1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kosovo na matatizo ya kikabila

P.Martin10 Machi 2008

Mnamo Machi 17 mwaka 2004 uvumi ulioenea katika mji wa Mitrovica kuwa watoto wa Kialbania walifurushwa na Waserb hadi kwenye Mto Ibar ulichochea umwagaji mkubwa wa damu dhidi ya Waserb.

https://p.dw.com/p/DMGt
Kosovars celebrate international recognition in Pristina, Kosovo, Monday, Feb. 18, 2008. Major European powers and the U.S. recognized Kosovo on Monday, a day after the province's ethnic Albanian leaders declared independence from Serbia. Giddy Kosovars danced in the streets when they heard of the endorsements. (AP Photo/Visar Kryeziu)
Wakosovo wakisherehekea kutambuliwa kwa tangazo la uhuru wake kutoka SerbiaPicha: AP

Shirika moja la Kitaliana linaloendeleza midahalo kati ya makabila mbali mbali mjini Mitrovica-(Italian Association for Peace)hujaribu kuwaelimisha vijana kuachana na mawazo yaliyotia mizizi na kusababisha mtengano wa kikabila.Watoto wa Kiserbia na Kialbania wanafundishwa historia tofauti.Vile vile kumependekezwa kuanzisha chuo kikuu kitakachowaleta pamoja vijana wa Kialbania na Kiserb katika mji wa Mitrovica.Chuo hicho pia kitatoa nafasi mpya za ajira.Mji huo tayari una chuo kikuu cha Waserbia kilichohamishwa kutoka mji wa Pristina ulio na wakaazi wengi wenye asili ya Kialbania.

Kwa upande mwingine,kuna hofu mpya kuwa hatua iliyochukuliwa na Kosovo hivi karibuni kujitangazia uhuru wake kutoka Serbia,itaathiri vibaya juhudi za kupunguza mwanya kati ya makabila hayo mawili.Katika siku zilizopita,serikali ya Yugoslavia ya zamani ilikuwa na siasa iliyohakikisha mchanganyiko wa makabila mitaani na wakaazi wengi katika mji wa Mitrovica walizungumza lugha zote mbili- yaani Kiserbia na Kialbania.Lakini siku hizi ni hatari kufanya kosa la kuzungumza na mtu kwa lugha ambayo si yake.

Tangu muda mrefu wataalamu wa kimataifa wametoa mwito wa kuchukua hatua za kufufua mazingira yenye mchanganyiko wa kikabila na vile vile kupiga jeki uchumi wa mji huo,lakini hakuna maendeleo makubwa yaliyopatikana.Matatizo ya kiuchumi ni miongoni mwa mambo yanayowazuia wakimbizi wa makabila mbali mbali kurejea Mitrovica na kuishi kama jamii moja.

Hakuna eneo lililoathirika vibaya zaidi kuliko mji wa Mitrovica tangu kusambaratika kwa viwanda vya serikali ya kisoshalisti.Chini ya serikali ya Yugoslavia ya zamani,kiasi ya watu 23,000 walikuwa wakifanya kazi katika migodi ya Trepca iliyokuwa na umuhimu mkubwa katika Kosovo.Migodi hiyo ilifungwa na NATO kwa sababu zilizohusika na mazingira.Sasa ni wawekezaji wachache waliojaribu kufufua sekta ya migodi.Vile vile inatuhumiwa kuwa viwanda vingi hutumiwa kwa ajili ya kuwekeza pesa zilizopatikana kwa njia zisizo halali,baada ya utaratibu wa kubinafsisha,uliotiliwa mashaka,kukosa kutoa nafasi mpya za ajira.

Hata hivyo,wapo wanaoamini kuwa uhuru wa Kosovo utaleta uwazi katika taasisi mbali mbali na wawekezaji watarejea katika kanda hiyo.Vile vile hali mpya ya Kosovo huenda ikasaidia kuimarisha uchumi na kwa njia hiyo kuwaleta pamoja watu wa makabila mbali mbali.