1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yajiandaa kutuma roketi angani

Admin.WagnerD9 Aprili 2012

Korea Kaskazini inajianda kusherehekea miaka 100 tangu kuzaliwa kwa muasisi wa taifa hilo Kim ill Sung kwa kutuma roketi angani ambayo inadai itabeba setilaiti ya hali ya hewa.

https://p.dw.com/p/14ZlY
Korea kaskazini ikizindua kombora, katika eneo la Musudan-ri mwaka 2009
Korea kaskazini ikizindua kombora, katika eneo la Musudan-ri mwaka 2009Picha: KRT TV

Lakini Korea Kusini na Marekani wanasema hicho ni kisingizio cha kufanya jaribio la kombora la masafa marefu, ambalo ni ukiukwaji wa azimio la Umoja wa mataifa na makubaliano kati ya Marekani na Korea Kaskazini.

Waandishi washuhudia
Katika hali isiyo ya kawaida, Korea Kaskazini imevialika vyombo vya habari vya kimataifa kushuhudia tukio hilo ili kuushawishi ulimwengu kuwa hatua yake hii ni kwa nia njema tu na wala ni kujaribu kombora la masafa marefu kama invyodaiwa na utawala mjini Seoul.

Afisa mmoja mjini Seoul alisema Korea Kaskazini ilikuwa inapanga kufuatisha uzinduzi huo wa setilaiti unaotarajiwa kati ya tarehe 12 na 16, na jaribio la tatu la kombora la nyuklia.

Lakini Mkuu wa kituo cha angani cha Tongchang-ri nchini Korea Kaskazini, Jang Myong-Jin alisema ni upumbavu kuuita uzinduzi huo wa setilaiti kama kisingizio cha kujaribu kombora la masafa marefu.

Jang Myong-Jin aliwambia waandishi wa habari kuwa uzinduzi huu ulipangwa muda mrefu kama mmoja ya shughuli za kusherehekea miaka 100 ya kuzaliwa kwa muasisi wa taifa hilo, na kuongeza kuwa hawafanyi hivyo kichokozi.

Roketi hii iliyopakwa rangi nyeupe na maandishi ya rangi ya samawati, ina urefu wa mita 30 na upana wa mita mbili na nusu. Wandishi pia waliona kwa karibu box lenye uzito wa kilo mia moja likiwa na antena tano na kufunikwa vipande vya kukinga umeme wa jua, ambalo maafisa walisema ni satelaiti.

Walisema setilaiti hii iliyopewa jina la Kwangmyongsong -3, au nyota inayong'a, itafanya kazi ya kukusanya taarifa za misitu na maliasili katika taifa hili maskini lakini lenye nguvu za nyuklia.

Kipimo cha ushupavu wa Kim Jong Un
Mafanikio ya roketi hii yatamuonesha mtawala mpya wa taifa hilo Kim Jong Un kama kiongozi shupavu.

Mpaka sasa Kim Jong Un amerithi nafasi moja tu, ya kiongozi wa jeshi la watu milioni 1.2 kati ya zote alizokuwa anashikilia baba yake Kim Jong ill, aliyefariki Desemba mwaka jana.

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-Un
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-UnPicha: AP

Chama tawala nchini humo kinatarjia kuitisha mkutano siku ya jumatano ambapo kitamteua Kim Jong Un kuwa Katibu Mkuu wa chama, nafasi nyingine muhimu iliyoishikiliwa na baba yake.

Siku ya Jumapili, ambayo ndiyo kilele cha maadhimisho ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa Kim ill Sung aliyefariki mwaka 1994 na kumuachia madaraka mwanaye Kim Jong ill, mamia ya maelfu wataingia katika mitaa ya Pyongyang kusherehekea kuzaliwa kwake.

Uzinduzi wa roketi hii umeistua pia China, ambayo ni mshirika na mfadhili mkuu wa Korea kaskazini. Japan ilisema siku ya jumamosi kuwa imejianda kuilipua roketi hiyo endapo itatishia usalama wake, na Korea kaskazini pia imetoa kauli kama hiyo.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\AFPE\RTRE
Mhariri: Mohamed Abdul Rahman