1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghadhabu yazuka baada ya Bemba kufutiwa kesi

Josephat Charo
15 Juni 2018

Gazeti la Süddeutsche lilikuwa na kichwa cha habari "Ghadhabu kuhusu Hukumu" Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC mjini The Hague yamuachia huru makamu wa rais wa zamani wa Congo, Jean Pierre Bemba.

https://p.dw.com/p/2zcQP
Internationaler Strafgerichtshof Jean-Pierre Bemba
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Kooren

Mhariri wa gazeti la Süddeutsche Zeitung alisema wanaharakati wa kutetea haki za binadamu mwishoni mwa wiki iliyopita waliukosoa uamuzi wa mahakama ya ICC wa kumuondolea mashitaka mwanasiasa huyo wa Congo na kiongozi wa zamani wa waasi, Jean Pierre Bemba. Gazeti lilimnukuu msemaji wa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International akisema hatua ya mahakama hiyo ni fedheha; ni kama kofi katika nyuso za wahanga. Naye Fiona McKay wa shirika la haki za binadamu la Open Society alinukuliwa akisema hatua hiyo ni pigo kubwa kwa mahakama ya ICC, ambayo kwa miaka kumi imetumia raslimali nyingi kushughulikia kesi ya Bemba. Bemba alihukumiwa kifungo cha miaka 18 jela katikati ya mwaka 2016 katika kesi ya kihistoria ambapo mbabe wa kivita aliwajibishwa kwa uhalifu ambao aliamuru au alioweza kuuzuia.

Nalo gazeti la Tageszeitung likizingatia pia hukumu hiyo, lilisema mbabe wa zamani wa kivita wa Congo, Jean Pierre Bemba, ameibua hisia mseto nchini mwake na miongoni mwa wanasheria katika ngazi ya kimataifa.

Mhariri anasema wafuasi wa Bemba nchini Congo wanamuona kama rais mtarajiwa. Haijawa wazi ikiwa Bemba atalazimika kukaa The Hague mwaka mwingine mmoja kwa kutiwa hatiani katika kesi nyingine ya kuwashawishi wapigaji kura, kwani tayari amekaa katika mahakama hiyo kwa miaka kumi.

Mwanaharakati wa Congo afariki kwenye ajali ya moto

"Luc Nkulula ameaga dunia, vijana wa Congo wamepigwa na butwaa" - ndivyo lilivyoandika gazeti la Tageszeitung. Luc alikuwa miongoni mwa waasisi wa kundi la vijana wanaopigania mageuzi la La Lucha, ambaye alifariki usiku wa kuamkia siku ya Jumapili katika mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, Goma.

Nyumba katika kitongoji cha Himbi cha mji wa Goma, ambamo alikuwa akiishi na dada yake, ilichomeka moto kabisa, kama picha na video zilivyoonesha. Kitanda chake kiligeuzwa kuwa majivu. Majirani wameelezea katika ripoti ya televisheni kwamba Nkulula alijaribu kujinusuru. Dadake alikuwa ameenda kujisaidia katika choo kilicho nje ya nyumba, akamuasha kwa mayowe alipouona moto mkubwa ukiwaka. Alijaribu kulifungua dirisha, lakini lilikuwa limekwama, kisha paa la nyumba hiyo lililokuwa likiwaka moto likamuangikia. Wakati wazima moto wa tume ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa nchini Congo, MONUSCO, walipofika, waliweza tu kuiopoa maiti ya kijana huyo aliyekuwa na umri wa miaka 33.

Zuma apania kurejea katika siasa

Gazeti la Tagesspiegel liliripoti kuhusu rais wa zamani wa Afrika kusini, Jacob Zuma, kwamba kapata pigo, lakini hajafika mwisho. Mhariri wa gazeti hilo alisema Zuma anapania kurejea katika ulingo wa siasa na amewaonya wapinzani wake wa kisiasa.

Südafrika Prozess gegen Jacob Zuma in Durban
Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob ZumaPicha: Reuters/N. Bothma

Zuma alinukuliwa akisema Ijumaa iliyopita kabla kwenda mahakamani kwa kesi ya rushwa inayomkabili kwamba hana majukumu tena na ndio maana anaonya watu watulie na washughulikie barabara mambo yao. Tetesi zimehanikiza kwamba Zuma, aliyetimuliwa madarakani, anapanga kurejea katika siasa, kauli mbiu yake isiyo rasmi ikiwa ni - "Usinichokoze!"

Mageuzi yaendelea kushamiri Ethiopia

Gazeti la Frankurfuter Allgemeine liliandika - "Wakuu wa majeshi walegeza msimamo". Waziri Mkuu wa Ethiopia amewaachia huru wafungwa wa kisiasa na kutoa ishara ya mageuzi kwa mataifa ya nje. Wapinzani wanashangaa, lakini wanabaki kutomuamini na kumkosoa.

Waziri mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, mwenye umri wa miaka 41 amejinasibu kama kiongozi wa kiafrika mwenye umri mdogo anayebeba matumaini katika mojawapo ya maeneo masikini kabisa duniani. Tangu wiki kadhaa habari njema zimekuwa zikijitokeza Ethiopia na ni nadra siku kupita bila kusikia hatua mpya zinazochukuliwa na serikali. Maelfu ya wafungwa wa kisiasa wameachiwa huru, akiwemo kiongozi wa upinzani, Andargachew Tsige, aliyehukumiwa kifo mnamo mwaka 2009 kwa kuasisi kundi la kigaidi la Ginbot 7. Katika jimbo la Oromia pekee jumla ya wafungwa 40,000 wameachiwa huru katika miezi michache iliyopita.

Wahamiaji wabaki Israel

"Mjadala wa kuwajumuisha wageni nchini Israel. Wawakilishi wa kibiasahra wanapinga kuwarejesha makwao wakimbizi wa kiafrika kutoka Israel" - hivyo ndivyo lilivyoandika gazeti la Neues Deutschland. Mhariri wa gazeti hilo la Neues Deutschland alisema serikali ya Israel imejaribu kwa kuwarejesha nyumbani wakimbizi 40,000 wa kiafrika wanaotokea Sudan, Sudan Kusini na Eritrea, lakini haijafanikiwa. 14,000 kati yao wanaishi mjini Tel Aviv. Huku serikali ya waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ikijadiliana na nchi za Ulaya juu ya kuwachukua wakimbizi hao, kundi la wafanyabiashara 64 sasa linapinga likisema gharama za kuwajumuisha katika jamii ni ndogo kuliko kuwarudisha makwao na kutainufaisha Israel.

Mwandishi: Josephat Charo/Pressedantenbank

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman