1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea ya kusini yasisitiza mazungumzo zaidi na Korea ya kaskazini

Sekione Kitojo29 Desemba 2010

Rais wa Korea ya kusini atoa wito wa majadiliano zaidi katika kuuvunja mpango wa kinuklia wa Korea ya kaskazini

https://p.dw.com/p/zr9q
Rais wa Korea ya kusini Lee Myung-bak.Picha: AP

Rais wa Korea ya kusini, Lee Myung Bak, ametoa wito leo kuvunjwa mpango wa kinyuklia wa Korea ya kaskazini mwaka ujao kupitia mazungumzo yanayofanywa na mataifa sita.

Hatua hiyo inaweza kuwa ishara ya kubadilika kwa msimamo wa Korea ya kusini kuelekea mazungumzo zaidi , ambayo pia yanahusisha Marekani, Japan , China na Urusi na ambayo yamekwama tangu mwaka 2008.

Hatuna njia nyingine isipokuwa kutatua mzozo huu wa kuvunja mpango wa kinyuklia wa Korea ya kaskazini kwa mazungumzo, amenukuliwa Lee na shirika la habari la nchi hiyo la Yonhap akisema .

Lee amesema kuwa kuna hali ya dharura mkubwa kwa sababu Korea ya kaskazini imepanga mwaka 2012 kufanya maadhimisho ya miaka 100 tangu kuzaliwa kwa muasisi wa taifa hilo, Kim Il Sung , na kuwa utakuwa mwaka nchi hiyo itakapokuwa na nguvu kubwa pamoja na ustawi.

Wakati rais huyo wa Korea ya kusini akihimiza majadiliano , lakini wadadisi wanasema kuwa nafasi ya mazungumzo ya jumuiya ya kimataifa ni finyu sana kwa sababu ya mgawanyiko mkubwa pamoja na kukosekana kwa mbinyo dhidi ya Korea ya kaskazini.

Lee Myung-bak, ambaye aliapa kuchukua hatua kali dhidi ya shambulio lolote jingine litakalofanywa na Korea ya kaskazini , pia ametoa wito leo wa kufanyika mazungumzo mapya kati ya Korea hizo mbili, akisema sera za msimamo mkali za kijeshi zinazochukuliwa na nchi yake hazitapunguza hali ya wasi wasi.

Mazungumzo ya pande sita yenye lengo la kuvunja mpango wa kinyuklia wa Korea ya kaskazini , ambapo Korea ya kaskazini ilijitoa katika mazungumzo hayo miaka miwili iliyopita, lilikuwa ni jukwaa pekee la kumaliza mpango huo na nchi hiyo ipatiwe msaada pamoja na kutambuliwa kidiplomasia, Lee amesema wakati wa kutoa mtazamo wake wa masuala ya nje katika wizara ya mambo ya kigeni.

Taarifa hiyo ilionekana zaidi kuwa inafungua njia ya kuanza tena majadiliano na kupingana na kauli iliyotolewa na afisa mmoja wa serikali ambaye hakutajwa jina na shirika hilo la habari la Yonhap wiki iliyopita , ambaye amesema kuwa mazungumzo zaidi hayatawezekana hadi pale Korea ya kaskazini itakapojiunga na mkataba wa kutosambaa silaha za kinyuklia, ambapo ilijitoa katika mkataba huo mwaka 2003.

Mwandishi : Sekione Kitojo / DPAE/RTRE

Mhariri : Othman Miraj