Kunatokota Syria, jee itaangukia katika vita vya kienyeji? | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.08.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Kunatokota Syria, jee itaangukia katika vita vya kienyeji?

Mbinyo wa kimataifa kwa utawala wa Rais Bashar al-Assad wa Syria unazidi kuwa mkubwa. Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia ametoa mwito wa kufanywa marekebisho ya kisiasa ya haraka na makubwa katika nchi hiyo.

default

Rais Bashar al-Assad akitoa hotuba mjini Damascus akiwalaumu watu wanaofanya njama dhidi ya utawala wake

Baada ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, Baba Mtakatifu Benedikt wa kumi na sita na wanasiasa wengine mashuhuri, sasa pia Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia ametoa mwito wa kufanywa marekebisho ya kisiasa ya haraka na makubwa katika nchi hiyo. Hata hivyo, Rais al-Assad anawachia vifaru vyake vya kijeshi vifanye kazi. Watu tisini mwishoni mwa wiki wameuwawa kutokana na  operesheni za kikatili zilizofanywa na utawala wa  Syria.
König und Premierminister von Saudi-Arabien Abdullah ibn Abd al-Aziz Al Saʿud im Juni 2010

Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia anambinya Rais al-Assad wa Syria afanye marekebisho

Rais al-Assad anatumia vifaru vya kijeshi dhidi ya watu wake mwenyewe. Mwisho wa  wiki iliopita, Syria haijajionea mwisho wa matumizi ya nguvu. Umoja wa Nchi za Kiarabu, Arab League, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Baba Mtakatifu Papa Benedikt wa kumi na sita- wote hao wametoa mwito kwa Rais Bashar al-Assad wa Syria akomeshe vitendo vya utumiaji nguvu dhidi ya wananchi wake. Hadi sasa miito hiyo haijafua dafu. Kesho waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki anakwenda Damascus.  Katika miaka iliopita Uturuki imekuwa na uhusiano mzuri na  Syria. Lakini sasa Waturuki wameishiwa na subira kwa utawala wa nchi hiyo. Hayo yalisemwa na waziri mkuu wa Uturuki, Tayyip Erdogan, mwishoni mwa wiki. Mpaka sasa hakuna kilichosaidia, lakini kuungwa mkono wananchi wa Libya ni muhimu, anasema mwanaharakati wa haki za binadamu wa Syria, Musab Azzawi:

"  Uungaji mkono wowote ambao utapewa watu wa Syria ambao wanapigania uhuru na heshima unakaribishwa na a utawapa nguvu. Lakini, kimsingi, wananchi wa Syria wameamuwa peke yao kuifuata njia yao ya kutumia nguvu na kupambana na utawala."

Maeneo yenye upinzani mkubwa huko Syria yamevamiwa na vifaru na majeshi ya usalama. Hama, mji ulioko  katikati ya nchi, tangu siku tisa sasa umezingirwa. Mashahidi pia  wanasema kwamba katika miji ya Homs, Deraa na katika viunga  vya  Damascus kumefanywa maandamano na kuna watu waliokufa. Haijawezekana kuzihakikisha habari hizo. Waandishi wa habari wa kigeni wanakatazwa kuingia Syria. Tangu jana  vifaru 25 vya kijeshi  na wanajeshi wamekuwa wakiushambulia mji wa Deir al-Zur, mashariki ya nchi hiyo. Hayo yamesemwa na  mwanaharakati wa kupigania haki za binadamu, Musab Azzawi, ambaye kwa mujibu yake yeye ana mawasiliano ya simu na wananchi wa mji huo:

" Serikali ina hofu kwamba watapoteza kuidhibiti miji. Kuna upinzani mkubwa. Utawala umejaribu kuwakamata baadhi ya machifu wa makabila ambao wanauunga mkono upinzani."

Serikali ya Syria kwa masiku sasa imekuwa ikizungumzia juu ya magengi yalio na silaha ambayo yamekuwa yakiwatisha wakaazi wa miji kadhaa, na imewataka wananchi wawe watulivu. Serikali imetaja kwamba utulivu utarejeshwa. Pia serikali imeonesha picha za mazishi ya wanajeshi ambao kwa mujibu wa serikali wamekufa katika mapambano kama mashahidi. Jambo hilo halijaweza kuhakikishwa pia.

Serikali ya Syria imetangaza kwamba kutakuweko uchaguzi wa bunge mwishoni mwa mwaka huu, na imeipunguza makali sheria juu ya vyama vya kisiasa. lakini upinzani unasema yote hayo ni danganya toto. Katiba ya Syria inahakikisha kwamba chama tawala cha Baath kina wingi mkubwa bungeni, bila ya kujali matokeo ya uchaguzi. Pia  nyadhifa muhimu za juu katika serikali na utawala zitakamatwa na wanachama wa chama hicho.

Hali ya mambo ni ya mkwamo. Kuna hofu kwamba Syria inateleza kuangukia katika vita vya kienyeji. Emad ad-din Rashid, mmoja kati ya wapinzani wa serikali, haamini tena kwamba kupitia serikali hii ya sasa kuna kitu chochote kingine kinachoweza kufanyika. Anasema serikali imepoteza uhalali wake, imeonesha kwamba inaweza kuuwa  watoto na vijana wanaoandamana. Alisema uchunguzi wao, na kutokana na idadi ya watu waliokamatwa, umeonesha wazi kwamba serikali imehusika na vifo hivyo, imetoa amri au imefumbia macho.. Kwa vile serikali hiyo imeyapa majeshi ya usalama silaha kufanya hayo,  hivyo, serikali hiyo haina uhalali wa kuweko.

Mwandishi: Wiening, Jens/ Othman, Miraji/ZR

Mhariri. Mohammed Abdulrahman

 • Tarehe 08.08.2011
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/12Ctj
 • Tarehe 08.08.2011
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/12Ctj

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com