1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kosovo yakabiliwa na mtihani mkubwa

Charo, Josephat16 Machi 2008

Serbia yataka sehemu ya kaskazini ya Kosovo iwe miliki yake

https://p.dw.com/p/DPLn
Waziri mkuu wa Serbia Hashim ThaciPicha: AP

´Karibu katika jamhuri ya Kosovo´. Hayo ni maneno yalioandikwa katika bango kubwa lililozinduliwa juma lililopita na waziri mkuu wa Kosovo, Hashim Thaci, katika kivuko cha Merdare kati ya jahmhuri hiyo mpya na Serbia. Bango hilo ni ishara ya mpaka kati taifa hilo jipya la Kosovo, ambalo linautenganisha wakati uliopita na siku zijazo za usoni.

Waziri mkuu wa Kosovo, Hashim Thaci, akiwa amesimama kando ya bango hilo lenye maandishi kwa lugha ya kiingereza, kiserbia na kialbania, amesema kutambuliwa kwa mpaka huo na nchi jirani ya Serbia kutakuwa muhimu kwa kutambuliwa hali ya baadaye ya Kosovo kuelekea Umoja wa Ulaya. Lakini Waserbia 100,000 wanaoishi kaskaszini mwa Kosovo hawataki kuwa sehemu ya ukweli halisi wa kisiasa wa hivi sasa, na katika msimamo wao huo wanaungwa mkono na Serbia.

Jimbo la Kosovo lilikuwa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa tangu mwaka wa 1999. Halmashauri mpya ya Umoja wa Ulaya iliyoundwa ya EUROLEX inatarajiwa kuchukua uongozi katika siku 120 tangu Kosovo kujitangazia uhuru wake kutoka kwa Serbia mnamo tarehe 18 mwezi uliopita.

Kiongozi wa kamati ya kimataifa ya Helsinki ya kutetea haki za binadamu, Sonja Biserko, amesema serikali ya Serbia imejaribu kwa kila njia kuchochea machafuko Kosovo na kuanzisha mgawanyiko, huku ikitaka eneo la kaskazini liwe sehemu ya Serbia.

´Mipango hii haikutangazwa kwa umma lakini tunaweza kuziona hatua hizo kila kuchao,´ ameongeza kusema kiongozi huyo wa kamati ya kupigania haki za binadamu. ´Serikali ya Serbia inavuka mpaka na jumuiya ya kimataifa haitauvumilia.´

Mamia ya Waserbia waliivamia mahakama ya Umoja wa Mataifa katika mji wa kaskazini wa Mitrovica Ijumaa wiki iliyopita wakidai kurudi kwa mfumo wa sheria za Serbia katika sehemu hiyo ya jamhuri mpya ya Kosovo. Wengi wamejiuzulu kutoka kwa polisi ya Kosovo iliyo na maafisa kutoka jamii mbalimbali. Siku kadhaa baada ya Kosovo kujitangazia uhuru kutoka kwa Seria, Waserbia walikichoma moto kivuko cha mpakani cha Jarinje wakipinga huduma za kodi na polisi zilizoanzishwa hapo na utawala wa Kosovo.

Mapema juma lililopita shirika la reli la Serbia liliifungua sehemu ya reli kutoka Kosovo kaskazini kwenda katikati mwa Serbia licha ya onyo kutolewa na utawala wa Umoja wa Mataifa kwamba hatua hiyo haikuwa halali. Kiongozi wa kanisa la Orthodox nchini Serbia, askofu mkuu Artemije, ametoa mwito tume za kimataifa nchini Kosovo zigomewe, hususan halmashauri mpya ya Umoja wa Ulaya, EULEX, ambayo ameieleza kuwa kikosi cha kuikalia Kosovo.

Serbia inapanga kufanya uchaguzi wa bunge na wa serikali za mitaa miongoni mwa Waserbia wanaoishi nchini Kosovo, mnamo tarehe 11 mwezi Mei mwaka huu wakati zoezi hilo litakapokuwa likiendelea nchini Serbia.

Dusan Janjic wa jukwaala mahusiano ya kimbari ameliambia shirika la habari la IPS kwamba kinachoelendelea hivi sasa ni kuundwa kwa taasisi zilizo sambamba. Waserbia na Walabania nchini Kosovo wana historia ya kuishi sambamba lakini mamlaka yakaenda kwa taifa lililonyang´anya madaraka.

Janjic alikuwa akizungumzia maisha tofauti baina ya Waserbia na Waalbania nchini Kosovo katika miaka ya 1990 wakati Serbia chini ya utawala wa rais Slobodan Milosevic ilipoanzisha utawala wa moja kwa moja katika jimbo hilo. Waserbia walitawala wakati huo, na Waalbania wakachukua taasisi kama vile kuanzisha shule za lugha yao katika makazi yao binafsi. Huduma msingi za afya zilitolewa na watalaamu wa afya waliofutwa kazi na maafisa wa Serbia. Uchaguzi ulifanywa kuchagua bunge na rais aliyekuwa tayari ameteuliwa.

Katika kipindi kifupi, kinachojitokeza ni mtihani mkubwa ikiwa maisha sambamba yanayosisitizwa hivi sasa na Serbia yataonekana katika taasisi. Hatimaye huenda yakashindwa na kusababisha hasara kubwa kwa Waserbia wa Kosovo. Haya yatakuwa marudio ya falsafa angamizi iliyowagharimu sana Waserbia.

Janjic alikuwa akizungumzia hatua ya rais Slobodan Milosevic kuyaunga mkono mapinduzi ya Waserbia dhidi ya uhuru wa Croatia kati ya mwaka wa 1991 na 1995. Waserbia wa Croatia walianzisha taifa la Krajina katika eneo lililokaliwa na idadi kubwa ya Waserbia la Croatia na kuwa na rais wao, bunge na mifumo tofauti ya sheria na elimu iliyofanana na mifumo ya Serbia kwenyewe.

Jamhuri iliyojitangaza yenyewe ya Krajina ilikoma kuwepo baada ya harakati ya jeshi la Croatia ya mwezi Agosti mwaka wa 1995. Zaidi ya Waserbia laki mbili walilikimbia eneo hilo na kurejea nchini Serbia. Idadi ndogo ya Waserbia wamerudi Krajina tangu wakati huo.

Janjic amesema watu wale wale waliounda mipango ya miaka ya 1990 ndio hao hao waliounda mpango wa hivi karibuni wa Kosovo.

Serikali ya Serbia mjini Belgrade imepinga matamshi ya kiongozi wa halmashauri mpya ya Umoja wa Ulaya, EULEX, Pieter Feith, kwamba hakutakuwa na jimbo wala uhuru wa kaskazini mwa Kosovo.

Miito ya tume ya Umoja wa Matiafa nchini Kosovo, UNMIK, kuitaka Serbia iheshimu azimio la Umoja wa Mataifa nambari 1224 na iache kuwaingilia Waserbia wa Kosovo haijatiliwa maanani. ´Azimio hilo la Umoja wa Mataifa bado linafanya kazi, na pande zote husika, ikiwemo Serbia, zinatakiwa ziliheshimu,´ amesema msemaji wa UNMIK, Alexander Ivanko, katika mji mkuu wa Kosovo, Pristina wiki iliyopita.