1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kumbukumbu ya mauaji ya Marikana yafanyika

Josephat Nyiro Charo16 Agosti 2013

Leo (16.08.2013) kumefanyika kumbukumbu ya mauaji ya wafanyakazi 34 wa mgodi wa Marikana wa kampuni ya Lonmin yaliyofanyika mwaka jana nchini Afrika Kusini.

https://p.dw.com/p/19QxL
08.2013 GDMA Sonderpreis des Publikums: Marikana bloodshed
08.2013 GDMA Sonderpreis des Publikums: Marikana bloodshed

Maelfu ya wafanyakazi na jamaa wa wachimba migodi hao waliopigwa risasi na polisi wakati wa mgomo wao wakidai nyongeza ya mshahara, wamekusanyika kwa kumbukumbu ya kwanza ya mauaji hayo, karibu na mgodi wa Marikana ambako Agosti 16 mwaka uliopita polisi waliwamiminia risasi 284 wafanyakazi waliokuwa wakifanya mgomo, hatua ambayo iliitumbukiza Afrika Kusini kwenye mzozo mkubwa na kuushtusha ulimwengu.

Kwa mujibu wa waandaaji wa kumbukumbu hiyo, viongozi wa kidini wamefanya maombi maalumu na majina ya wafanyakazi wote waliouwawa yamesomwa. Kumetolewa pia maelezo ya kina kuhusu jinsi mauaji hayo ya kiholela yalivyofanyika. Watu wamenyamaa kimya wakati unaokaribia ule ambao polisi waliwafyetulia risasi wafanyakazi hao.

epa03692947 Jacob Zuma, President of South Africa attends the opening plenary session titled 'Building with BRICS' at the World Economic Forum on Africa 2013 in the Cape Town International Convention Centre, South Africa 09 May 2013. Under the theme _Delivering on Africa_s Promise_, the 23rd World Economic Forum on Africa is a platform for regional and global leaders from business, government and civil society to deepen the continent_s integration agenda and renew commitment to a sustainable path of growth and development. EPA/NIC BOTHMA
Rais wa Afrika Kusini, Jacob ZumaPicha: picture-alliance/dpa

Siku mbili kabla kumbukumbu ya leo, rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, alitoa taarifa kuwahimiza watu kuhusu amani, maombi na kutafakari yaliyotokea katika mgodi wa Marikana. Hapo jana kamishna wa kitaifa wa jeshi la polisi, Riah Phiyega, alitoa mwito kuwepo na utulivu katika kumbukumbu za leo. "Cha muhimu zaidi tunaomba watu wasibebe silaha za hatari kama vile visu, marungu, bunduki au silaha nyingine hatari," alisema kamishna huyo. Wafanyakazi walianza kukusanyika jana mchana, baadhi wakiandamana katika makundi madogo madogo wakiwa na matawi na vijiti, wakiimba nyimbo na huku wengine wakikaa kimya kwenye vilima vilivyo karibu na mgodi huo mkubwa duniani wa madini ya platinum huo Marikana.

Chama cha ANC chasusia kumbukumbu

Wakati huo huo, chama tawala nchini Afrika Kusini, ANC, na serikali imesema haotojihusisha na kumbukumbu hiyo ikisema haiwatambui waandaaji, kundi lenye mafungamano na chama cha wafanyakazi chenye msimamo mkali. Uamuzi huo umedhihirisha bayana mipasuko na mivutano kuhusiana na mauaji ya kiholela ya Marikana, ambayo yameelezwa kuwa mabaya kabisa kuwahi kutokea tangu kumalizika utawala wa ubaguzi wa rangi mwaka 1994. Hakuna afisa yeyote wa serikali atakayetoa hotuba mahala hapo kwa mujibu wa ratiba iliyoonekana na shirika la habari la AFP.

Akieleza juu ya uamuzi huo, msemaji wa chama cha ANC, Ishmael Mnisi, amelishutumu kundi linalojumuisha chama cha wafanyakazi cha AMCU, kinachopingana na chama tawala kwa kuiteka nyara kumbukumbu hiyo ya leo katika mgodi wa Marikana. Akizungumza na na shirika la habari la Reuters, Mnisi amesema watu wanataka kulitumia janga la Marikana kwa manufaa yao ya kisiasa. Kundi la Marikana lililoratibu kumbukumbu hiyo pia linajumuisha mchungaji mmoja mashuhuri na wakili anayeziwakilisha familia za wahanga wa mauaji ya Marikana.

Uchunguzi bado haujakamilika

Itakumbukwa kwamba kabla kufanyika mauaji hayo, watu 10, wakiwemo maafisa wawili wa polisi, walikufa wakati kukiwa na mgomo wa kususia kazi kudai mishahara iongezwe. Uchunguzi wa mauaji ya Marikana haujakamilika, huku ukicheleweshwa na kukwamishwa na mivutano kuhusu ukosefu wa udhamini wa kifedha kutoka kwa serikali kama ada ya huduma za kisheria kwa wahanga.

Judge Ian Farlam (2nd R), chairperson of the Marikana commission of inquiry, flanked by members of the commission, observe a minute of silence on October 1, 2012 in Rustenberg during the opening of an inquiry into the police killing of 34 miners and related violence in August 16. The Marikana Commission of Inquiry, appointed by President Jacob Zuma, began what is expected to be four months of deliberations at Rustenburg Civic Centre, just a stone's throw from the mine where police gunned down striking platinum miners. AFP PHOTO (Photo credit should read -/AFP/GettyImages)
Tume ya uchunguzi iliyoteuliwa na rais ZumaPicha: Getty Images

Hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyebebeshwa dhamana kuhusu mauaji ya Marikana. Mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Afrika Kusini, Eusebius McKaiser, amesema hakuna taarifa kamili kuhusu jinsi mauaji hayo yalivyofanyika na tume maalumu ya uchunguzi haitarajiwi kukamilisha kazi yake hivi karibuni. "Kwa mantiki hiyo watu watasubiri sana kujua ni nani anayebeba dhamana kisheria kwa mauaji hayo ya wachimba migodi 34," ameongeza kusema McKaiser.

Tume ya serikali ilitarajiwa kukamilisha kazi yake Januari mwaka huu, lakini shughuli ya kusikiliza kesi na ushahidi haijakamilika. Hali hiyo inawafanya watu wengi kujiuliza kama tume hiyo itatoa ripoti yake ya mwisho kabla muda kupita wa kutekeleza kikamilifu mapandekezo ya uchunguzi huo.

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limeonya kwamba uwazi unahitajika katika kutegua kitendawili cha mauaji ya Marikana. "Athari za muda mrefu kwa heshima na ulinzi wa haki za binaadamu nchini Afrika Kusini zitakuwa kali iwapo maafisa wa serikali watashindwa katika uchunguzi wao," amesema Noel Kulutwa, afisa wa shirika hilo.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/RTRE/DPAE

Mhariri: Saumu Yusuf