1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi la IS lasambaratishwa nchini Iraq na Syria

20 Oktoba 2017

Kundi linalojiita dola la kiislamu IS linaonekana kuishiwa nguvu wakati huu ambapo makabiliano makali yanaendelea kati yao na vikosi vya jeshi na wapiganaji nchini  Iraq na Syria.

https://p.dw.com/p/2mFut
Irak Kampf um Mossul
Picha: picture-alliance/Kyodo

Haya yanajiri baada ya miji mikuu iliyokuwa chini ya kundi hilo la IS katika mataifa hayo kukombolewa. Sasa kuna matumaini ya ushindi dhidi ya kundi linalojiita dola la kiislamu IS nchini Iraq na Syria.

Kundi hilo lililohusika na baadhi ya maovu dhidi ya raia, sasa linaonekana kusambaratishwa.

Baada ya kuwatendea ukatili wenyeji walioishi chini ya amri yao kwa zaidi ya miaka mitatu, wapiganaji hao sasa wanangángána kubakia katika maeneo madogo nchini Iraq na Syria, iliyozingirwa na wanajeshi wa ndani kutoka pande zote.

Wachache, hata hivyo, wanatarajia kundi hilo kuondoka kabisa au umwagikaji damu kumalizika katika nchi hizo mbili na ukanda mzima.

Wacha tutazame kwa undani kikundi hicho cha dola la kiislamu, kupanda na kuathirika kwa nguvu zake za kujenga dola la kiislamu na nini cha kutarajiwa.

Kundi la IS lililotokana na baadhi ya wale waliokuwa katika kundi la kigaidi la al Qaeda nchini Iraq kilianza kuenea mashariki mwa kati mapema mwaka wa 2014, kwa kuuteka mji wa Falujah na maeneo yenye kuuzunguka mji wa Ramadi.

Mnamo mwezi juni, kundi hilo likauteka Mosul ambao ni mji wa pili mkubwa Iraq, ambapo kiongozi wake Abu Bakr al-Baghdadi alipojitangazia dola la kiislamu.

Kundi hilo likaahidi haki na usawa pamoja na kufuata muongozo wa kiislamu lakini hakutimiza hilo. Kwa miaka michache waliwatesa watu waliokuwa chini yao ikiwa ni pamoja na kuwaua na kuwanyanyasa kingono wanawake na wasichana na miongoni mwa ukatili mwengine walioufanya.

Kikundi hicho pia kilivutia watu wa kila aina wakiwemo wapiganaji wa kigeni na kuundwa kwa IS kulikuwa kwa mkakati na hatimaye ikajitanua kimataifa.

Kilichosalia

Marekani ilizindua kampeni ya mashambuzi ya angani dhidi ya IS nchini Iraq mwezi Agosti mwaka wa 2014. Na mwezi mmoja baadaye nchini Syria.

Nchini Iraq marekani ilishirikiana na vikosi vya serikali vikifanya kazi na kundi la washia pamoja na wapiganaji wa kikurdi maarufu kamapeshmerga. Nchini Syria ilishirikiana na wapiganaji wakisyria wanaongozwa na wakurdi SDF.

Vikosi hivi vimefanikiwa kuwaondoa wanamgambo wa IS kutoka ngome moja hadi nyengine kwa miaka mingi. Pigo kubwa lilikuja mwezi Julai  wakati mji wa Mosul ambao kwa muda mrefu umeonekana kuwa mji wa utawala wa IS kuachiliwa huru.

Nchini Syria kundi la IS limeonekana kuishiwa nguvu wakati ambapo vikosi vya wapiganaji wakisyria wanaongozwa na wakurdi vikishirikiana na marekani na vikosi vya serikali ya Syria vikiungwa mkono na washirika wao wa kirusi vinawashambulia kwa mapigo tofauti kwa wakati mmoja.

Irak Kampf um Mossul gegen den IS
Uharibifu mkubwa wa mijiPicha: Getty Images/A. Al-Rubaye

Gharama Kubwa

Mapambano dhidi ya IS umekuja kwa gharama kubwa kwa mataifa ya Syria na Iraq, na mateso makubwa kwa wale waliovumilia utawala wa kikatili wa wanamgambo hao. Mapigano na makombora ya angani yameharibu miji iliyokuwa imekuwa na kuyageuza kuwa maeneo yasiotizamika.

Wiki mbili zilizopita muungano ukiongozwa na marekani ulitangaza umeirudisha asilimia 83 ya ardhi iliyokuwa ikitumiwa na kundi la IS kwa wananchi wa eneo hilo tangu mwaka wa 2014, na kuwaokoa zaidi ya wasyria na wairaqi milioni 6 katika mchakato huo.  Takriban wananchi 735 wameuawa bila kukusudia kutokana na mashambulizi ya ndege ya jeshi la muungano likiongozwa na marekani ingawa wanaharakati na wachunguzi wa vita wanakadiria kuwa idadi hiyo imeongezeka.

Katika miaka mitatu, tangu kundi la IS lianze kuunda dola la kiislamu , limewaua maelfu ya watu, limesababisha mamilioni kukimbia makazi yao na kufanya bidii kuwashawishi watoto kwa kuwafunza itikadi kali ya kidini.

Kupanuka kwa kundi hilo, na vita vya mara kwa mara pamoja na miungano iliyoundwa kuikabili IS imeathiri mweleko wa kisiasa na wa madhehebu nchini Syria na Iraq.

Vikosi vyote vinavyokabiliana na kundi hilo vitalazimika kuwa macho hata baada ya kuukomboa mji wa mwisho uliyokuwa chini ya IS. Kwa namna fulani sasa wanakabiliwa na changamoto kubwa zaidi. Wachambuzi wanasema wapiganaji hao watasubiri muda mwafaka kujizindua upya au kutekeleza mashambulizi ya kujitolea muhanga.

Mwandishi: Fathiya Omar/APE

Mhariri: Iddi Ssessanga