KOMBE LA COSAFA MSUMBIJI LEO UWANJANI | Michezo | DW | 27.04.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

KOMBE LA COSAFA MSUMBIJI LEO UWANJANI

Kinyan'ganyiro cha kombe la castle cup kinazikumbanisha Zimbabwe na Madagascar huku wenye Msumbiji wakiwa na miadi na Ceyschelles.

Katika Bundesliga-Ligi ya Ujerumani ,juhudi za mabingwa Bayern munich kunyakua alao tiketi ya 3 ya champions League-kombe la klabu bingwa barani ulaya msimu ujao kwa kuipiku Stuttgart au Bremen ziliopo nafasi ya pili nay a tatu,zimepatwa na mkosi kati ya wiki hii pale mshambulizi wao mwengine baada ya Schweisteiger, kuumia.

Mara hii, ni chipukizi wao wa miaka 21-Lukas Podolski alieumia goti na yamkini akawa nje ya chaki ya uwanja kwa kipindi cha miezi 6 ijayo.Podolski atahitaji kufanyiwa opresheni na hivyo atakosa mapambano 4 yaliosalia msimu huu ya bundesliga kuichezea Bayern Munich.

Ikiwa Munich itashindwa kumaliza nafasi 3 za kwanza msimu huu, basi itakua mara ya kwanza tangu kupita miaka 11 haitacheza katika kombe la klabu bingwa barani ulaya msimu ujao.

Munich iko nafasi ya 4 katika ngazi ya Bundesliga na pointi 5 kabla ya changamoto za mwishoni mwa wiki hii nyuma ya viongozi wa Ligi Schalke.

Schalke ilifunga jana safari hadi Bochum si masafa marefu kutoka uwsanja wao wa Gelsenkirchen.Schalke ikitamba wakati huu na majogoo wake akina Kuranyi na staid wao wa asili ya Ghana Asamoah na mbrazil Lincoln,ilinadi kwamba haiineiachia Bochum kuitilia kitumbua chake mchanga –mapambano 5 kabla msimu kumalizkka.

Kwani, ushimndi dhidi ya Bochum unaikaribisha Schalke karibu zaidi na taji la ubingwa msimu huu –miaka 49 tangu walipotawazwa mara ya mwisho mabingwa wa Ujerumani hata kabla kuanza kwa Bundesliga,1963.

Bochum lakini ikiwa nafasi ya 11 ya ngazi ya Ligi kabla changamoto hii ,ikitaka kukwepa kuteremshwa daraja ya pili.Kwahivyo, kwa timu zote mbili mpambano wao huo ukawa wa kufa-kupona.

Hatari kubwa lakini kwa Schalke wakati huu inatoka kwa Werder Bremen inayosimama nafasi ya pili ya ngazi ya Ligi na inayokodoa macho kuvaa taji baada ya kupepesuka kati ya wiki hii katika nusu-finali ya kombe la Ulaya la UEFA ilipozabwa juzi mabao 3:0 na Espanyol ya Spain.

Bremen ina miadi na Armenia Bielefeld hapo kesho na taarifa kuwa stadi wao anaevuma Miroslav klose huenda akawaacha mkono na kujiunga na Bayern Munich msimu ujao huenda ikagubika kivuli katika mpambano wao wa kesho.

Changamoto nyengine za Bundesliga jumamosi hii ni kama hivi:

Alemaania Aaachen inacheza na Hertha Berlin.Berlin ilitumai kumuajiri kipa wa taifa Lehmann msimu ujao, lakini Lehmann amerefusha kwa mwaka mmoja mkataba wake na Arsenal London.Mainz 05 yakumbana na Hannover 96.

Borussia Dortmund ina miadi na Eintracht Frankfurt.Nuremberg, inaumana na Wolfsburg.Energie Cottbus itakamilisha duru hii jumapili ikiita nyumbani Bayer Leverkusen.

Katika changamoto za kombe la klabu bingwa barani ulaya kati ya wiki, Manchester United iliitimua shukurani kwa bao la dakika za kufidia la Wayne Rooney, AC Milan ya Itali.

Ushindi wa mabao 3:2 wa MANU unaifungulia mlango nusu wa kucheza tena finali ya kombe la klabu bingwa ama na Chelsea ilioilaza Liverpool kwa bao 1:0 juzi katika nusu-finali nyengine au na Liverpool endapo itaugeuza mkuki kwa Chelsea duru ijayo.

Milan lakini, imewaonya Manchester kuwa wachunge –nyumbani watyakuwa hatari zaidi kuliko walivyokuwa Manchester.

Katika kombe la pili la Ulaya-lile la UEFA ishara zote zaonesha itakua finali ya timu pekee za Spain.

Kwani, katika nusu-finali ya kwanza ,Osasuna imeilaza mabingwa Sevilla bao 1:0 na moja kati ya timu hizo 2 itacheza finali.Katika mpambano wapili, vishindo vya Bremen kuzima zahama za Espanyol nyumbani huko Spain, hazikufua dafu.

Bremen ilizabwa mabao 3:0 na sasa inanin’giniza matumaini ya mwisho katika duru ijayo nyumbani kufuta madhambi hayo ya mabao 3.

Kocha wa Bremen asema:

“Sina kipya cha kusema.Tunajishughulisha tu sasa na mpambano huo ujao na ndio kwetu muhimu kabisa.”

Jürgen klinsmann aliekua kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani katika kombe lililopita la dunia mwaka jana,anarejea katika medani ya dimba nchini Ujerumani.

Lakini, sio kama kocha ,bali kama mchambuzi wa dimba katika TVKlinsmann ambae haondoi uwezekano wa kuwa kocha tena, ana umri wa miaka 42 na anazungumza kingereza kama maji,lakini pia kitaliana na kifaransa akiwa amezichezea ligi za nchi hizo 3.Klinsmann aliarifu kwamba, amepitisha miezi 10 iliopita akijifunza kispanish na mbinu mpya za kufunza dimba.

Chini ya usukani wake, Ujerumani ilimaliza nafasi ya 3 nyuma ya mabingwa wa dunia Itali na makamo-bingwa Ufaransa katika Kombe la dunia.

DIMBA BARANI AFRIKA:

Tukigeukia dimba barani Afrika-Super eagles au timu ya Taifa ya Nigeria itajinoa makali mjini Nairobi,Kenya kabla kujitosa uwanjani Juni 2 kwa changamoto na Ugandan Cranes mjini Kampala.

Berti Vogts –aliekua kocha wa timu ya Taifa ya Ujerumani,aliwaambia maripota kati ya wiki, kuwa anapanga changamoto ama na Kenya au Tanzania kujinoa kabla kuwasili Kampala.

Berti Vogts akasema kuwa Nigeria itakaa Kenya hadi siku 4 kujiandaa .Vogts akitazamiwa kutangaza listi yake ikiegemea zaidi mastadi wa Nigeria wanaocheza huku Ulaya.Nigeria iliilaza Uganda bao 1:0 tu pakle timu hizo 2 zilipokumbana huko Lagos.

Uganda iko nafasi ya pili ya kundi lao ikiwa na pointi 4 kwa 9 za Nigeria.Timu nyengine katika kundi hili la 3 ni Lesotho na Niger.Ni mshindi tu wa kundi hili ndie ataketoroka na tiketi ya kwenda Ghana mwakani kwa Kombe la Afrika hapo Januari.

Wenyeji wa Nigeria –Kenya Harambee Stars nao wametangaza watajinoa na mahasimu wa Nigeria-Uganda. Hii ni sehemu ya maandalio yao kwa kombe la Afrika .Harambee Stars wenye miadi na Swaziland mjini Mbabane Juni 2,wataonana na Ugandan Cranes, mjini Nairobi Mei 20.Wanigeria wanatazamiwa kuwasili nairobi Mei 25.

KOMBE LA COSAFA :CASTLE CUP:

Mabingwa mara 3 wa kombe hilo Zimbabwe wanakabiliwa leo na uwezekano wa kuaga kombe hili wakiwa uwanjani na Madagascar huko Msumbiji.Kwani, Zimbabwe walishindwa kuwaita wachezaji wake kadhaa maarufu wanaocheza n’gambo.

Kwahivyo, kabla kuingia uwanjani leo ,Zimbabwe ilibidi kutegemea chipukizi wake wengi wa timu yake ya chini ya umri wa miaka 23.Zimbabwe ilitwaa mara ya mwisho kombe la COSAFA 2005 na nusu-finali ya leo na Madagascar ingeikatia tiketi kwa finali nyengine.

Wenyeji Msumbiji, wana miadi na visiwa vya Ceyschelles huko Machava Stadium.Mabingwa watetezi wa hivi sasa Zambia, wameingia moja kwa moja katika timu 4 za mwisho.Kombe la COSAFA linajumuisha timu 13 za kusini mwa Afrika pamoja na wenyeji wa kombe la dunia 2010-Afrika Kusini.

 • Tarehe 27.04.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHcH
 • Tarehe 27.04.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHcH