1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa upinzani DRC afungwa jela

Admin.WagnerD29 Desemba 2016

Upinzani umeonya kuwa mashtaka dhidi ya viongozi wa upinzani na wanaharakati wanaompinga Rais Kabila yanaweza kusababisha kuvunjika kwa mazungumzo yanayoendelea. Upinzani umetaka baadhi ya kesi hizo kufutiliwa mbali.

https://p.dw.com/p/2UzlG
Kongo | Präsident Joseph Kabila
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Mahakama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imemhukumu kiongozi mmoja wa chama cha upinzani kifungo cha miaka mitano gerezani. Hayo ni kwa mujibu wa kundi moja linalotetea haki za binadamu nchini humo. Wakati huo huo, watu 50 wamekufa kutokana na mafuriko nchini humo.

Mahakama hiyo imempata kiongozi wa upinzani Frank Diongo na hatia ya kuwazuilia wanajeshi watatu kinyume na sheria wiki iliyopita wakati wa maandamano na ghasia jijini Kinshasa, ambazo zilisababisha vifo vya raia kadhaa. Hayo yamesemwa na Georges Kapiamba, wakili na mtetezi wa haki za binaadamu ambaye alihudhuria kesi hiyo.

Frank Diongo ambaye ni mkuu wa chama cha upinzani cha MLP, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa hakuweza kujitetea mahakamani kwa sababu za hali ya kiafya lakini akataja hukumu hiyo kuwa ya kisiasa. Hata hivyo serikali imekana kuwa hukumu hiyo ilitolewa kufuatia ushawishi wa kisiasa.

Mashtaka yanatishia mazungumzo

Hukumu hiyo inajiri wakati wawakilishi wa upinzani wa Rais Joseph Kabila wakisema wanakaribia kufikia makubaliano yatakayomwezesha kiongozi huyo kuondoka madarakani ifikapo mwishoni wa mwaka 2017, hiyo ikiwa baada ya uchaguzi wa rais mpya.

Viongozi kadhaa wa upinzani na wanaharakati wanaompinga Kabila wamekamatwa tangu mwaka uliopita kwa kile wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wanataja kuwa njama za kisiasa, huku upinzani ukitaka baadhi ya mashtaka hayo kutupiliwa mbali.

Waandamanaji mjini Kinshasa
Waandamanaji mjini KinshasaPicha: DW/W. Bashi

Mapema wiki hii, kiongozi mkuu wa wawakilishi wa upinzani Felix Tshisekedi, alisema mazungumzo yanaweza kuvunjika kufuatia mashtaka dhidi ya Diongo na viongozi wengine wa upinzani. Nikimnukuu alipohojiwa na shirika moja la habari nchini humo, Tshisekedi alisema ''Tunatoka katika uchokozi mmoja hadi mwingine. Ikiwa hali hii itaendelea, hatutaisaini mkataba.''

Uchaguzi wa DRC ulipaswa kufanyika mwezi uliopita, lakini serikali iliuahirisha hadi Aprili mwaka 2018 ikisema shughuli ya kuwasajili mamilioni ya wapiga kura imechelewa. Upinzani unamlaumu Kabila kwa kujaribu kusalia madarakani, madai ambayo Kabila amekataa.

Mafuriko yawaua watu 50

Kando na hayo, mvua nyingi ambazo zimenyesha katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuanzia mapema wiki hii zimesababisha mito kuvunja kingo hivyo kutokea kwa mafuriko ambayo yamewaua watu 50 kusini magharibi mwa Kinshasa. Gavana wa Jimbo la Kati nchini Kongo, Jacques Mbadu ameliambia shirika la habari la AFP. Ameongeza kuwa shughuli za kutafuta miili zaidi ambayo huenda imezikwa na matope zinaendelea.

Zaidi ya watu,10,000 wameachwa bila makaazi baada ya nyumba zao kufurika maji karibu na mji wa Boma karibu na mpaka wao na Angola. Meya wa mji huo Marie –Jose Nsuami amesema na kuongeza kuwa jopo la dharura limeundwa kuwasaidia waathiriwa

Mwandishi: John Juma/AFPE/RTRE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo