1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

kombe la Afrika.

30 Januari 2008

Kamerun ina miadi jioni hii na Sudan wakati mabingwa Misri maadui zao ni Chipolopolo-Zambia.

https://p.dw.com/p/CztP

Katika changamoto za Kombe la Afrika la mataifa,jioni hii ni zamu ya timu za kundi C kucheza wakati mmoja:Mabingwa Misri wana miadi na Chipolopolo Zambia mjini Kumasi wakati simba wa nyika-Kamerun wanaumana na mamba wa mto Nile-Sudan huko Tamale.

Mabingwa Misri wanatarajiwa kukata tiketi yao ya robo-finali ambako tayari Ivory Coast,Ghana,Nigeria na Guinea zimeshatangulia na zinawasubiri.

Simba wa nyika –kamerun wanashabaha mbili hii leo:Kwanza Samuiel Eto’o anataka kutia bao lake la 15 ili kuivunja kabisa ile rekodi alioisawazisha majuzi alipotia bao lake la 14 katika Kombe la Afrika. Kwa mabao yake pia Kameroun inatarasjia kukata tiketi ya robo-finali ya kombe hili la Afrika.

Firimbi ikilia tu hivi punde huko Sekondi,mkamerun Samuel eto’o hataona chochote uwanjani isipokua lango la Sudan na Kamerun nzima inategemea mabao yake leo kuikatia tiketi ya duru ijayo.Kwani, kuaga mashindano katika duru ya kwanza kwa simba wa nyika,ni madhambi makubwa kwa mashabiki wake wa afrika.Kamerun iko nafasi ya pili katika ku ndi C ikiwa na pointi 3 baada ya kuirarua Zambia kwa mabao 5-1.

Kocha wa simba wa nyika,mjerumani Otto Pfister, amenukuliwa kusema,

„wachezaji wetu wanaelewa umuhimu mkubwa wa mechi hii mahsusi na sote itaamua vipi heshima yetu.Itatupasa kuwa macho na shabaha yetu ni kushinda tu.“-alisema Pfister.

Ushindi leo utaifungulia mlango kamerun kujiunga na safu ya Tembo wa Corte d’iviore,Black stars-Ghana,Super eagles-Nigeria

Sudan,yaonesha itarudi nyumbani Khartoum,ambako kombe hili lilianzishwa,1957 na kudurusu tena dimba ili kisipite kipindi kingine cha miaka 32 kabla haikurudi katika finali za Kombe la Afrika.Mamba wa mto Nile wameshindwa kuwatafuna maadui zao na wanarudi kutamba katika kanda ya Afrika mashariki na kati ambako imezionea Zanzibar na Ruanda katika kombe lililopita la Challenge Cup.Katika Kombe la afrika la mataifa, Sudan inapokea leo mkono wa buriani na huu si msiba utakaoifika leo pekee Sudan bali hata wenzao wa COSAFA-Namibia,Afrika Kusini na pengine Zambia.

Mabingwa Misri wana pointi 6 kwa 3 za Kamerun na wana miadi leo na chipolopolo-Zambia huko Kumasi.Misri inahitaji pointi 1 tu kutoka kapu la Zambia kusonga mbele katika njia ya kutetea taji lake ililoshinda nyumbani miaka 2 nyuma.

Mali jana iliaga Kombe la Afrika ikifuata nyayo za Benin,iliolazwa na Nigeria.Stadi wake maarufu Freddie Kanoute amesema anazingatia kustaafu katika timu ya taifa baada ya Mali kupigwa kumbo nje ya mashindano haya.Mali jana ilizabwa mabao 3-0 na Ivory Coast baada ya Didier drogba kutia bao la kwanza kuadhimisha mara ya 50 kuvaa jazi ya taifa.Kanoute amearifu kwamba ataufikiria uamuzi huo baadae.

Ijumaa hii,Freddie Kanoute,ni mmoja kati ya mastadi wanaoweza kutangazwa wachezaji bora wa mwaka wa dimba wa Afrika.