1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kitisho cha vifo zaidi katika maeneo ya mafuriko

17 Agosti 2010

Umoja wa Mataifa hii leo umeelezea wasiwasi wake kuhusu hali mbaya za afya zinazozidi kuhatarisha maisha ya watu katika maeneo yaliyoathirika na mafuriko nchini Pakistan.

https://p.dw.com/p/Open
In this photo provided by the United Nations, an aerial view of the flooding in the province of Punjab, near the city of Multan in Pakistan, is shown Sunday, Aug. 15, 2010. U.N. Secretary General Ban Ki-moon said Sunday he has never seen anything like the flood disaster in Pakistan after surveying the devastation and urged foreign donors to speed up assistance to the 20 million people affected. (AP Photo/United Nations, Evan Echneider)
Eneo lililofurika katika jimbo la Punjab.Picha: AP

Wakimbizi milioni 20 wanaishi kambini au sehemu zilizo wazi na wanakosa chakula au maji safi ya kutosha. Ripoti za magonjwa yanayoambukizwa kutokana na maji machafu kama tumbo la kuharisha na magonjwa ya ngozi zimekuwa zikiwasili kutoka kwenye makambi hayo.

Dr.Abdulla Assaedi naibu mkurugenzi wa kanda, wa Shirika la Afya Duniani(WHO) amesema, inatrajiwa kuwa idadi ya wagonjwa itaongezeka, halikadhalika vifo.Kwa mujibu wa daktari huyo, mafuriko yameharibu au yameangamiza asilimia 20 ya vituo vya afya vya taifa na wafanyakazi 30,000 wa huduma za afya wameathirika.

Mvulana wa miaka minne amefariki kambini kutokana na magonjwa ya tumbo katika mji wa bandari wa Karachi kusini mwa Pakistan na mvulana wa miaka sita amepoteza maisha yake kutokana na pepopunda.

Afisa wa matibabu Khalid Ansari amesema, timu yake imebaini watu 400 wakiwa na homa kali na magonjwa ya tumbo-wengi wao wakiwa ni wanawake, watoto na wazee. Ameongezea kuwa magonjwa ya ngozi pia ni mengi.

Wakati huo huo,maafisa wa serikali wanasema,msichana wa miaka 17 amefariki kutokana na magonjwa ya tumbo katika hospitali ya wilaya huko Rajanpur mji ulioko katika jimbo la kati la Punjab ambalo limekumbwa na mafuriko makubwa.

Hii leo, Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF limesema kwamba mamilioni ya wanawake na watoto wako hatarini kuambukizwa magonjwa. Daniel Toole mkurugenzi wa kanda wa shirika hilo, amesema kuwa nchi hiyo ina magonjwa sugu ya kuharisha, ya kipindupindu na magonjwa sugu ya mapafu. Kwa maoni yake, hali hiyo itasababisha matatizo kuzagaa katika maeneo hayo.

Mafuriko hayo yaliosababishwa na mvua kubwa za masika wiki mbili zilizopita, hadi sasa yameuwa watu 1,400, yamezamisha asilimia 20 ya ardhi ya nchi hiyo na yameangamiza nyumba na mamia ya barabara na madaraja kadhaa.

Umoja wa Mataifa umetowa wito wa kupatiwa dola milioni 460 kuwasaidia angalau watu milioni sita - lakini nchi hiyo itahitaji mabilioni ya dola kwa ajili ya ujenzi mpya.Hadi sasa Umoja wa Mataifa umepokea dola milioni 160 tu kati ya michango iliyoahidiwa.

Mwandishi:P.Martin/DPA/RTRE

Mhariri:Charo,Josephat