1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kivumbi cha Ligi ya Mabingwa kuendelea

Bruce Amani
20 Februari 2017

Timu za Uhispania Atletico Madrid na Sevilla, na timu za England Leicester City na Manchester City zinashuka dimbani wiki hii katika hatua ya 16 za mwisho ya Ligi ya Mabingwa

https://p.dw.com/p/2XvRR
Deutschland Bundesliga- Zweitkampf Omer Toprak von Bayer Leverkusen gegen Capixaba von Atletico Mineiro
Picha: picture- alliance/AP Photo/J. Raoux

Atletico Madrid, waliofika fainali mbili kati ya tatu za mwisho za Champions League watakwaruzana na Bayer Leverkusen uwanjani BayArena. Kocha wa Atletico Diego Simeone amelazimika kumwacha nje nahodha Diego Godin ambaye ni majeruhi. Kipa Jan Oblak amepona maumivu ya bega na amesafiri na kikosi.

Katika mpambano mwingine wa kesho, Manchester City itachuana na Monaco nyumbani. City wanalenga kutinga robo fainali kwa mara ya pili katika historia yao, baada ya kucheza katika nusu fainali msimu uliopita. Kocha Pep Guardiola atachunguza hali ya nahodha Vincent Kompany kabla ya kuamua kuhusu kikosi kitakachoanza. Kevin de Bruyne, Leroy Sane, Raheem Sterling, David Silva na Yaya Toure wote wanatarajia kuanza mchezo huo baada ya kupumzishwa mwishoni mwa wiki

Madrid Diego Simeone bei Atletico vs Leverkusen
Atletico Madrid inapigiwa upatu kuizidi nguvu Bayer LeverkusenPicha: picture alliance/epa/J. Martin

Siku ya Jumatano, mabingwa wa Premier League, Leicester City, ambao kwa sasa wanajitahidi kuepuka shoka la kushushwa ngazi, watacheza ugenini dhidi ya Sevilla katika mkondo wa kwanza. Sevilla wameshinda mataji matatu mfululizo ya Europa League na kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa La Liga Uhispania

Juventus, mabingwa wa Italia na ambao walicheza fainalin ya 2015 watasafiri kupambana na Porto mjini Lisbon.

FIFA meeting

Rais wa shirikisho la Kandanda Duniani – FIFA Giano Infantino atakutana na zaidi ya marais 50n wa vyama vya soka barani Afrika katika mkutano wa kilele ambao sio wa kawaida kabisa mjini Johannesburg wiki hii.

Kila mwanachama wa nchi 54 za bara hilo amealikwa katika mkutano huo wa siku nzima, ulioitishwa kujadili masuala ya jumla katika mchezo wa kandanda na kufafanua mipango ya FIFA ya kutanua timu zitakazoshiriki katika Kombe la Dunia pamoja na mabadiliko katika miundo yake ya maendeleo. Marais wa vyama vya kandanda Afrika watagawanywa katika makundi mawili ambapo 25 watakutana na Infabtino na maafisa wengine wa FIFA kesho Jumanne, na kundi jingine kufanya hivyo Jumatano. Ni mara ya kwanza mkutano wa aina hiyo kuandaliwa ambapo FIFA inazungumza moja kwa moja na viongozi wa kandanda la Afrika.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman