1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi la waasi wa Darfur latishia hujuma nyingine dhidi ya Khartoum

Kalyango Siraj12 Mei 2008

Sudan imevunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Chad

https://p.dw.com/p/DyQJ
Rais Omar el-Bashir wa Sudan. Serikali yake imevunja uhusiano wake wa kibalozi na Chad baada ya kuilaumu kuunga mkono waasi wa Darfur wa JEM waliofanya hujuma ya kwanza dhidi ya mji wa Khartoum mwishoni mwa wiki.Picha: AP

Kiongozi wa kundi la waasi wa Darfur ambalo lilifanya mashambulizi dhidi ya mji mkuu wa Sudan wa Khartoum mwishoni mwa juma, amesema kuwa atafanya hujuma nyingine dhidi ya mji huo hadi serikali ya sasa itakapoondolewa.

Hata hivyo serikali inasema waasi wametawanyika.

Kiongozi huyo wa kundi la Justice and Equality Movement JEM Khalid Ibrahim, ametoa onyo hilo jumatatu akitumia simu ya setilaiti akionya kuwa kundi lake litaendeleza mapambano dhidi ya mji mkuu hadi kuung'oa utawala wa rais Omar Al Bashir.

Kiongozi huyo ambae kundi lake la JEM lilihujumu Omdurman ambacho ni kiunga cha magharibi mwa jiji kuu la Khartoum,amesema kuwa kuna shambulio lingine linalonukia.

Hata hivyo hakuna taarifa huru kuthibitisha aliko kiongozi huyo ambae amedai kuwa yuko Omdurman.

Kiunga hicho kimekuwa tulivu usiku kucha na maafisa wa serikali wanasema waasi wote waliofanya hujuma wamekimbia.

Shahidi moja amesema jumatatu kuwa vikosi vya usalama vimelizingira jengo moja ambapo inafikiriwa ndiko wamejificha watu ambao wanaweza kuwa waasi.

Serikali ya Sudan inailaumu jirani yake Chad kwa kuwaunga mkono waasi ambao wamefanya shambulio hilo la kwanza katika mji huo wa Khartoum.Inasemekana takriban watu 65 sio wameuawa hadi sasa.

Serikali ya Sudan pia imechukua hatua zingine za kujihami dhidi ya waasi kama vile kumtia mbaroni, kiongozi wa upinzani Hassan al-Turabi na vigogo wengine wanne wa chama chake.

Kundi la waasi la JEM linaajenda fulani ya uislamu na baadhi ya viongozi wake walikuwa washirika wa Turabi katika kipindi kilichopita.Hata hivyo yeye amekanusha madai hayo.

Matukio haya mapya yanakuja wakati juhudi za kisiasa za kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa Darfur.Baadhi ya wahusika,mfano wa mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa wa Darfur Jan Eliasson, wanaona kama matokeo haya yanatishia juhudi kama hizo.

Waasi hao walitoka Darfur umbali wa kilomita 600 na kufanya hujuma hiyo,jumamosi ambapo utawala wa Khartoum unasema wasingeweza kufanya hivyo bila msaada wa Chad na wakati huo kuvunja uhusiano wa kidplomasia na N'Djamena.

Lakini serikali ya rais Idris Deby imekanushwa kuhusika na kushangazwa na hatua ya haraka ya Khartoum ya kuvunja uhusiano wa kibalozi,ingawa wachambuzi wa mambo wanasema huenda iliwasaidia waasi wa JEM ili kulipiza kisasi cha shambulio la waasi dhdi ya mji mkuu wa Chad miezi mitatu iliopita.

Marais wa Chad na Sudan walisaini mkataba wa kutoshambuliana mwezi Machi.Lakini kila mmoja anamlaumu mwingine kwa kuvunja mkataba huo kwa kuunga mkono kundi la waasi wanaotaka kuwaondoa madarakani.

Maafisa waserikali wa Sudan wameliondoa kundi la JEM katika mchakato wa kutafuta amani kutokana na shambulio la mwishoni mwa juma.