1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi la G11 kukutana Jordan

Thelma Mwadzaya17 Mei 2007

Viongozi wa mataifa ya Kiarabu na Ulimwengu wanakutana nchini Jordan katika Kongamano la masuala ya Kiuchumi.Mkutano huo unalenga kujadilia mbinu za kupanua biashara vilevile kutafuta amani katika eneo la Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/CHEC

Wawakilishi wa kundi la mataifa 11 yanayoendelea wanakutana pembezoni mwa kongamano hilo linaloanza hii leo na kumalizika jumapili.Jumla ya washiriki 50 wanatarajiwa kuhudhuria.

Mada ya mkutano huo wa kila mwaka ni kupanua biashara kwa madhumuni ya kufanikisha juhudi za kuimarisha uchumi vilevile umuhimu wa kudumisha usalama.Mfalme Abdullah wa 2 anafungua rasmi kikao hicho huku akitoa wito kwa washiriki kutia juhudi zaidi uongozini kusuluhisha migogoro,ushirikiano wa kiuchumi vilevile maendeleo.

Mkutano huo wa G11 unashirikisha mataifa ya Croatia,Ecuador,Georgia,Honduras,Indonesia,Jordan,Morocco,Paraguay,Sri lanka na Tunisia unapahwa kufanyika hapo kesho.Mataifa tisa wanachama wamethibitisha kuwa wanahudhuria kikao hicho.

Kongamano hilo linalenga kupunguza madeni ya mataifa wanachama,kupambana na umasikini vilevile kuimarisha hali ya maisha ya wakazi.Aidha masuala ya maendeleo ya kisiasa ,ghasia vilevile migogoro katika eneo la Mashariki ya Kati yanapangwa kujadiliwa.

Suala jengine litakalojadiliwa ni mabadiliko ya wajibu wa Marekani nchini Iraq katika kipindi cha miaka mitano iliyopita aidha kutathmini matokeo ya maendeleo katika eneo la Mashariki ya Kati linalokumbwa na ghasia.

Wajibu wa viongozi wa kisiasa kutoka Mataifa ya Kiarabu katika juhudi za kutafuta suluhu ya matatizo yanayokumba eneio hilo vilevile kujiondoa kwa mataifa ya Magharibi nao upo katika ratiba ya mkutano huo.

Mkutano wa mwaka jana uligubikwa na mazungumzo kuhusu mvutano kati ya Israel na Palestina..mkutano wa mwaka huu unanuia kuwaleta pamoja Rais wa Palestina Mahmoud Abbas na Waziri wa mambo ya kigeni wa Israel Tzipi Livni.Bwana Abbas anatarajiwa kutoa hotuba yake mwishoni mwa mkutano huo kufuatia ghasia zinazokumba Palestina tangu jumapili iliyopita.

Masuala ya kiuchumi yanajadiliwa ili kutathmini umuhimu wa ongezeko la pato la mafuta kwa nchi husika.Mataifa hayo yanataraji kuzungumzia namna ya kutafuta mbinu nyingine za biashara ili kutoegemea zaidi katika biashara ya mafuta.

Kulingana na ripoti ya Kongamano hilo iliyotolewa mwezi Aprili Emarati inaongoza kiuchumi ikilinganishwa na mataifa mengine ya Arabuni na kufuatiwa na Qatar na Kuwait.Hata hivyo Emarati inachukua nafasi ya 29 kiuchumi ulimwenguni.

Ripoti hiyo inaongeza kuwa mataifa ya Arabuni sharti yazidishe ushindani wa kibiashara ili yaweze kuendelea kuwapo katika uchumi wa ulimwengu katika sekta nyingine mbali na nishati.

Masuala ya Mazingira yanatarajiwa kuzungumziwa na wshiriki kwani mataifa mengi katika eneo hilo yanakabiliwa na uhaba wa nishati huku machache tu yakijihusisha na hatua za kupata nishati inayoweza kutumika tena na tena.

Washiriki maarufu akiwemo Malkia Rania wa Jordan,Waziri Mkuu wa Emarati Sheikh Mohammed bin Rashid al Maktoum vilevile balozi wa zamani wa Saudia nchini Marekani Prince Turki al Faisal wanatarajiwa kuhutubia kikao hicho.

Wageni wengine mashuhuri ni Rais wa Afghanistan Hamid Karzai,Waziri Mkuu wa Pakistan Shawkat Aziz pamoja na Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza John Reid.