1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la klabu bingwa Afrika

14 Septemba 2009

Schalke yaikatisha tamaa Fc Cologne katika Bundesliga

https://p.dw.com/p/JexK
Lukas Podolski wakipambana na SchalkePicha: AP

-Katika Kombe la klabu bingwa barani Afrika,timu 2 za Nigeria -Kano Pillars na Heartland pamoja na moja ya Sudan Al -Hilal zimeingia nusu-finali ya kombe hilo.-Schalke yaichapa FC Cologne mabao 2-1 nyumbani jana na kuparamia ngazi ya 3 ya Ligi nyuma ya Hamburg na Leverkusen.

- Premier League-Ligi ya Uingereza, Manchester City ikitamba na mtogo Adebayor,imeendelea na rekodi yake ya kutoshindwa tangu msimu kuanza.

-Na Chama cha riadha cha Afrika Kusini-Athletics South Africa-kimemtaka mwenyekiti wake kurejea katika Baraza -tawala la shirikisho la riadha Ulimwenguni (IAAF) kufuatia mkasa wa bingwa wa mita 800 Caster semenya aliegunduliwa sehemu mwanamke-sehemu mwanamume.

Ligi mashuhuri barani Ulaya:

Mperu Jefferson Farfan,jana jioni alilifumania lango la FC Cologne dakika ya pili tu ya mchezo na mara baada ya mapumziko, aligawa pasi maridadi kwa Mgeorgia Kobiashvili kwa bao la pili la Schalke lililoiapiza Cologne kuganda mkiani mwa Bundesliga. Ingawa jogoo la FC Cologne, Lukas Podolski lilisawazisha bao la kwanza la Schalke ,hatima yao ilikwishaandikwa jana jioni.Kwa ushindi wa mabao 2:1, Schalke imeparamia ngazi ya tatu ya Ligi nyuma ya Hamburg na Bayer Lebverkusen zenye pointi sawa.

Baadae kocha wa Schalke,alieitawaza mabingwa Wolfsburg, msimu uliopita Felix Magath alisema:

"Nimeridhika kuondoka hapa mshindi ingawa kwa bahati tu"

Wakati Hamburg na Leverkusen zinaongoza Bundesliga kileleni, FC Cologne haikushinda hata mara moja tangu msimu huu kuanza na wana pointi 1 tu kwa kumudu sare nyumbani na Frankfurt. Mapambano 3 yajayo hayatakuwa pia rahisi kwa Cologne:kwani baada ya miadi yake na Stuttgart Jumamosi ijayo,itakua zamu na Bayern Munich ambayo inaanza kusahau misukosuko yake ya mwanzo wa msimu huu kinyume na Cologne.

Munich imechupa hadi nafasi ya 5 ya Ligi baada ya kuirarua Borussia Dortmund kwa mabao 5-1.La kukumbukwa ni bao maridadi la mfaransa Franck Ribery kutoka mkwaju wa free-kick.

Kocha wa Bayern Munich,mholanzi Van Gaal akielezea kwanini Dortmund haikutamba licha ya kutangulia kutia bao la kwanza, alisema:

"Nadhani ustadi bora wa kila mchezaji wetu ndio ulioleta tofauti na ushindi."

Bremen hadi Jumamosi ikiwa nafasi ya tatu ,haikumudu zaidi ya sare 0:0 katika mpambano wake na jirani yake Hannover. Hamburg iliizaba Stuttgart mabao 3-1 wakati Bayer Leverkusen iliwakomea mabingwa Wolfsburg mabao 3-1 na kuwa pointi sawa na Hamburg kileleni mwa Bundesliga.

Ama katika Premier League-Ligi ya Uingereza, Manchester City, imeendelea kutamba msimu huu mpya kwa ushindi wao wa mabao 4-2 dhidi ya Arsenal.Jogoo la Togo lililokuwa likiichezea Arsenal hadi mwisho wa msimu uliopita, Emmanuel Adebayo alizusha mtafaruku uwanjani: Baada ya bao lake alilotia ,alitimka mbio kutoka upande mmoja hadi mwengine wa uwanja kusherehekea bao hilo na la 3 la Manchester City mbele ya mashabiki wa Arsenal.

Chelsea pia iliendelea na ushindi wake msimu huu kwa kuikandika ya Stoke City mabao 2-1.Lilikuwa bao la Florent Malouda dakika ya mwisho ya mchezo lililokamilisha ushindi mwengine kwa Chelsea.Manchester united iko pointi 3 nyuma ya Chelsea baada ya kutoka nyuma na kuitandika Tottenham Hotspur mabao 3-1.Muisraeli Yossi Benayoun alilifumania mara 3-hattrick-lango la Burnley kuchangia ushundi wa mabao 4-0 wa Liverpool na kuiweka timu yake nafasi ya 5 na pointi 6 nyuma ya Chelsea.

Katika la liga, nchini Spain: mabingwa FC Barcelona na mahasimu wao wa jadi Real Madrid kila moja iliondoka na ushindi na kila moja ikiwa na pointi 6 ziko kileleni .valencia imejiunga nazo huko juu.Mreno Cristiano Ronaldo aliingia uwanjani kukomea bao la 3 -0 dhidi ya espanyol.Zlatan Ibrahimovic alitia bao 1 na akamtayarishia pasi maridadi Lioenl Messi kwa bao la pili la Barca katika lango la Getafe.

Katika Serie A, Juventus nayo inaendelea kutamba na hasa baada ya mlinzi wao kutoka Uruguay Martin Caceres akiichezea JUVE mara ya kwanza alitia bao.David Trezeguet akatia bao la pili dhidi ya Lazio Roma.Mkamerun Samuel Eto-o aliipatia Inter Milan bao katika lango la AC Milan na kuipachika Inter pointi 2 nyuma ya viongozi wa Ligi.

Duru nyengine ya Kombe la klabu bingwa barani Afrika ilikuwa uwanjani mwishoni mwa wik na timu 2 za Nigeria, Kano Pillars na Heartland zikijiunga na Al Hilal ya Sudan zimeingia nusu-finali ya kombe hilo kama vile Halima Nyanza anavyosimulia:

Nafasi 1 iliosalia katika kinyanganyiro cha nusu-finali, inaaniwa kati ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na mabingwa wa zamani wa Kombe hili, Etoile du Sahel ya Tunisia mwishoni mwa wiki hii .Pillars ya Nigeria ilitoka nyuma mara mbili na kuiambia Zesco United ya Zambia, "kutangulia -si kufika."

Bao la Bello Korfamata mnamo dakika ya 86 ya mchezo, lilitosha kuhakikisha ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya wazambia.

Heartland pia ya Nigeria ililipiza kisasi kwa TP Mazembe kwa ushindi wa mabao 2:0 huko Owerri,kusini-mashariki mwa Nigeria.Etoile -mabingwa wa Afrika miaka 2 iliopita imejongelea Mazembe hadi pointi 2 kufuatia ushindi wake wa mabao 2:0 dhidi ya Monomotapa ya Zambia.Al Hilal imipiku El Merreikh kwa bao 1:0 alilotia Badr Abdalla.

Mkasa wa bingwa wa dunia wa mbio za mita 800 wanwake wa Afrika kusini Caster Semenya. Taarifa zilizovuja majuzi zinadai uchunguzi aliofanyiwa umegundua yeye sehemu ni mwanamke na sehemu ni mwanamume.

Uchunguzi wa IAAF-shirikisho la riadha ulimwenguni ulipelekea kujiuzulu katika Baraza lake kwa mjumbe wa Afrika kusini, Leonard Chuene.Taarifa kutoka Johannesberg, zinasema "Atheletics South Africa" -chama cha riadha cha Afrika kusini, kimemtaka mwenyekiti wake Leonard Chuene,kurejea kuchukua kiti chake katika baraza hilo la IAAF.

Rais wa IAAF, msenegal Lamine Diack, alimuandikia barua rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, mwezi uiopita akimuomba amtake Chuene asijiuzulu katika Baraza hilo.Chuene akitazamiwa kukutana kesho na waziri wa michezo wa Afrika kusini Makhenkesi, Stofile anaetazamiwa kuidhinisha rasmi uamuzi huo wa kurejea IAAF.

Uhusiano kati ya Afrika kusini na Shirikisho la riadha ulimwenguni uliharabika kutokana na mkasa wa Caster Semenya.Wakati kurejea katika Baraza la IAAF kwa Chuene kunabainisha kuna shabaha ya kupunguza mvutano , waziri wa michezo wa Afrika Kusini, Stofile, ni majuzi tu alipotangaza vita na IAAF

Muandishi: Ramadhan Ali / DPAE

Mhariri:M.Abdul-Rahman