1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi la Taliban ladai uhuru wa habari.

Sekione Kitojo11 Machi 2007

Kundi la wapiganaji la Taliban , kundi la wanaharakati wa Kiislamu ambao waliitawala Afghanistan kati ya mwaka 1996 na 2001 na hivi sasa ni kundi la waasi , limeonyesha sura ya kisiasa wakati walipomteka nyara mwandishi raia wa Italia wiki hii.

https://p.dw.com/p/CHIR
Wanajeshi wa Marekani na NATO wakijitayarisha kufanya mashambulizi yao ya majira ya machipuko nchini Afghanistan.
Wanajeshi wa Marekani na NATO wakijitayarisha kufanya mashambulizi yao ya majira ya machipuko nchini Afghanistan.Picha: AP

Sura inayotoa Taliban kutokana na tukio hili la utekaji nyara na ukweli kwamba mmoja kati ya viongozi wao wa ngazi ya juu analishughulikia suala hili, imezidisha hali ya wasi wasi juu ya hatma ya Daniele Mastrogiacomo.

Mastrogiacomo, mwenye umri wa miaka 52 aliwasiliana kwa mara ya mwisho na gazeti lake, linalojulikana kama La Republica lenye makao yake makuu mjini Rome, siku ya Jumapili , wakati alipoliambia kuwa siku inayofuata atakuwa na mkutano ambao una shaka kidogo.

Siku ya Jumanne , Taliban walisema kuwa wamemkamata Mastrogiacomo kwa kuingia katika eneo lao , wilaya ya Nadi Ali katika jimbo la kusini la Helmand bila ya ridhaa yao , na kwamba anahojiwa kwa madai kuwa alikuwa anafanya upelelezi kwa ajili ya jeshi la Uingereza.

Maneno yaliyotumiwa na Taliban yanaelemea katika mamlaka ya kisiasa ambayo inajiona kuwa inaudhibiti katika eneo Fulani, na ambayo inapambana katika vita dhidi ya wale ambao inawaona kuwa ni wavamizi, majeshi ya Marekani na NATO.

Siku ya Jumanne majeshi ya washirika wa Marekani ya NATO na majeshi ya Afghanistan yalianza mashambulizi yao ya majira ya machipuko, yaliyopewa jina la Achilles. Operesheni hiyo inahusisha kiasi cha wanajeshi wa kigeni 4,500 na wanajeshi wapatao 1,000 wa Afghanistan.

Taliban imeripoti kuwa utekaji nyara huo uliongozwa na Mullah Dadullah, ambaye anafikiriwa kuwa ni kamanda wa kundi hilo na kiongozi namba mbili baada ya kiongozi wa muda mrefu mwenye heba Mullah Omar.

Ujumbe uliowekwa katika mkanda wa kunasia sauti, huenda kwa kutumia sauti ya kamanda Dadullah uliwasilishwa siku ya Jumatano kwa mwandishi habari wa shirika la habari la AFP nchini Pakistan.

Ujumbe huo unadai kuwa Mastrogiacomo amekiri kuwa alikuwa anafanya upelelezi kuhusu maeneo ya Taliban ili majeshi ya Uingereza yaweze kuwashambulia.

Mhariri wa gazeti la La Republica Ezio Mauro amesema kuwa Mastrogiacomo ni mwandishi wa habari za vita ambaye kila mara amekuwa akiandika habari huko Iraq, Lebanon, mashariki ya kati na Afghanistan na kwamba amefanyakazi na gazeti hilo kwa muda wa miaka 27 na sio na jeshi ama idara ya upelelezi ya nchi yoyote ile.

Shutuma hizo za Taliban zinaweza kuwa mtego ili kuhalalisha operesheni pana zaidi ya kisiasa, kama sauti katika ukanda huo inayodhaniwa kuwa ya Dadullah inavyosema kuwa mataifa ya magharibi yametoa uhuru kwa vyombo vyao vya habari, lakini sio kwa Taliban , ikiwa na maana kuwa wanataka uhuru kamili wa habari, suala ambalo Taliban inasema ama iwe uhuru kamili ama uhuru huo uondolewe.

Msemaji katika ukanda huo amesema kuwa haikubaliki kuwa watoaji habari wa Taliban wamewekwa jela wakati waandishi wa habari wa mataifa ya magharibi wako huru.

Alikuwa anazungumzia kuhusu msemaji wa Taliban Mohammed Hanif , aliyekamatwa Januari, na Abdul Latif Hakimi, aliyekamatwa Oktoba 4, 2005 ambaye amedai kuachiliwa huru.

Watu hao wote wawili wamekuwa mara kwa mara wakiwasiliana na vyombo vya habari vya Afghanistan na vile vya kimataifa, kwa simu.

Hata hivyo Dadullah ameongeza kuwa suala la mwanzo kujadiliwa litakuwa iwapo vyombo vya habari view huru ama la. Baadaye wataamua juu ya hatma ya mfungwa wao.