1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiwingu bado chatanda Marekani

Admin.WagnerD2 Oktoba 2013

Mkwamo wa kisiasa katika bunge la Marekani haujaonyesha dalili yoyote ya kupatiwa ufumbuzi, na kuziacha shughuli za serikali ya nchi hiyo katika hali ya kusahaulika.

https://p.dw.com/p/19sgs
Watalii wakiwa karibu na kibao kinachotangaza kufungwa kwa mnara wa Uhuru, kufuatia kufungwa kwa sehemu ya shughuli za serikali.
Watalii wakiwa karibu na kibao kinachotangaza kufungwa kwa mnara wa Uhuru, kufuatia kufungwa kwa sehemu ya shughuli za serikali.Picha: Reuters

Kushindwa kwa bunge hilo kupitisha bajeti ya serikali, kumewaathiri maelfu kwa maelfu ya wafanyakazi na makampuni, huku rais Barack Obama akilaazimika kukatiza ziara yake nchini Indonesia. Kukatika kwa ufadhili kwa sehemu kubwa ya serikali kulinza jana Jumanne wakati jitihada za chama cha Republicans kusimamisha au kuchelewesha utekelezaji wa sheria ya huduma za afya zilipokwamisha upitishaji wa bajeti ya nchi hiyo.

Maelfu warudishwa nyumbani
Viongozi wa Warepublican walikuja na mkakati mpya kujaribu kuifungua tena serikali kwa taratibu, lakini hawakufanikiwa kulishawishi baraza la wawakilishi. Karibu wafanyakazi 800,000, ambao ni theluthi moja ya jumla ya wafanyakazi wote wa serikali ya Marekani wamesimamishwa kazi katika tukio hilo la kusimama kwa shughuli za serikali ambalo ni la kwanza katika kipindi cha miaka 17.

Rais Barack Obama akizungumza katika Bustani ya Rose iliyopo ikulu ya White House.
Rais Barack Obama akizungumza katika Bustani ya Rose iliyopo ikulu ya White House.Picha: Reuters

Lakini hata wakati mashirika mengi ya serikali yalifunga milango yake, ubadilishanaji wa bima za afya, ambao ndiyo kiini cha sheria mpya ya afya ya rais Obama ulikuwa unaendelea, yakipokelewa maombi ya kupatiwa bima ya afya, ambayo itaanza Januari mwakani.

Vita vya Kiitikadi
Akizungumzia hatua ya baraza la wawakilishi ambalo linadhibitiwa na chama cha Republicans kuzuwia kupita kwa bajeti, rais Obama aliwatuhumu Warepublican kwa kile alichokiita vita vya kiitikadi vyenye lengo la kuikwamisha sheria yake ya afya, maarufu kama Obama Care.

"Hili kuliko kitu chochote kingine, linaonekana kuwa ndiyo kile Warepublican wanachokisimamia siku hizi. Najua ni jambo la ajabu kuwa chama kimoja kinaweza kufanya watu kutokuwa na bima ya afya kuwa ajenda yake kuu. Lakini kwa bahati mbya ndivyo inavyooneka.

Na cha kushangaza zaidi, ni kwamba kuikwamishwa serikali yetu, hakutimizi lengo lao," alisema rais Obama wakati akihutubia katika bustani ya Rose iliyoko katika ikulu ya White House.

Obama alisema sheria hiyo ambayo inawahakikishia Wamarekani huduma za afya za gharama nafuu, ilipitishwa na baraza la wawakilishi na katika seneti, na mahakama ya juu ilitoa hukumu ya kuihalalisha kikatiba. Alisema pia sheria hiyo ilikuwa suala kuu katika uchaguzi uliyopita, na kwamba lilishatatulia na kwamba itakuwepo pale kwa kudumu. Alisema kutokana na ufadhili wake, sheria hiyo haijaathiria na ufungaji wa serikali.

Makumbukusho ya Jafferson nayo ilifungwa kutokana na mkwamo uliyosababisha kufungwa kwa shughuli za serikali.
Makumbukusho ya Jafferson nayo ilifungwa kutokana na mkwamo uliyosababisha kufungwa kwa shughuli za serikali.Picha: Reuters

Afuta ziara nchini Malaysia
Jumanne jioni, wabunge wa Republican katika baraza la wawakilishi walijaribu kupitisha sheria yenye lengo la kufungua baadhi ya idara za serikali kama vile mbuga za wanyama, ile ya watumishi wa zamani wa jeshi na ile ya huduma za jiji la Washington kama vile ukusanyaji taka, lakini baraza la Seneti lilikataa pendekezo hilo,na Ikulu ya White House pia iliahidi kuipigia turufu sheria hiyo.

Wakati huo, Waziri mkuu wa Malaysia Najib Razak, amesema leo kuwa rais Obama amefuta ziara yake nchini humo kutokana na mkwamo wa kisiasa uliyosabishwa kufungwa kwa sehemu ya shughuli za serikali. Sasa rais Obama amabye alitarajiwa kuwasilisha hotuba nchini Malaysia tarehe 11 mwezi huu, atawakilishwa na waziri wake wa mambo ya kigeni Johna Kerry.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe,ape
Mhariri: Yusuf Saumu