1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kizazi njia panda - awamu ya kwanza

26 Juni 2014

Bongo Academy ni shule ya fahari. Ni shuleni hapo wanapokutana nyota wa mchezo huu Mercy, Trudy, Dan na Niki - vijana wanne wanaotoka kwenye mazingira na matabaka tofauti. Na wala hawajui changamoto zinazowasubiri.

https://p.dw.com/p/1BdwO
Crossroads Staffel 1
Picha: DW

“Nimesimama kwenye njia panda, nikijaribu kuwa jasiri. Nigeukie wapi? Natokea wapi?'' Mashairi haya ya muziki wa Rap katika mchezo wa kuigiza wa “Kizazi Njia Panda”, yanaonyesha ukweli wa mambo. Yametolewa na mmoja wa vijana waigizaji kwenye mfululizo wa vipindi vipya vya Noa Bongo Jenga Maisha Yako, kueleza hali ngumu wanayokutana nayo vijana wa Afrika kila siku wanapochukua maamuzi kuhusu mkondo upi wa maisha wanapaswa kuufuata.

Wasikilizaji wanapata fursa ya kuwafahamu nyota wapya wa mchezo huu wa redio, Mercy, Trudy, Dan na Niki kwenye vipindi vyote 26 vya awamu mbili za mchezo huu. Wote wanakutana shuleni, japo wanatoka kwenye mazingira tofauti ya jamii. Wasikilizaji wanafuatilia maisha yao ya kila siku, wanapofanya maamuzi ya hatma ya maisha yao.

Mchezo wa “Kizazi Njia Panda” unawapa motisha wasikilizaji vijana kujadili na kutafakari yote waliyoyasikia na waliyoyashuhudia. Kwa mara ya kwanza kabisa, kupitia mkanda wa video kwenye mtandao wa Noa Bongo Jenga Maisha Yako, wasikilizaji wanapata fursa ya kuona picha halisi ya hisia za washiriki wa mchezo huu kuhusu yale yanayoelezewa kupitia mchezo wa redio. Ujumbe wa Mercy, Trudy, Dan, Niki na wengineo, unaonyesha nia njema- kama inavyoelezewa kwenye wimbo wao, mwishoni mwa mchezo huu: Tunaweza licha ya hali ngumu, maisha yetu yamo mikononi mwetu!

Awamu ya Kwanza:
Maamuzi magumu yanayotukabili

Hatimae Mercy amepata msaada wa masomo kujiunga na shule ya sekondari ya Bongo Academy, inayosifika nchini mwao. Hiyo ni kama ndoto kwa msichana huyu mwenye miaka 15 anayeishi mtaa wa mabanda. Maisha ni magumu nyumbani kwao. Mama yake anatarajia kujifungua mtoto mwengine huku wadogo zake wawili wakipelekwa kuishi na shangazi yao aliyejitolea kuwatunza - lakini je, atatimiza ahadi hiyo?

Trudy, rafiki mpya wa Mercy, anajaribu kumsaidia kuyazoea mazingira ya maisha mapya shuleni Bongo. Lakini ushawishi wake una athari gani? Matatizo yanaanza pale vijana wawili wanapompenda Mercy. Wanafunzi wenzake, Dan na Niki wote wawili wanajaribu kumtongoza Mercy, lakini mmoja wao ndiye anayemvutia Mercy…

Niki anatokea kwenye familia yenye uwezo wa kadri. Na baada ya kuteuliwa kuwa kiranja wa darasa lao, anaona kuwa hii ni fursa nzuri kabisa ya kuwafurahisha wazazi wake. Lakini hii ni kinyume kabisa na Dan. Nyumbani kwao nchi jirani, aliwakosesha usingizi wazazi wake, ndio maana wakampeleka shuleni Bongo, atakapopata elimu bora zaidi. Kulingana na mipango ya wazazi wake, anatarajiwa kurithi biashara zao...


Mercy, Trudy, Dan na Niki wanalazimika kufanya maamuzi magumu, wakati wa muhula wa kwanza - maamuzi ambayo huenda yakabadilisha kabisa maisha yao.

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi

Gundua zaidi

Onesha taarifa zaidi