1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kisa cha rushwa dhidi ya Waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert cha pamba moto.

28 Mei 2008

Kiongozi wa Leba Ehud Barak kuitisha mkutano na waandishi habari

https://p.dw.com/p/E7W1
Waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert.Picha: AP

Waziri wa ulinzi wa Israel Ehud Barak ameitisha mkutano na waandishi habari leo,pakizuka fununu kwamba huenda akamtaka Waziri mkuu Ehud Olmert ajiuzulu baada ya mfanya biashara mmoja wa kimarekani kutoa ushahidi katika kesi ya rushwa dhidi ya Waziri mkuu huyo.

Chama cha Bw Barak cha Leba ni mshirika mkuu katika serikali ya mseto inayoongozwa na Bw Olmert, na bila shaka huenda uchaguzi mpya ukalazimika kuitishwa, hali itakayovuruga mwenendo wa mazungumzo ya amani kati ya Israel na Wapalestina.

Mbunge mmoja wa ngazi ya juu wa Leba Danny Yatom alisema ama Bw Olmert anajiondoa mwenyewe au Leba kijitoe serikalini, matamshi yanayoashiria kwamba huenda Bw Barak akatoa dai hilo hilo katika mkutano huo na waandishi habari baadae leo.

Mfanyabiashara wa kimarekani Morris Talansky mwenye umri wa miaka 75 alitoa ushahidi jana kwamba alimpa Bw Olmert dola 150.000 ndani ya bahasha, kama mkopo binafsi fedha ambazo hakuzilipa ,zaidi ya miaka 15 iliopita kabla mwanasiasa huyo mkongwe hakuchaguliwa kuwa kiongozi wa Israel.

Bw Olmert ambaye mawakili wake watamhoji Bw Talansky mwezi Julai amekiri alipokea fedha hizo kutoka kwa mfanyabiashara anayeishi mjini Newyork Marekani, lakini akasema zilikua ni mchango halali kwa ajili ya kampeni ya uchaguzi. Akikana kwamba ametenda kosa,alisema pamoja na hayo atajiuzulu ikiwa atashtakiwa

Kwa mujibu wa katiba ikiwa Olmert atajiuzulu, Rais Shimon Peres anaweza kumteuwa mwanasiasa mwengine kuchukua nafasi yake, baada ya kushauriana na viongozi wa vyama vinavyokilishwa bungeni.

Anayepewa nafasi ya usoni zaidi ni waziri wa mambo ya nchi za nje Bibi Tzipi Livni ambaye pia ni mjumbe mkuu katika mazungumzo ya amani na wapalestina, ambayo Marekani inamatumaini yanaweza hadi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu kufikia makubaliano juu ya kuundwa taifa la wapalestina, ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Ikiwa Bw Olmert mwenye umri wa miaka 62 atalazimika kukaa kando kwa muda wakati waendesha mashtaka wakiendelea na kesi ya rushwa dhidi yake, Bibi Livni akiwa naibu waziri mkuu atachukua hatamu za uongozi kwa siku 100 za kipindi cha mpito.

Kuna tetesi kwamba kiongozi wa chama cha Leba Bw Barak anazingatia uwezekano wa kuunda serikali ya dharura na chama cha mrengo wa kulia cha Likud cha Benjamin Netanyahu na kukiacha kando kile cha Kadima cha Bw Olmert.