1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kituo cha ARD na taarifa za shambulio la Kunduz

Kabogo Grace Patricia22 Desemba 2009

Kituo hicho cha utangazaji kimepata taarifa za siri kuhusu shambulio lililofanywa Afghanistan, Septemba mwaka huu.

https://p.dw.com/p/LAIw
Waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier.Picha: AP

Kituo cha utangazaji cha umma cha ARD nchini Ujerumani kimepata taarifa za siri zinazozusha maswali juu ya nani alijua nini kuhusu shambulio la anga katika eneo la Kunduz, Afghanistan, Septemba mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 142.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ujerumani ilitaarifiwa ndani ya muda wa masaa manne baada ya Ujerumani kutoa amri ya kutekelezwa shambulio hilo, linalodaiwa kuwaua raia kadhaa.

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wakati huo, Frank Walter Steinmeier, sasa yuko katika shinikizo la kutakiwa aeleze kwa nini wiki iliyopita alisema kuwa hali ya mambo haikujulikana kwa muda wa siku nne baada ya shambulio hilo kutokea.

Suala hilo hadi sasa limesababisha aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Franz Josef Jung pamoja na maafisa wawili wa ngazi ya juu wa jeshi la Ujerumani kujiuzulu.