliuliza bunge libadili ibara 34 za katiba kama sehemu ya mageuzi ya kisiasa. Mageuzi hayo makubwa kikatiba ni ya kwanza kuwahi kufanywa tangu mwaka wa 1971. Yalipitishwa na bunge linalodhibitiwa na chama tawala cha rais Hosni Mubarak wiki iliyopita, na yamekosolewa na Marekani na kusababisha miito ya upinzani kutaka kura ya maoni igomewe.

Chama kikubwa cha upinzani nchini Misri, Islamic Brotherhood, kimesema kitafanya maandamano licha ya marufuku ya serikali, hivyo kusababisha wasiwasi wa kuzuka mapigano baina ya wafuasi wa chama hicho na polisi kama yale yaliyozuka wakati wa kura ya maoni juu ya katiba mnamo mwezi Mei mwaka juzi.

Katika kura ya maoni wapigaji kura hii leo hawaamui juu ya kila ibara lakini wanatakiwa wapige kura aidha kuyaunga mkono au kuyapinga mageuzi yote yaliyoandaliwa na rais Mubarak na chama chake tawala cha National Democratic, NDP. ´Naapa kwa Mungu sijui napigia kura kitu gani, amesema Abdel Salaam, mchoraji wa mjini Cairo. ´Kama sitapiga kura pengine nitapata matatizo,´ ameongeza kusema mwanamume huyo.

Ina maana gani? ameuliza Abdallah, dereva wa teksi mjini Cairo wakati alipokuwa akipeleka teksi yake kwenye barabara za mjini humo zilizojaa maafisa wa polisi wa kupambana na fujo. ´Matokeo ya kura zote za maoni hujulikana kabla kura yenyewe kupigwa,´ ameongeza kusema dereva huyo wa umri wa miaka 50. ´Wamisri tunajua kinachoendelea lakini hatuwezi kusema lolote isije tukakamatwa na kutupwa gerezani,´ akamalizia kusema.

Jana mwana wa kiume wa rais Mubarak, Gamal, aliwatolea mwito Wamisri wajitokeze kwa wingi kushiriki katika kura hiyo ya maoni, akisema mageuzi ya katiba ni hatua muhimu kuelekea mageuzi zaidi kisiasa.

Wakosoaji wa mageuzi hayo wanasema Wamisri hawatalindwa tena dhidi ya kuingiliwa na serikali na uhuru wao kushiriki katika siasa utabanwa zaidi. Baadhi ya wakosoaji wanasema mageuzi hayo ni juhudi ya kuibadili Misiri iwe taifa la kipolisi.

Rais Hosni Mubarak na chama chake cha NDP anasema mageuzi hayo yanalenga kuzuia Uislamu usitumiwe vibaya kwa maslahi ya kisiasa. Serikali ya rais Mubarak inahoji kwamba kwa kuongeza mamlaka ya polisi kuhusiana na kuwakamata washukiwa na kufanya misako ya nyumba kwa nyumba, mageuzi hayo yatasaidia kupiga vita ugaidi.